wanablogu wote, kupitia kwa ndesanjo na mtimkubwa mkavu

awali ya yote napenda washukuru kwa ichango yenu mizito ambayo imenigusa sana moyoni. nabofya hii huku chozi lanilenga kwa kuona wengi wanafuatilia blogu hili kiasi hicho. hakika niliaga kwa kutojua ukubwa wa hamasa ilopatikana baada ya kuifungua.

nabofya leo nikiwa nimefikia uamuzi, ila kabla sijausema naomba niwatake radhi wote niliowakera ama kuwasumbua kwa kuaga kule; kama nilivyosema, sikudhani wengi mnapitia blogu hili, nilidhani ni kina nkya na ndesanjo na mark msaki na pengine idya. kumbe ni zaidi.

nawaangukia wote na kuwataka radhi, sikuwa na nia mbaya wala kutaka kutikisa kibiriti, kwani nashukuru mungu huko nishavuka; hivyo chonde, chonde naomba mnipe furaha wote mliochangia na hata ambao hamkuchangia mseme kama mmenisamehe.

kufanya kosa sio kosa, kosa kurudia kosa...

waama, baada ya yote hayo napenda kuwataarifu kuwa leo naenda zenji kwenye tamasha la sauti za busara kwa siku tano, hivyo sintokuwa dar kwa muda. na kwa vile uamuzi wangu ni kwanza kuomba radhi kwa usumbufu wowote ulotokea, na pili ni kutamka rasmi kwamba nimebadili uamuzi (hasa kuzingatia kwanza ushauri wa ndesanjo, kisha nyote mlochangia) kwamba sio tu siondoki bloguni, bali pia nitazidisha juhudi za kazi huku nikitegemea michango ya mawazo ambayo si lazima yawe ya kusifia. naona raha nikikosolewa.

so, i am back!

kwa kudhihirisha hilo, na hata kabla ya kukimbilia gatini kukwea boti kuelekea zenj, naweka picha ilomfanya mwalimu nyerere achukie kwenda mpirani.

hapo ni uwanja wa taifa dar, julai 4, 1972 na huyo ni rais gaffar nimeiry wa sudan akikagua taifa stars iliyokuwa inapambana na timu ya taifa ya sudan, ambapo jukwaani mwalimu nyerere naye alikuwepo. timu yetu iliingia uwanjani vifua wazi kwa vile walikuwa hawana jezi...

toka shoto ni mohamed chuma, omar zimbwe, kitwana manara, kepteni abdulrahman juma na anaetokeza kichwa ni abdallah 'king' kibaden. ingawa stars walishinda 3-0 lakini mwalimu nyerere alikasirika sana kwa kudhalilishwa huko, na toka siku hiyo hajakanyaga tena uwanjani kuangalia kabumbu.

nani wa kumlaumu mwalimu kwa hili? je, mlio ughaibuni mna la kuchangia.

kama nilivyosema: I AM BACK! STAY TUNED!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 24 mpaka sasa

 1. Bora umetusikia Michuzi. nakushukuru kwa usikivu wako na ndio sababu tutaendelea kufuatilia matukio mbalimbali ya Tanzania na ulimwengu kwa ujumla kupitia kamera ya Michuzi. Nimesoma maoni yote 24 ya wanablogu na jinsi walivyokuomba kwa nguvu usiondoke, na wewe ukayakubali jinsi yalivyo,...Cheers!

  ReplyDelete
 2. Ahsante sana Bw. Michuzi kwa uamuzi wako wa busara. Ni kweli hii blogu yako inafuatiliwa na watu wengi sana kutoka pembe zote za dunia. Kazi unayoifanya ni nzuri sana kwani inatuburudisha na kutuelimisha!

  Mungu azidi kukubariki!

  ReplyDelete
 3. Sawa sawa Mambo si Haya bwana, Wewe ndugu yangu endelea kuelemisha jamii kwa nguvu zako zote na kesho utaona mafanikio yake maana kama nilivyo sema website nyingi zilizo endelea zimeanza kama ulivyo anza mfano google, wikipedia.com, amazon na ebay, n.k. ambazo sasa respect na zina thamani kubwa.

  Endelea na kazi ndugu yangu mafanikio utayaona baadae (Mvumilivu ula mbivu).

  ReplyDelete
 4. Bora umebadili mawazo maana wengine tulishaanza kutokwa na machozi.Thank you kwa hii picha ya Taifa Stars.Hawa jamaa walikuwa wazalendo kweli kweli.

  Sir Nyamranga
  Columbus, Ohio

  ReplyDelete
 5. Brother Michuzi,
  kama kuna siku umenifurahisha basi ni leo, kwanza kwa kuonyesha utu uzima wako (najua wewe sio Mjaluo)kwa kukubali kusikiliza maoni ya wengi. Blogu yako inatupa burudani sana tu, ndio maana napenda kutoa shukrani zanguza dhati.

  Dennis Londo-Helsinki

  ReplyDelete
 6. Jamani!

  Mwaka 1972 kama sikosei Waziri wa Utamaduni, Vijana, na Michezo alikuwa Ndugu Chediel Mgonja. Ni kwa amri ya Waziri Mgonja mwaka huo huo 1972 kama sikosei vilabu vya mpira ndipo viliposhurutishwa kubadili majina toka majina ya kigeni kwenda ya Kiswahili. Na moja kati ya vilabu vilivyokumbwa na zoezi hilo ni wekundu wa Msimbazi ambao walisilimishwa jina la Simba toka Sunderland.

  Sasa hapa nastaajabu kwamba mwaka huo huo 1972 timu ya taifa ikaingia uwanjani bila jezi mbele ya Marais Nyerere na Rais Nimeir. Haya ni moja ya mambo yanayokerehesha sana. Hayati Rais Nyerere akakereheka kiasi kwamba akasusia kandanda! Ninaona kususia kandanda halikuwa suluhisho. Suluhisho lilikuwa ni kutafuta kwa nini timu iliingia uwanjani bila jezi? Nani alikuwa anawajibika kuipatia timu jezi? Na kwa nini hakuipatia timu jezi? Halafu yangepatika majibu ya maswali haya tatizo lingetafutiwa suluhisho la kudumu na kama kulikuwa kuna mzembe au muhujumu anahusika basi angechukuliwa hatua kali za kisheria.

  Hii picha inanikumbusha tena kuhusu "Kesi ya cheki ya Lagos" Nakumbuka timu yetu iliposhiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho tangu michuano hii ilipoanzishwa mwaka 1957 katika fainali za kombe la mataifa huru ya Afrika mwaka 1980 yaliyofanyika mjini Lagos, Naijeria. Jamani, naisikia sauti ya Ahmed Jongo inapiga kelele masikioni mwangu kutokea radioni ikitokea uwanja wa Dag Hammarskjold, Ndola Zambia "..Peter Tino anatupatia tiketi ya kwenda fainali Lagos.. Rais Kenneth Kaunda anafuta machozi.." Hili lilikuwa pambano la marudiano uwanja wa ugenini kwa hiyo matumaini ya kumshinda mcheza kwao yalikuwa finyu. Nakumbuka pambano la kwanza lilichezewa nyumbani pale Temeke Neshino, Stedium. Nakumbuka jezi Taifa Stars za njano na mikato miwili ya bluu kifuani. Nakumbuka saa za usiku tulivyokuwa tunasubiri kuletewa matangazo (live coverage) na RTD toka Lagos, Naijeria. Halafu nakumbuka jinsi walivyoshindwa na kurejea nyumbani vichwa chini. Lakini kwangu mimi na Watanzania wengine wenye mtazamo kama wangu Taifa Stars walikuwa mashujaa.

  Turejee kwenye "Kesi ya Cheki ya Lagos" Kama ilivyo ada ni kwamba timu ikishiriki mashindanoni hupewa pesa zilizopatikana katika michezo hiyo. Taifa Stars hali kadhalika wakalipwa pesa zao za kushiriki kwenye fainali ya kombe la Mataifa Huru ya Afrika kama haya yanayoendelea sasa nchini Misri. Waandaji wa mashindano wakamkabidhi mmoja wa viongozi wa timu ya taifa hiyo hawala ya fedha ya kushiriki michuano. Stafillullah! Kumbe alikuwa kibaka. Akaichikia hiyo hawala ya fedha. Hiyo "kesi ya cheki ya Lagos" Iliwahi kujadiliwa hadi bungeni lakini ng'oh! Hawala haikupatikana wala hakuna aliyeshtakiwa kwa wizi huo. Hili ni jambo la kuhuzunisha sana ukitazama suala hili kwa ujumla wake kihistoria ya Tanzania katika michezo. Ni suala linalogusa michezo, siasa, mfumo wa sheria, na kadhalika, na kadhalika.

  Ndugu zanguni, naona mtiririko wa mawazo unaanza kupandana na ninaogopa nitaandika sana. Sasa hivi nawaona viongozi wazalendo wapenda kandanda kwa moyo wao wote kina Hayati Mzee Tabu Mangara Tabu, Hayati Mwamba Majuto, Hayati Mzee Luhui, James Kassanda, Hamad Kiluvia, Shiraz Sharif, Kocha Paul West Gwivaha, Kocha Shabani Marijani, kocha Tambwe Leya, Kocha Nabii Camara, naiona Taifa Stars ikiwa golini na Juma Pondamali, (2) Daudi Salum, (3)Hayati Mohamed Kajole, (4)Kapteni Leodgard Tenga, (5) Jela Mtagwa(aliyepata kuwekwapicha yake kwenye stempu), (6) Adolph Rishad, (7) (8)Hussein Ngulungu, (9) Peter Tino, (10)?, na (11) Kassim Manara(mchezaji pekee wa Tanzania aliyecheza ligi daraja la kwanza Ulaya na kuwahi kuwa mfungaji wa goli la mwezi).

  Naona nalewa mawazo ngoja niache,

  F MtiMkubwa Tungaraza.

  ReplyDelete
 7. Kuhusu suala la JK (RIP)kukasirika kwa sababu kudhalilishwa mimi sioni kama lina msingi. Yeye kama kiongoziwa serikali ilimbidi afahamu wawakilishi wa Taifa wanakula nini na wanavaa nini wakati muhimu kama huo. Vinginevyo naona alikuwa nataka kutia kash kash mawaziri wake bila sababu za msingi.

  Dennis

  ReplyDelete
 8. Niliwasahau makocha Hayati Ray Gama, Kocha Joeli Bendera (Waziri Mdogo wa Michezo serikali ya awamu ya nne), Hayati Kocha Samsarov, Rud Guntherdolf, Kocha Mansour Magram, Kocha Vita wa Romania ambaye ndiye chimbuko wa wachezaji wengi wa Pan Africa (Wakali wa Mtaa wa Kongo) mathalani kina Pondamali, Adolf, na wengineo wengi waliotokea Yanga Kids. Najisikia naongea Kiingereza "What went wrong and when with Tanzania soccer?"

  F MtiMkubwa Tungaraza.

  ReplyDelete
 9. Mr mchuzi wewe ndio muhimu hapa,wengi tumekujahapa kwa sababu yako,one of the best ever photographer in africa, na daily news ndio gazeti la kale kupita yote hapo TZ,kutoka office yako tunapata picha za kihistoria,
  binafsi nakuadmire sana pale unapoleta picha za matukio mawili from different location in very short time,, very professional guy.
  we need you here man 4 sure.

  kuhusu hii picha ya kina kibaden king kifua wazi inaonyesha jinsi watanzania enzi hizo walivyokuwa wamejaa uzalendo na utaifa ulivyokuwa mbele,sio siku hizi.inaonyesha tazizo ilikuwa pesa za kununua sare hakuna na wala sio walaji kama waliokaa FAT miaka ya karibuni, kwani vijana hao walikuwa wanajua sabubu ya wao kuwa vitumbo wazi na wakashinda tatu bila. kama wangekuwa wanazulumiwa vipaji vyao kama sasa wasingeshinda. nawapa sana hongeza hao vijana na viongozi wa nyakati hizo.ubadhirfu ulikuwa unaogopwa kama ukoma miaka hiyo, hata wengi mnajua,
  mimi nawashauri watanzania wenzangu kwamba michezo ndio kitu kikubwa sana cha kufanya taifa letu lijulikane kila kona hapa duniani,na wala sio mbuga za wanyama&kilimanjaro& hata hiyo miss tanzania haina lolote,kwani ni watu wachache sana hapa ughaibuni wanajua ma miss america,miss uk, nk ila tukiweza kuweka mchezaji mmoja tu, kwenye premeirship(manchster united,arsenal, ect)au Garbiel selasie, waghaibu wengi watatujua.na vijana wenye uwezo huo tunao na hakika,
  jamani wTZ wenzangu tuweke utaifa mbele/uzalendo ndio siri ya maendeleo. jamjuah

  ReplyDelete
 10. Tehe! tehe! tehe! tehe!
  Angalia hiyo mishababi tumbo wazi lakini ikashinda goli tatu!

  Hakika tunatoka mbali. Mpira zamani ulikuwa upendo na uzalendo. Ingekuwa leo hii hakuna mchezaji ambaye angekubali kucheza.

  Lakini leo napata taswira kwa nini Tanzania tuko nyuma kisoka. Huwezi kumlaumu moja kwa moja Mtakatifu Nyerere isipokuwa watendaji wake hawakuona umuhimu wa soka hata kutomshirikisha. Labda angalishirikishwa hali ya soka isingalikuwa kama ilivyo leo. Yaani hawakuona hata aibu kumkaribisha sokani tena akiwa na kiongozi wa nchi ya nje!

  Kilichomkasirisha Nyerere ni kutoshirikishwa (mawazo yangu). Sasa alikuwa kama amesusa akifikiria wahusika watajirudi (kama Michuzi) na kumshirikisha. Mijamaa ndio kwanza ikafikiri hataki masuala ya soka abadani.They missed a point and soccer plumented as such.

  ReplyDelete
 11. Michipix waweza kutupatia tupicha twa Nelson Mandela na Papa Yohanne wa Pili walipotembelea-ga Bongo mwaka 1990?

  ReplyDelete
 12. akhsante michuzi kurudisha timu kwa nguvu. mungu akubariki. unajua kuna kanuni moja maishani na mimi naiamini. kuwa shughuli yoyote unaifanya ukiwa duniani, usiihesabu kama ni upotezaji wa muda....mfano, angalia watu waliiongoza migomo vyuo kikuu...au kujishughulisha na serekali za wanafunzi...leo wanamake viopngozi wazuri wa taifa e.g.J.K..mimi naamini kuwa tukipewa kazi ya kusafisha sakafu, mimi nikatumia masaa 10, wewe ukatumia masaa 6 mtu akija anaweza kusema tofauti....kila kazi hujenga juu ya nyingine....leo hii michuzi ulikuwa hunijui, nilikusoma tu kwenye magazeti....eti sasa tunawasiliana kama managlobu na pengine marafiki....kaza buti, ndio maisha ni lincon alisema jitume ukisubiri opportunity ikufikie...usikae ukitegemea utakutana nayo...aksante tena kurudi kiwanjani....

  turudi kwa hili la timu ya taifa...ninachojua Mh. J.K. na pengine ndilo ilikuwa ni tatizo ni kukosa mawazo wa wengine nayo yasikike...zaidi ya fikra za mwenyekiti...sasa kama mwenyekiti alisusa kwa ajili ya JEZI si ndio hapo akawapa kina Ndolanga na wengine kugeuza FAT mali binafsi na kusahau kuwa FAT inabeba dhamana ya taifa!! sio huko tu ni hata kwenye urembo kina Braza Lundenga...wote wanachukulia hii kitu kama ni personal property...kinachotakiwa TZ ili tuendelee ni kuwa kila mtu anachofanya kinatakiwa kiwe wazi na ijulikane ni jinsi gani anajenga nchi...iwe ni mtu binafsi au serekali...hakuna kitu kinatakiwa kuwa siri mbele ya jicho la umma/serekali....kikiwa siri basi ni teyari rushwa!!

  fikra nyingi zenye akili za fikra za mwalimu zilisababisha usawa kujengwa katika misingi ya uonevu au kulea umasikini...tunasema nini juu ya wanamuziki wetu e.g. western jazz na wengine kufa masikini wakati kwa uchungu wakisimulia habari za kina dada asha na dezo dezo kupigwa upya kongo? kulikuwa na haja gani ya Mbaraka mwinishehe hukimbilia Kenya kurekodi?? mambo kama hayo na mengine yakaua mfumo wa ajira kupitia secta hizo sisizotambuliwa....matokeo yake ni wazazi kutounga mkono vipaji na uwezo wa watoto wao, kuua masomo ya michezo na sanaa mashuleni....KWANI YA NINI KAMA HAYALIPI KIMAISHA?? SI BORA USOMEE UTAWALA AU FEDHA UKAAJIRIWE SEREKALINI??? J.K junior ana kazi kubwa na wizara ya utamaduni...nashangaa hadi leo hawajazungumzia watapigania vipi hati miliki na ulinzi wa kazi za watu....pia kuitisha wawekezaji wa ndani na nje katika upande huo..........


  aksante

  ReplyDelete
 13. michuzi hukutuonyesha chini, pengine hata ndula ilikuwa zero...walikung'uta ndochi!!

  ReplyDelete
 14. Michuzi,

  Kulaleki, ni vyema umebadili uamuzi wako wa kuondoka.

  Jana nimeshinda kijiweni siku nzima nakusubiri tulijadili suala hili kwa kina na nijaribu kukushawishi usiondoke.

  Bahati nzuri nimechungulia hapa leo naona umeamua kubaki.

  Bomba sana mkuu.

  ReplyDelete
 15. Mark na wengine,

  SANTURI INACHEZA UPANDE WA KWANZA
  Uliyosema ninayaafiki kwa kila hali. Miye kwa sababu ya uchechefu wa msamiati huwa naita kukosa kujua MAANA. Viongozi wa kisiasa wa Tanzania huwa wanaona soka kama mchezo wa wanaume ishirini na mbili wanaokimbizana na kukimbiza mpira kwa dakika 90. Halafu huwa kuna refari akisaidiana na washika vibendera kuhakikisha kwa hawa mashababi ishirini na mbili hao hawaumizani. Kwa hiyo soka kwao ni burudani ya baada ya kazi siku ya Jumamosi kuanzia saa kumi na dakika kumi na tano jioni. Shughuli yoyote ya maana hufanywa asubuhi mpaka adhuhuri, au alasiri, au jioni. Ikiwa ndivyo hivyo basi kwanini wachukue muda wao kumakinikia jambo la dakika tisini tena Jumamosi jioni?!

  NAIPINDUA SANTURI UPANDE WA PILI
  Soka huchezwa na mashababi 22. Kumi na moja toka kila upande. Huchezwa na wachezaji kumi na moja toka kila upande. Wachezaji hao hutumia viungo vyote vya mwili isipokuwa mikono. Huchezwa kwenye eneo la mraba la mita mia nne. Kama ilivyo kawaida ya makundi yoyote yawe ni vyama vya kisiasa, wafuasi wa imani za kidini, na kadhalika huwa yana wafuasi wake hali kadhalika soka. Kwa hiyo Inapochezwa soka huwa si wachezaji ishirini na mbili wanaoshiriki huwa kuna kundi kubwa la mashabiki wa timu hizo wanaoshiriki. Mashabiki hawa huwa pengine wapo uwanjani, au majumbani au vilingeni wakishiriki kwenye pambano kwa kusikiliza radio, au majumbani au migahawani wakitazama pambano kupitia kwenye luninga. Ushabiki wa soka unaweza kuwa ni maradhi mabaya yasiyotibika. Kuna mashabiki wa soka ambao wamewahi kufikia hatua ya kujiua pale timu wanayoishabikia iliposhindwa. Kuna wengine ambao wamepoteza mali zao kwa kualifia (betting) matokeo ya mapambano ya soka. Kuna wengine waliouawa au kujeruhiwa na mashabiki wa timu pinzani. Na wapo waliopoteza urafiki na hata wapenzi kwa sababu ya kushabikia soka.

  Wacheza soka ni wa kulipwa ni watu wanaopata vipato vikubwa kuliko marais, wabunge, na viongozi wengine wa kisiasa, au wanataaluma walioenda kwenye taasisi mbali mbali za elimu kwa miaka zaidi ya nusu ya maisha yao! Soka ni moja ya ajira inayotengeneza mamilionea vijana kwa kazi halisi yenye kipato halisi. Soka ndiyo kazi pekee inayoweza kumlipa mtu asiyejua kusoma wala kuandika mamilioni ya fedha kutokana na uwezo wake wa kulisakata kabumbu.

  Pambano la soka ni shughuli ambayo inaajiri na kutoa vipato kwa njia mbali mbali na kwa watu mbali mbali. Kwa mfano, pambano moja la soka la ligi ya daraja la kwanza huleta vipato kwa wachezaji, wenye njia za usafiri, nyumba za wageni na mahoteli, wenye migahawa ya chakula, kwa makampuni ya vinywaji baridi, makampuni ya habari kama radio, luninga na magazeti, wauza makabrasha(merchandise), makampuni ya usalama na polisi na FFU, wauza petroli na dizeli, makampuni ya umeme, simu, telegramu na kadhalika. Halafu kuna pato kubwa linaloenda ofisi ya kodi mapato. Pato hili huwafaidisha na wananchi wengine ambao siyo mashabiki wa soka!

  Katika somo la sosiolojia kuna kipengele cha sanaa na michezo kama taasisi za jamii. Hiki kipengele kinasema kwamba michezo ni kigezo kinachoonyesha afya, mpangilio (how organised or disorganised), nidhamu, na uwezo kufanya mambo kwa pamoja kwa watu wa jamii inayohusika (coordiantion). Kwa mantiki hiyo na kuwaangalia kina Mohamed Chuma na wenziye wakiwa vifua wazi tunaweza kuijadili vipi jamii yetu ya Tanzania?

  Naona ule ugonjwa wangu wa mawazo kupandana unaanza tena. Akilini imenijia picha ya Mohamed Chuma akiwa na bendera ya Tanzania akizunguka uwanja wa taifa kuaga rasmi kustaafu kucheza namba tatu timu ya taifa baada ya kuitumikia kwa miaka kumi! Namuona Hayati Mohamed Kajole akiirithi nafasi Mohamed Chuma. Namuona Hayati Mohamed Kajole pale ofisi za BIMA Mtaa Samora akiwa mtu mwenye furaha saa zote ulipokutana naye. Inanijia pia picha ya Kocha Mohamed Msomali akiwa kavaa kanzu yake nyeupe karibu na jumba la sinema Sapna, mtaa wa reli Morogoro. Naona ofisi za mamlaka ya tumbaku na wachezaji aliowazalisha Kocha Msomali wakiwemo Charles Boniface Mkwasa, Zamoyoni Mogellah (kama sikosei ndiye mshambuliaji aliyepata kufunga magoli mengi kuliko mwingine yoyote katika historia ya ligi kuu ya Tanzania) Omar Hussein, golikipa Hamad masarakasi, na wengineo. Naliona jiji la Morogoro. Naona makao makuu ya timu ya Mseto, Zaragoza, na Aston Villa. Ninamuona Beki mashuhuri na sanifu sana Kocha Kido Simkoko. Nakumbuka siku nilipoimba na Cosmas Chidumule na kundi zima la wana Matimila ukumbi wa Bwalo Morogoro nilipomaliza kuimba Kocha Kido Simkoko alipokuja kunipa mkono na kuniambia "..Sikujua kama una kipawa cha kuimba, safi sana.." Mawazo yangu hayajakaa sawa, nasikia huzuni.

  F MtiMkubwa tungaraza.

  ReplyDelete
 16. mti mkubwa..ni kweli kabisa uliyosema....nimebwabwaja kimtindo karibu kama huo pale kwenye blogu la nkya....unayosema ni kweli...kama wanavyosema barabara ni mishipa ya nchi (kimuundo) basi michezo ni labda tuite moyo. tatizo pia lililopo kwenye nchi zetu ninavyoona ni mzunguko wa hela. na hili ndio tatizo kubwa la wanyonge wanyonge huwa tunaanzisha biashara lakini hela haipo...wateja wanataka sana kutumia huduma zetu lakini hela imepotea......mchezo huzungusha sana hela..na matukio ya utamaduni kama yangekuwepo...nakumbuka mji kasoro bahari niliwahi kuwa na teksi...kama kuna mechi keshokutwa siku tatu kabla hela inazunguka si kawaida...kipande chako dereva ikifika saa sita kakamilisha....anatafuta cha kwake...mapema tu saa mbili naye amekuwa tajiri....wachilia mbali mahoteli mabaa na kila kitu...kuna haja ya wizara husika kuhakikisha kuwa kila mkoa unakuwa na matournament ya kitosha kila mara ili basi hela izunguke na iwafikie watu...

  ndio maana kitu kimoja huwa najiuliza nikiangalia wenzetu walioendelea....utakuta mtu hana akiba kubwa ya uzeeni, lakini hela anayopata inazunguka kwa njia kama ya kodi na gharama juu za maisha ...na yeye anahakikishiwa malipo uzeeni...mpaka kifo chake...je kuna haja gani ya sisi kukusanya hela mlima na kuzificha ulaya?

  cheers

  sitaki kurudia , lakini

  ReplyDelete
 17. Mark,

  Asante kwa majibu.

  Ulichokisema hapo ndicho ambacho nimekisema lakini kwa uchechefu wa msamiati mimi nimekiita kujua MAANA. Ukijua maana ya jambo unalolifanya basi utalifanya kwa ufasaha wake. Hilo nimeliona na kulielewa wakati nikizagaazagaa huku ughaibuni. Maanake kama ni mnyama kachichwa basi ataliwa nyama na utumbo wake, ngozi yake itatengenezewa mavazi iwe makoti, suruali, viatu, au mikanda, mapembe yatengenezewa urembo na mapambo, mifupa na meno vitatafutiwa shughuli zake. Nikija katika fani ya sanaa na michezo nimeona jinsi wasivyobakisha kitu kuanzia kuuza tiketi za mlangoni, vinywaji, matangazo, burudani, usafiri, umeme, simu, huduma za posta, usalama, wafanyakazi wa kujitolea (volunteers), wafanyakazi wa kulipwa, na kila sekta inayohusika itapata mlo na kipato chake.

  Ukiangalia soko la muziki wa vijana ndiyo utaogopa. Kuna kitabu kimoja kinaitwa modern trends nilikisoma miaka kadhaa iliyopita wakati nikifanya utafiti mmoja juu ya vijana. Ukikipata kitabu hiki ndiyo utajua jinsi wanaojua MAANA wanavyotengeneza uchumi kutokana na jambo lolote lile ambalo linaweza kuingiza kipato na kuunda ajira.

  Mwaka 1998 nilikuwa Manchester, Uingereza. Moja ya vitu nilivyotaka sana ni kuuona uwanja wa MAN UTD na kununua jezi yao. Siku ikapangwa tukaenda kama kundi. Nilipofika uwanjani nilistaajabu kuona mabasi yaliyojaa watalii chungu nzima kutoka nchi mbali mbali za dunia. Jingine lililonitoa jasho ni bei ya hizo ughali wa jezi zilizokuwa zinauzwa kwenye duka la timu. Nikakumbuka jumba la wekundu wa Msimbazi kama hujawahi kuingia mle ndani tafuta siku uingie. Lile jumba mule ndani kama makumbusho kubwa sana nikaiambia nafsi yangu "..Simba na wao wangekuwa na akili kama hii wangeula sana.."

  Kama ulivyosema yatupasa kuanza kushiriki kimatendo katika kuleta hizi hoja kiutendaji. Kwa sababu wengi wa wale waliopo madarakani si kweli kama wanajua sana nini haswa wanachotakiwa kukifanya. Inatakiwa tuwasiliane nao na tueleweshane nao mpaka waelewe MAANA ya kile tunachokisema halafu sote kwa pamoja tukitokee na nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya huku tukijua tunapoelekea. Kwa sababu nguvu mpya, kasi mpya, na ari mpya bila kujua tunapokwenda tunaweza kujikuta tunakwaana kwa kishindo kibaya sana.

  F MtiMkubwa Tungaraza.

  ReplyDelete
 18. nashukuru sana kwa hoja hii...maana yake kuwa nilichodhani ni sahihi na wazee wazima mumeona hivyo hivyo....ni kweli sisi tuliojua maana tusaidie wenzetu kubadilisha mambo...hata kama watatuita wapinzani (rejea bloguni mwangu)..maana siku hizi kama ilivyokuwa zamani challenge zilifananishwa na upinzani. natumaini JK ni mtu mwelewa na akitoa fursa za kushirikisha toka kwa wadau wote ...sio wanaojua maana tu bali walio teyari kutekeleza umaana (kujua na kutekeleza ni vitu viwili tofauti)ni bora anayejua machache akatekeleza yote.....

  imekuwa ni mtindo uliokuwapo miaka mingi watu walio na nguvu kufurahia GAP kati yao na wenzao. GAP si tatizo inategemea mnyonge ana nini na anajimudu vipi maana hata norway na sweden yapo maGAP. walio kwenye nafasi/ wenye nguvu wanawajibika kuwa na wanyonge wanajinyanyua na sio kufurahia kuombwa bia!!!

  namtakieni mwisho mwema wa wiki!

  ReplyDelete
 19. Mti Mkubwa kwa historia ninakuvulia kofia. Safi sana.

  ReplyDelete
 20. F. Mti Mkubwa ulisoma Oysterbay Primary School?

  Kumbukumbu yako ya soka poa sanaaa! I, too, wonder what happened?

  Hiyo listi ya Lagos 1980 umewasahau akina Ahmed Amasha, Leopold "Tasso" Mukebezi, Mohamed?/Ahmed? Salum, bila kusahau mawinga machachari Omari Hussein na Thuweni Ali.

  Naam, mpira siku zile tulikuwa tunajisifia but now......damn!

  ReplyDelete
 21. Oh Michuzi. Safi sana kurudisha timu. Kwenye hii familia ya blogu inakuwa pigo sana tunaposikia mmoja wetu anaondoka. Tunafurahi na kupiga miluzi ya furaha anapoongezeka.

  ReplyDelete
 22. Interesting blog, take a look at mine if you will. http://teazertv.blogspot.com it is all about my favourite website really, Teazer.tv . They have everything that is about pornoif that is your thing.

  ReplyDelete
 23. Asante Michuzi kwa uamuzi mzito wa kubakia. siyo siri blogu yako yako inaongoza zingine zinafuatia. Sijawahi kuipata ya Ndesanjo lakini kwa hoja zake alizokuwa anatoa kwenye gazeti la Mwananchi(shida ya magazeti yasiyoujua mtandao) nadhani nayo itakuwa moto
  Hiyo timu ya soka kama walishindwa kupata fulana kweli walikuwa na viatu. Hebu pekua kwenye rekodi zako utupe hiyo maana inawezekana walikuwa wakimsaidia kuku.

  ReplyDelete
 24. Ni vema umerejea. Pongezi. Blogu yako ni dirisha lituwezeshalo kuona matukio yanoyojiri huko nyumbani.

  ReplyDelete

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...