HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO WA TAASISI YA KUZUIA RUSHWA (TAKURU) MBEYA, 20 FEBRUARI, 2006


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Utawala Bora),
Mhe. Philip Marmo;
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira),
Mhe. Mark Mwandosya;
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Mhe. John Mwakipesile;
Mkurugenzi Mkuu wa TAKURU,
Meja Jenerali Anthony Kamazima;
Viongozi wa Serikali,
Viongozi na Watumishi wa TAKURU.

Kwanza kabisa nawashukuru kwa kunialika kuja kufungua mkutano wa mwaka huu wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa.. Nimekuja hapa leo kujifunza. Meja Jenerali Kamazima anaelewa vizuri moja ya nguzo za uongozi Jeshini kuhusu wakati gani wa kutafuta habari. Moja ya wakati wa kufanya hivyo ni pale unapopewa eneo jipya la kuongoza. Huna budi ulijue vizuri eneo lako kwa kujifunza yote yahusuyo eneo hilo, ufahamu mipaka yake, ujue eneo lako ikoje, uwajue askari wako, ujue uwezo wao na uyajue matatizo yao. Hivyo, niko hapa mbele yenu leo kutimiza wajibu huo wa kiongozi katika vita dhidi ya rushwa.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Watanzania wamenipa ridhaa ya kuwaongoza na niliwaahidi kuendeleza kupambana na Rushwa. Nilisema vile kwa kujiamini kwani nilijua nyie mpo. TAKURU ndio askari wa mstari wa mbele katika vita hii. Mmekuwa mnaifanya vizuri. Naamini tukishirikiana tutapata mafanikio zaidi. Kwa hiyo nimekuja hapa kufanya mambo matatu muhimu. Kwanza kabisa kuwaambia kwamba Serikali ya Awamu ya Nne imeamua kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Nimekuja kuwaambia kuwa nawategemea sana katika mapambano haya. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja nanyi bega kwa bega na nitawapa kila aina ya ushirikiano katika harakati zenu za kupambana na maovu haya katika jamii. Pili, nimekuja kujifunza zaidi kuhusu harakati zenu, mafanikio yenu, na matatizo yenu katika vita hivi. Shabaha yanguhapa ni kutaka tuelewane juu ya njia na mbinu bora zaidi za kuendeleza mapambano haya! Na, tatu nimekuja kuwaeleza matarajio yangu na ya Watanzania kwenu katika vita hivi.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Napenda mwanzoni kabisa mwa hotuba yangu niwashukuru kwa kazi kubwa, na nzuri mnayolifanyia taifa letu. Pia nawapongeza kwa mafanikio mliyoyapa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Nimefurahi kusikia kuwa mmefanikiwa kufungua ofisi karibu katika kila Mkoa na katika Wilaya nyingi hapa nchini. Vile vile, mmeajiri na kusomesha wachunguzi na watumishi wengine wengi na wazuri na hivyo kuimarisha uwezo wenu wa kiutendaji. Pia mmefanya kazi kubwa ya kuelimisha umma kuhusu athari za Rushwa na mbinu za kupambana nayo. Kwa ujumla nimefurahi kuona kiasi gani mmejenga uwezo wa kitaasisi kupambana na rushwa katika mazingira mapya ya sasa. Aidha, nafurahishwa na ushirikiano na mawasiliano mazuri yaliyopo baina yenu na Wizara na Idara mbalimbali za Serikali ambayo yamewezesha utekelezaji wa mapendekezo yenu juu ya mbinu na mikakati ya kupambana na rushwa nchini.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Nawapongeza pia kwa kuandaa Mpango Mkakati (Strategic Plan) wa TAKURU wa miaka mitano ijayo (2006-2011) ambao, pamoja na mambo mengine, unatoa maelekezo ya namna ya kupambana na rushwa kubwa ambazo zina athari kubwa kwa uchumi wetu. Ni matumaini yangu kwamba mtajipanga vizuri kuutekeleza mpango wenu huo kwa nguvu zenu zote. Mimi na wenzangu Serikalini tutakuwa nyuma yenu kuwatia moyo na kuwapa ushirikiano unaostahili.
Vilevile, nimetiwa sana moyo na habari katika taarifa ya Mkurugenzi Mkuu kwamba katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, pamoja na changamoto zinazowakabili, kazi yenu ya uchunguzi na upelelezi katika Wizara mbalimbali imewezesha kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 50 ambazo zingefujwa kwa njia ya rushwa. Hili peke yake, licha ya kazi nyingine nyingi kubwa na muhimu mnazofanya, linatosha kuwanyamazisha wale wenzetu wanaohoji ufanisi wa jitihada zenu na haja ya kuendelea kuwepo kwenu.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Ndugu Washiriki,
Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi kubwa katika juhudi za kupambana na rushwa katika miaka kumi iliyopita. Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa ulitengenezwa mwaka 1999. Sheria mpya za kuimarisha mapambano dhidi ya Rushwa, kama vile Sheria ya Fedha ya 2000 na Sheria ya Manunuzi ya Serikali ya 2000, zilitungwa. Kanuni na taratibu nyingi mpya zilitengenezwa na za zamani ziliimarishwa ili kuleta uwazi na uwajibikaji. Mwanya mkubwa wa rushwa na ufujaji wa mali ya umma ulipunguzwa kipenyo chake. Taasisi ziliimarishwa na nyingi mpya – kama vile TRA na Tanroads – zilianzishwa. Utumishi wa umma uliboreshwa kutoa motisha na kuongeza ufanisi.
Mafanikio ya hatua hizo yalionekana. Mapato ya Serikali yaliongeza na matumizi yalisimamiwa vizuri. Uwazi ukaongezeka na watu wakaanza kuogopa kuomba, kutoa na kupokea rushwa. Hata hivyo, pamoja na juhudi zote hizi, wote tunafahamu kwamba rushwa bado ipo ndani ya jamii yetu. Kiwango cha rushwa ndogo ndogo kinapanda kwa kasi hasa katika mahakama, polisi, ardhi, huduma za afya na sehemu nyingine. Huo ndio ukweli. Kwenye Serikali za Mitaa nako hali sio nzuri. Rushwa kubwa nayo inaongezeka hasa kwenye mikataba na manunuzi ya Serikali. Hali ni mbaya vilevile kwenye shughuli za kisiasa. Imefikia sasa hali ya watu kujenga imani kwamba bila kuhonga mtu hawezi kuchaguliwa kuwa kiongozi. Kwa hiyo changamoto bado ni kubwa, licha ya mafanikio ya miaka kumi iliyopita.
Nyie ndio kikosi cha dafrao katika mapambano haya na ndio wataalam wa kuendesha vita dhidi ya rushwa kisayansi. Nimeelezwa kwamba moja ya mada zenu katika mkutano huu ni mwelekeo wa TAKURU katika kupambana na rushwa kuanzia mwaka huu. Ni matumaini yangu kuwa mtaitumia vizuri fursa ya mkutano huu kuzungumzia na kuelewana kuhusu namna ya kuendeleza mapambano haya kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi siku za usoni. Ningependa kuona kwa namna gani mmejipanga kwa mbinu na mkakati kuikabili rushwa kubwa na rushwa inayowakera wananchi vijijini, mitaani na maofisini.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Tatizo la rushwa lina historia ndefu kwenye kila jamii ulimwenguni kote. Rushwa imekuwepo tangu binadamu walipoanza kuwa na mamlaka na dhamana ya kiutawala na kiuongozi kwa binadamu wenzao. Sio tatizo la Tanzania pekee; wala sio tatizo la Afrika pekee. Rushwa ipo kwenye nchi zinazoendelea na zile zilizoendelea; ipo kwenye nchi za kidemokrasia na za kidikteta. Lakini, kuwepo kila mahali duniani haina maana kuwa ni jambo halali na linalokubalika. La hasha!! Rushwa ni kitu haramu na kisichokubalika.
Chimbuko la rushwa ni tamaa ya baadhi ya watu waliopewa dhamana ya utumishi na uongozi wa umma kutumia mamlaka yao kwa manufaa yao binafsi. Ni matokeo ya mmong’onyoko wa maadili binafsi (personal ethics) wa watu hao kiasi cha kuwafanya wasiogope na wala kujali kabisa kuvunja maadili ya kazi zao na imani ya umma kwao. Kuzidi kuenea kwa rushwa katika jamii ni ishara ya mapungufu katika uwezo wetu wa kitaasisi kuizuia. Pia ni ishara ya kushindwa kwa ushawishi wa kisiasa, kijamii na kidini kwa jamii ili ichukie, ikemee na iikatae rushwa. Mafanikio katika vita hivi yanategemea ushirikiano wa nguvu za kisheria na dola, ushawishi wa kijamii, dhamira ya kisiasa, na uimara wa maadili binafsi na ya jamii.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Rushwa ni kitu hatari sana kwa maendeleo ya taifa letu. Ni dhuluma kubwa kwa haki za jamii. Na kwa wakati huu tunapoelekeza nguvu zetu nyingi katika kuinua uchumi na kuondoa umaskini, rushwa ni kikwazo kikubwa sana. Kisiasa, hasa kwenye chaguzi za viongozi wenye mamlaka ya umma, rushwa inazorotesha ukuaji wa demokrasia. Inawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kwa kuifanya haki hiyo iwe ya watu wachache wenye uwezo wa kifedha. Rushwa inafanya uongozi kuwa kitu kinachonunulika kama bidhaa. Hii inapunguza uhalali wa mamlaka za uongozi na utawala kwa wanaoingia kwa rushwa. Ikiachwa kushamiri rushwa inapunguza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa demokrasia. Kwenye vyombo vya haki rushwa inazorotesha utawala bora na utawala wa sheria. Inahatarisha amani na utangamano wa nchi kwa kuleta dhana kwamba haki inauzwa na haiwezi kupatikana kwa njia ya kawaida. Hatuna budi kuipiga vita rushwa kwa nguvu zetu zote.

Ndugu Mkurugenzi na Ndugu Washiriki,
Rushwa ikikithiri inaweza kuwa hatari kwa usalama wa nchi. Kwa kuwa rushwa ni jambo linalowakera wananchi linaweza kuwafanya wawachukie watumishi wa umma na Serikali yao hasa wanapokata tamaa kwa kushindwa kupata haki, huduma na usalama wao. Wananchi wanaweza kupoteza imani kwa viongozi wao na Serikali yao na hivyo kuvuruga mshikamano, utangamano na utulivu katika nchi. Ikifikia hatua hiyo rushwa inaweza kuwa tatizo la kisiasa na kiusalama. Wananchi wanaweza kubuni na kuanzisha njia na mifumo sanjari na mbadala ya kutafuta haki na kujilinda wao na mali zao. Ushahidi wa hili tunauona kwenye umaarufu wa vikundi vya ulinzi kama vile Sungusungu na kuongezeka kwa vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi (mob-justice). Kwa kutambua ukweli huo na hatari zinazoweza kutokea hatuna budi basi tupambane na rushwa kwa nguvu zetu zote na uwezo wetu wote.
Mapambano dhidi ya rushwa ni vita halali kabisa kwa jamii kupigana na kupata ushiriki. Athari za Rushwa kwa uchumi ni kubwa. Rushwa inapunguza kasi ya kuleta maendeleo kwa vile fedha zinakwenda mifukoni mwa watu badala ya kufanya shughuli iliyokusudiwa ya kuiletea jamii maendeleo. Serikali hupoteza mapato stahiki. Miradi hutekelezwa chini ya kiwango na huduma zitolewazo kuwa za kiwango cha chini au hata kuwa duni kabisa. Rushwa inaongeza gharama ya kufanya biashara. Matokeo yake ni kwamba bei ya bidhaa huwa kubwa isivyo stahili na mzigo hubebeshwa mwananchi. Gharama za kufanya biashara zikiongezeka, kutokana na rushwa, tunatengeneza uwanja wa ushindani wa kibiashara usio sawia/tambarare kwa washindani wote. Kampuni zilizo na washirika kwenye Serikali na vyombo vya mamlaka ya umma – hata kama hazina ufanisi ndizo zinazonufaika. Kampuni ambazo hazina washirika au hazina uwezo wa kugharamia rushwa, na mara nyingi hizi huwa ni zile ndogo, zinashindwa kushindana kwa ukamilifu.
Kutokana na rushwa utendaji wa Serikali na shughuli za umma huyumba . Hadhi ya Serikali mbele ya wananchi hushuka hasa pale sheria na taratibu haziheshimiwi. Unapokuta taratibu za mipango miji, hifadhi ya mazingira, usalama barabarani, na nyinginezo hazifuatwi, dhana hujengeka kuwa Serikali haiko makini katika usimamizi wa ubora wa huduma kwa wananchi.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Kuna dhana potofu kwamba rushwa inarahisisha mambo kwa kuondoa ucheleweshaji (cutting the bureaucratic red-tape). Dhana hii haina msingi kwa sababu wapokea rushwa hujibunia mikakati, sheria na taratibu ndefu za kuongeza ucheleweshaji ili kutengeneza mianya na mazingira zaidi ya kupata rushwa. Na mara nyingi wanaoathirika na mbinu hizi za wapokea rushwa ni wale wanyonge wasio na uwezo wa kutoa rushwa.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Nimefurahi kwamba mna mipango na mikakati mizuri ya kupambana na rushwa. Lakini, ukweli ni kwamba ili mfanikiwe, na sisi wengine Serikalini hatuna budi tuchukue hatua za makusudi za kisera na kiutendaji zitakazoongezea nguvu juhudi zenu. Ningependa kuona kuwa kila kiongozi katika eneo lake awe ndiye kamanda wa vita hiyo pale alipo. Waziri afanye hivyo na Katibu Mkuu pia. Hali kadhalika Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wengineo wote wafanya hivyo. Naamini tutapata mafanikio ya kutia moyo.
Moja ya aina ya rushwa yenye kero kubwa kwa wananchi wa kawaida ni ile yakutakiwa kumlipa chochote “kitu kidogo” mtumishi wa umma ndipo apate huduma. Mtu kuambiwa “sijaamka leo” au “mkono mtupu haulambwi” ni dhuluma na inakera sana. Ni kweli kwamba kishawishi kikubwa cha rushwa hii inawezekana kuwa kipato kidogo kwa watumishi wa umma. Jawabu lake kwa kiasi kikubwa linawezekana kuwa ni kuongeza kipato cha watumishi wa umma. Niliahidi kulishughulikia suala hili. Ni makusudio yangu kuwa miezi michache ijayo niunde tume ya kuangalia maslahi ya watumishi wa umma. Lakini kama kwa watumishi wala rushwa imeshakuwa ni hulka ya kuomba na kupokea rushwa inawezekana kabisa kuwa hatua hizo hazitasaidia. Huenda ndiyo kwanza wakapandisha dau.
Ndiyo maana basi hatuna budi kulitazama suala hili kwa mapana zaidi. Tubane mianya ya rushwa na tuzidishe mapambano. Sisi, kwenye Serikali Kuu na Serikali za Mitaa lazima tuongeze uwezo na ubora wa utoaji huduma na kuhakikisha kuwa kuna haki na usawa kwenye upatikanaji wa huduma. Tusimuonee haya anayefanya kinyume cha hayo. Wakati mwingine rushwa inatokana na wananchi wenyewe kutokuzifahamu haki zao. Tukiongeza juhudi kwenye elimu ya uraia na kuwahamasisha wananchi kuchukia na kukataa kutoa rushwa tutapiga hatua. Naomba nyie wenzetu mtusaidie kwenye hili. Najua mmefanya kazi nzuri katika kutoa elimu kwa umma. Naomba muendelee. Elimu haina mwisho na elimu kuhusu mapambano haya haina ukomo.
Natambua pia kuwa mmefanya jitihada kubwa katika kupambana na rushwa ndogo ndogo. Tuwe wakali zaidi katika mapambano hayo. Pasiwepo na kulegeza uzi. Mtandao wa ofisi zenu mpaka kwenye ngazi ya wilaya pamoja na elimu kwa umma vimesaidia. Lakini, changamoto kubwa iliyoko mbele yenu ipo kwenye rushwa kubwa kubwa na rushwa nono nono. Kwa muda mrefu sasa TAKURU imekuwa ikilaumiwa kwa kushughulikia rushwa ndogondogo inayohusisha watumishi wa vyeo vya chini. Mara nyingi uongozi wa TAKURU umekuwa ukijibu na kuelezea ugumu na muda mrefu unaotakiwa kupata ushahidi wa rushwa kubwa kubwa. Maelezo kwamba rushwa ni rushwa tu, hata kama ni ndogo na yale ya ugumu wa kupata ushahidi wa rushwa kubwa kubwa hayajawaridhisha wananchi walio wengi. Watu wanataka kuona tatizo hili linashughulikiwa ipasavyo kwani rushwa kubwa kubwa ndizo zinazodumaza maendeleo.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Natambua kwamba, taasisi yetu imekuwa na kazi kubwa ya kujiunda upya na kujijenga upya kwa watu, ujuzi, stadi, dhamira na nyenzo kukabiliana na rushwa kubwa. Kwa miaka kumi iliyopita mlikuwa mkifungua ofisi mikoani na wilayani, mmekuwa mkiajiri na kusomesha watumishi wenu. Kwa ujumla mmekuwa mkijijenga kimiundombinu na kitaasisi. Naamini kazi hiyo imefanyika vizuri, nawapongeza. Naomba sasa muazimie kwamba miaka mitano ijayo itakuwa ni ya kuonesha matunda ya kazi yenu, ya kujipanga kwenu.
Tumieni mkutano huu kuangalia ni namna gani mtaboresha mbinu na maarifa yenu katika kupambana na rushwa hizi kubwa vilivyo. Hayo ndiyo matumaini yangu kwenu na ndiyo matumaini ya Watanzania wenzetu wote wenye nia njema na nchi yetu.
Mkurugenzi Mkuu,
Naomba nitaje maeneo kadhaa ambayo nadhani itakuwa busara kuyatilia mkazo katika mipango yenu.
Tayari nimetaja rushwa katika mikataba. Kadhalika nimeshaelezea, Bungeni, nia yangu ya kutaka kuangalia upya taratibu za kuingia mikataba zinazotumiwa na serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kubaini mianya ya rushwa na kuongeza uwazi na uwajibikaji ili kulinda maslahi ya umma. Naomba TAKURU isaidie katika zoezi hili na kuishauri Serikali juu ya mapungufu yaliyopo katika taratibu zilizopo sasa ili yarekebishwe.
Katika zoezi hili, msisahau kuangalia pia michakato ya majadiliano, viwango vya utekelezaji, muda wa utekelezaji, kuhusika au vinginevyo kwa mamlaka za udhibiti wa utekelezaji (regulatory agencies) na hatua sahihi za kuchukua endapo masharti ya mikataba yatavunjwa.
Ni jukumu lenu TAKURU kutumia ujuzi wenu kubaini mapema mikataba batili au ile isiyokuwa na manufaa kwa taifa na kuishauri serikali ili ichukue hatua zinazostahili kabla fedha na mali havijapotea. Kinga ni bora kuliko tiba.
Eneo la pili lenye tuhuma ya kuwa na mianya ya rushwa kubwa kubwa ni la manunuzi/ununuzi (procurement/purchases) Serikalini. Sina budi kukiri kuwa Sheria ya Manunuzi na taratibu nzuri na rahisi za ununuzi zilizowekwa zimesaidia sana kupunguza ukubwa wa kipenyo cha mwanya wa rushwa katika eneo hili. Hata hivyo bado kuna maneno yahusuyo upendeleo, mgawanyo usio sawa, kutokuwepo uwazi wa kutosha wala ushindani halisi kwa kuwa washindani wengine hupewa habari za viwango vya gharama mapema. Kadhalika kuna madai kuwa ununuzi hauzingatii gharama na ubora wa bidhaa. Kwa ajili hiyo yapo madai kuwa wakati mwingine bidhaa zinapewa gharama za juu zaidi na kama gharama ni za kawaida basi baadhi ya bidhaa hazifikishwi kwa mnunuzi kwa maelewano baina ya wanunuzi na wauzaji. Fedha nyingi za serikali hupotea kupitia mwanya huu wa rushwa. Fuatilieni taratibu za manunuzi na ununuzi serikalini kubaini na kuziba mianya ya rushwa katika eneo hili nalo. Nia yangu ni kutaka kuona pesa kidogo tulizo nazo zinatumika kwa manufaa ya umma na watu walio wengi na siyo kuendeleza maslahi binafsi ya watu wachache.
Eneo jingine ambalo ningependa mlizungumze katika mkutano huu ni matumizi ya udanganyifu katika miradi ya taifa, na hasa ile inayofadhiliwa na nchi za nje. Yapo malalamiko dhidi ya udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za miradi mikubwa inayofadhiliwa na wahisani ama pekee yao au kwa ubia na Serikali yetu.
Mimi naamini Serikali inaweza kudhibiti matumizi ya fedha ili wananchi ambao ndio walengwa, wanufaike. TAKURU ifuatilie madai ya kuwepo rushwa na udanganyifu katika taasisi husika na ichukue hatua zinazostahili zilizopo katika mamlaka yake kisheria. Kwa yale ambayo yako nje ya uwezo wenu toeni ushauri serikalini kwa hatua muafaka na kuziba mianya ya rushwa katika maeneo hayo.

Mkurugenzi Mkuu na Ndugu Washiriki,
Vile vile, niongelee rushwa kwenye shughuli za kisiasa, hasa kwenye uchaguzi. Nililiongelea jambo hili Bungeni Disemba mwaka jana, lakini nataka nilirudie tena. Yameanza kujitokeza mawazo na hisia kuwa kunaanza kujengeka utamaduni kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Matendo mengi ya wagombea, mashabiki na wapambe yanaelekeza hivyo. Wasiwasi wangu ni kwamba, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Jambo hili linanisumbua. Nakubali kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi, kwa kila chama na kwa kila mgombea. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali.
Kwa maoni yangu hatuna budi kupiga vita jambo hili ili tuzuie isije kuwa utaratibu wa kawaida na utamaduni. Tutakuwa tumekwisha. Ningependa sana kupata maoni yenu juu ya nini kifanyike tukomeshe jambo hili la hatari. Bado ninayo dhamira ya kutekeleza azma yangu ya kutaka jamii tulizungumze jambo hili na hatimaye tuelewane kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Nimesema mambo mengi ya kufanywa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa. (Prevention of Corruption Bureau), kwa imani yangu kwamba TAKURU inao wajibu huo na inaweza. Kwangu mimi neno la msingi katika jina la taasisi yenu ni Kuzuia, (Prevention).
Nataka mzidi kujijenga kwa upande wa kuwa kweli ni taasisi ya kuzuia rushwa. Kuelimisha umma namna ya kupambana na rushwa ni mbinu muhimu ya kuzuia. Nimetiwa moyo sana na jitihada mlizokuwa mnazifanya kwa upande wa kuelimisha umma na kuwasisitizia wananchi wakatae kutoa hongo, hata kama matokeo ya kukataa ni bugudha, kunyanyaswa na pengine hata kunyimwa haki. Nawaomba muendelee kuwajenga imani wananchi ili wanapodaiwa rushwa wakatae kutoa.
Nawaomba mtengeneze mikakati ya kuwafanya wananchi waione hatari ya rushwa kuwa kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Hatimaye, tunaweza kufika mahali ambapo rushwa itakuwa haivumiliki katika jamii ya Tanzania. Hili litafanikiwa kwa kuweka msisitizo kwenye kuelimisha, kuhamasisha na kuwachochea watu wachukie, wakatae na waianike rushwa.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Pamoja na majukumu hayo mnayo kazi ya msingi ya kutambua na kuwadhibiti wanaohusika na kutoa na kupokea rushwa; kuwakamata na kuwashitaki. Kwa maana hiyo basi, taaluma ya msingi ya TAKURU ni uchunguzi na upelelezi. Huwezi kukamata na kushitaki wanaotuhumiwa kula rushwa bila kuwa na utaalamu na miundombinu ya uchunguzi na upelelezi. Nimefurahi kuona katika taarifa yenu mnazidi kujiimarisha kwa watu na mafunzo stahiki. Bado mnahitaji kuongezewa watu na fursa zaidi za mafunzo. Niseme tu kwa leo kwamba nimeipokea taarifa yenu na maombi hayo. Acheni tukaifanyie kazi na Waziri muhusika na Utawala Bora.
Sambamba na hili, nawaomba nilisisitize suala la maadili ya watumishi wenu. Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuhusu mahakama kwamba rushwa inaweza kuwepo kila mahali lakini ikishaingia kwenye mahakama basi haki itakuwa imetoweka. Mtu unaweza kusema hivyo hivyo kwamba ikiwa ndani ya TAKURU uadilifu utapotea mapambano dhidi ya rushwa hayatawezekana. Ningependa sana kuona kwamba chambo chetu hiki kinakuwa na viongozi na watumishi wanaotukuka kwa sifa za uadilifu na kwamba hawatuhumiwi au kufikiriwa kuwa wala rushwa. Napata faraja kuona kuwa jambo hili mnalipa uzito unaostahili na kulisisitiza. Nawasihi muendeleze msimamo huo huo. Msilegeze uzi hata mara moja kwa heshima ya TAKURU na maslahi mapana ya Taifa letu.
Kwa hiyo nimefurahi kusikia kwenye maelezo ya Mkurugenzi Mkuu kwamba katika mkutano huu mtapata wasaa wa kupitia kwa kina Code of Conduct ya TAKURU ambayo
mmeshaiandaa. Nawatakia kila la heri katika majadiliano yenu.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Nimeyasikia maelezo yahusuyo ubutu wa Sheria ya Kuzuia Rushwa na ucheleweshaji wa marekebisho ya Sheria hiyo mambo ambayo mmesema ni vikwazo vikubwa katika kufanikisha vita dhidi ya Rushwa nchini. Nashauri Waziri wa Nchi anayehusika na Utawala Bora akae na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waangalie tatizo liko wapi na kulipatia ufumbuzi.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Nawashukuru tena kwa kunialika. Nawatikia kila la heri kwenye kazi yenu hii ngumu na muhimu kwa taifa letu. Kama nilivyosema awali, mategemeo yetu ya kushinda vita dhidi ya rushwa yapo kwenu. Tutashirikiana kwa karibu na kwa hali na mali. Naomba msiwe taasisi ambayo iko mbali na wananchi, washirikisheni wananchi. Msipofanya hivyo ni sawa na samaki kuwa nje ya maji kwa vyovyote vile uhai wake utakuwa mashakani. Nguvu yenu ni wananchi. Watumieni, waelimisheni wajengeni imani na taasisi hii wawasaidie.
Yapo maeneo mengi ya kushughulikiwa, na mengine mengi mnayajua wenyewe. Lakini kwa leo niishie hapa. Mengine tutaelekezana mara kwa mara katika utaratibu wa utendaji kati yenu na ofisi yangu. Natambua sana kuwa kazi yenu ni kubwa, na nzito na nyeti. Muione hivyo, mpangilie mipango yenu kwa kutambua ukweli huo. Katika kufanya hayo, naomba wakati wote mkae mkijua kuwa niko pamoja nanyi daima. Naomba nimalize kwa kuwasihi kuheshimu na kuzingatia kanuni ya ukweli na kuepuka kuonea au kusingizia watu. Chunguzeni, chunguzeni kila mnaloambiwa na kusikia ili mpate ukweli. Lakini msionee wala kutisha watu.
Mkurugenzi Mkuu, Viongozi na Watumishi wa TAKURU, baada ya kusema hayo mengi nina furaha kutamka kwamba mkutano huu umefunguliwa rasmi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. narudia kusema kuwa Tanzania tumepata raisi.... Bravo Brother JK! kwa kweli mimi sina kuongeza kwani hata yale niliyomwandikia kabla sijajua atakuwa raisi mpya ameonyesha kuafanyia kazi, na ameongeza uchambuzi mkali sana, hapo mimi sina la kuongeza!!!

    raisi wetu amejijenga kwenye dhana ambayo ndio halisi kuonyesha kuwa matatizo yetu mengi ni ya kujitakia!! - hongera sana mimi naamini pia kuwa tusingepaswa kuwepo hapa tulipo kama system igekuwa imetengemaa na kuwa effricient! tunashukuru kusisitiza elimu kwa umma na pia kufanya kazi ya kutia oil utendaji wa serekali!! yafaa nini basi ishu ya kina mwiraria - kenya wakati washakomba hela?? TAKURU itangulie mbele kuzuia uharibifu....

    maeneo manne na mie nitarudia hapa ili kuweka msisitizo na kuyazamisha kichwani!

    1. Mikataba
    2. Procurement
    3. Miradi hasa ya donor funded
    4. Siasa!

    kamalizia kuwa sio vyema kutishia wenzao na kuwaonea!! Bravo JK! - Asante Michuzi! kitu umekipakua bado cha moto!!

    ReplyDelete
  2. Tanzania ina Rais wa awamu ya Kwanza na ya nne. Mfalme Mkapa sioni hata sababu ya Michuzi kutubandikia picha zake humu. Muache aondoke maana hakuthamini watu na sasa JK kama ni hivi mzee sisi tuko radhi kufichua wala rushwa bila uoga. Nitaandika makala yangu Tanzania, Nashukuru kwa Hotuba hii uliyotuwekea Michuzi. Nimeisoma neno kwa neno na hapa ndipo utambue kuwa kuna kizazi kinaingia ambacho kinafuatilia mambo na kutunza kumbukumbu. Mungu ibariki Tanzania, muonyeshe JK njia na muepushe na wezi na wala rushwa wasimbadilishe.

    ReplyDelete
  3. ila Makunyanzi yasiyobebeka yanataka kumsumbua! nimechangia pale kwa Jeff....mkuu wa polisi alitoa rushwa in advance !! labda ndio maana hadi leo hakijaeleweka!! tena rushwa nono nono!! kwa kweli hapa JK ana mtihani...kuwa raisi wa kisasa anayeongoza kuangalia fadhila hata zile zisizohitajika, asiyeangalia makunyanzi au kutudhibitishia kuwa historia hujirudia...

    mtakumbuka kuna wakati niliuliza huyu IGP ni mjumbe wa NEC moja kwa moja kwa nafasi yake?

    cheers!

    ReplyDelete
  4. nilisahau kudondoo, Omari aliviolate hiyo sehemu ya mwisho na ya muhimu aliyoitaja raisi..RUSHWA KATIKA SIASA

    ReplyDelete
  5. Bila kuchafua waloyoongea wachangiaji waliopita, walau sasa tumepata rais wa Tanzania. Sio rais wa Dar es Salaam na Dodoma na Moshi. Ama niwe nimeanza kuzeeka fikra, nilimuona Mkaka mkoani Mbeya mara mbili tu: mwaka 1995 na Mwaka 2000 (Uanjua kwa shuguli gani?). Walau sasa hata Michuzi atakuwa akiandamana naye mikoani kuchukua tu-picha.

    ReplyDelete
  6. Si wakati muafakaa kumfagilia JK,
    Tunataka kazi mbona Mahita bado yupo madarakani.Ilitakiwa kupandishwa kizimbani kwa Zombe na wenzake kuandamane na kuwajibika kwa Mahita si kwa vifo tu hata utendaji mbovu wa jeshi lake,Kikwete si mwanasiasa tu wewe ni askari nimefurahishwa na hotuba ya tume ya corruption squad maana iko hiyo tume na hatujasikia ikiunguruma ndo maana naiita corruption squad na si anticurruption General Kamazima una miaka mingapi tangu umeshika kikosi hicho kilicho mshinda Mafta na sasa ni wakili wakujitegemea, mbona hatujakusikia,zaidi tunaona watanzania wenzetu wakiishi maisha ya ajabu kama vile wako ahela wakati tukiwauliza kipato hicho wamekipata wapi hawana maelezo rushwa ya Tanzania haihitaji mtu kwenda shule iko wazi lakini watendaji aidha ni wala rushwa au watueleze wanashindwaje kuikabili.
    Tamati mimi sitakufagilia JK nataka kuona matendo Uncle Ben amesifiwa mpaka siku aliyoondoka madarakani sasa ndo anaonekana si kitu,mbona hatukuliona hapo awali wakati benki zikiunzwa na taarifa zisizo na uhakika zikidai kuwa hata yeye ana hisa chungu mzima.Watanzaniamuwe macho na changamkeni sasa komboeni nchi hii.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...