Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mhe. Festo Mgina, akizungumza wakati wa kufunga kikao cha Baraza la Madiwani.
Sehemu ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wakifuatilia Mjadala wa bajeti.

Na Afisa Habari Mufindi.
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi limejadili, kuridhia na kupitisha rasimu ya bajeti yenye zaidi ya shilingi bilioni 62.926, ikiwa ni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ujao wa Fedha 2018/2019, ambapo makusanyo ya ndani ya Halmashauri ni Bilioni 4.162 kati ya Fedha zote.

Akiwasilisha rasimu ya bajeti kwenye kikao maalum cha Baraza, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Isaya Mbeje, amesema, Halmashauri inatarajia kukusanya, kupokea na kutumia zaidi ya Bilioni 62.926, ambapo kati ya Fedha hizo Bilioni 40.728 ni Fedha kutoka Serikali kuu maalum kwa ajili ya mishahara ya Watumishi, Bilioni 17.205 zimeelekezwa kwenye Miradi ya Maendeleo huku Bilioni 4.992 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Mbenje ambaye pia ndiye Afisa Mipango wa Halmashauri, amevitaja vipaumbele vya bajeti hiyo kwa mwaka wa Fedha wa 2018/2019 kuwa inaangazia ukamilishaji wa miradi ambayo haikukamilika kwa miaka ya nyuma hususani ukamilishaji wa Majengo ya sekta ya Afya na Elimu, Ukarabati wa Madarasa chakavu ya baadhi ya Shule za Msingi, ukusanyaji Mapato kwa njia ya kielekroniki, Kutoa huduma bora za kijamii, kuinua uchumi wa wananchi na kuimarisha Miundombinu.

”Mhe Mwenyekiti rasimu hii ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri ni Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/2019, rasimu hii itaendelea kujadiliwa na kupatiwa ushauri kwenye vikao vya ngazi ya Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI Pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge” alibainisha Bw. Mbenje.

Azungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi ambaye pia ndiye Diwani wa kata ya Mninga Mhe. Festo Mgina, amewataka Madiwani kutoa ushirikiano kwenye zoezi la ukusanyaji wa mapato pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapoto ili yasaidie kuharakisha maendeleo kwa kuzingatia kuwa asilimia 60% Mapato ya ndani yanatakiwa kuelekezwa kwenye miradi ya Maendeleo.

“Mkurugenzi wewe pamoja na timu yako tuendelee kuchapa kazi, tunasifa ya Ushirikiano kati ya timu ya Madiwani na Timu yako, tuendeleee kufanya kazi kwa umoja, uadilifu na ushirikiano Kwani sisi kama Viongozi tunatakiwa kuwa chachu ya Maendeleo”

Rasimu ya bajeti ya 2018 – 2019, aimeandaliwa kwa kuzingatia, Ilani ya Chama cha tawala CCM, Mwongozo wa bajeti wa mwaka 2018/2019, Mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2017, Malengo 17 ya maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa pamoja na mpango mkakati wa miaka 05 wa Halmashauri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...