Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameziagiza DAWASA na DAWASCO kuhakikisha zinafikisha huduma ya maji kwenye maeneo yaliyo pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam, ambapo kuna uhaba mkubwa wa maji pamoja na kuwa na wakazi wengi zaidi na si kujikita katikati ya jiji hilo tu.
Naibu Waziri Aweso ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kikazi katika Wilaya ya Temeke kujionea uhalisia wa utekelezaji wa miradi ya maji, wilaya ambayo imekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na huduma hafifu ya majisafi  na salama.
Aweso amesema kuwa kuna haja ya DAWASA na DAWASCO kuimarisha huduma ya maji kwenye maeneo ya pembezoni mwa jiji kama Temeke, Kigamboni, Ukonga, Mbagala na Segerea ili kukidhi mahitaji makubwa ya maji kwa wakazi wengi wanaoishi maeneo hayo.
''Fanyeni utaratibu wa kukarabati miradi ya zamani kama hatua ya kwanza na ya haraka ya kuwapatia wananchi maji, wakati mkiendelea kutekeleza miradi mipya na mikubwa ambayo utekelezaji wake utachukua muda mrefu. Mmejikita sana katikati ya jiji, ambapo kwa sasa huduma hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa. Umefika wakati wa kuwekeza maeneo ya pembezoni kwa sasa, na wakazi hawa nao wafurahie huduma ya maji ya uhakika'', aliagiza Naibu Waziri Aweso.
Aidha, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji alitoa onyo kwa manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam kutowapa kazi wakandarasi wasio na uwezo. Pia, kuchukua hatua stahiki kwa wakandarasi wote wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi, huku akiwahakikishia wakandarasi wote kulipwa fedha zao kwa wakati ili wasikwame katika utekelezaji wa miradi hiyo.
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso (kushoto) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Issa Mangungu walipokuwa kwenye Shule ya Sekondari ya Mbagala Kuu kujionea upatikanaji wa huduma ya maji katika shule hiyo.
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akikagua mradi wa maji wa KIWICA uliopo Kijichi, Mbagala.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akitoa maelezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji Majisafi DAWASCO, Mhandisi Aaron Joseph (mwenye miwani) eneo la Kijichi Mbagala.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...