Na Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na Biashara za Magendo na aina mbalimbali za ukwepaji kodi kupitia Viwanja vya Ndege, Vituo vya Forodha Mipakani, Njia za panya pamoja na Bandari bubu kuacha mara moja vitendo hivyo. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo
Bw. Charles Kichere, hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayebainika kusafirisha bidhaa kwa kutumia njia za magendo na kukwepa kodi ikiwa ni pamoja na kutaifishwa mali zote zitakazokamatwa pamoja na chombo kilichotumika kusafirisha au nyumba iliyohifadhi bidhaa hizo. 
 Taarifa hiyo imesema kwamba, kukwepa kodi ni Kosa la Jinai kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2005 na Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015. Aidha, taarifa hiyo imesisitiza kuwa, ukwepaji kodi husababisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuikosesha Serikali mapato yake halali ya kuimarisha uchumi ambayo yangeiwezesha Serikali kutoa huduma za jamii kwa wananchi wake na kuwepo kwa ushindani usio kuwa wa haki na usawa kati ya bidhaa zinazoingizwa nchini zikiwa zimelipiwa kodi na zile zinazouzwa bila kulipiwa kodi stahiki kutoka nje ya nchi. 
 Vilevile, ukwepaji kodi huhatarisha maisha ya walaji kwa kuingiza bidhaa ambazo hazijathibitishwa viwango vya ubora na usalama wake kupitia mamlaka husika ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). 
Pia, huhatarisha uchumi na usalama wa nchi kwa sababu ya uwezekano wa kuingiza vitu vya hatari kama vile silaha. 
 Taarifa hiyo ya Kamishna Mkuu wa TRA imewaomba wananchi kutoa taarifa ya mfanyabiashara au kampuni yoyote inayojihusisha na vitendo vya Biashara ya Magendo na ukwepaji kodi kwa kupiga simu namba +255 22 2137638 au +255 784 210209.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...