* Ni gazeti maarufu la The Sunday Standard

* Ni baada ya kuwa kumzushia mambo na kumkashifu bila sababu yoyote

* Lakiri kuwa habari zake hazikuwa na ushahidi wowote



GAZETI la kila Jumapili la Sunday Standard la Kenya limemwomba radhi Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwa kuandika habari za uongo, uzushi na zenye nia ya kumvunjia heshima na hadhi kiongozi huyo.

Likiomba radhi hiyo chini ya habari ya kichwa cha habari "Apology to Tanzania PM" (Maombi ya Radhi kwa Waziri Mkuu wa Tanzania) iliyochapishwa katika ukurasa wa 27 wa toleo la gazeti la Sunday Standard la Januari 13, siku 11 zilizopita, gazeti hilo lilisema:

"Gazeti la Sunday Standard sasa limethibitisha kuwa madai yaliyochapishwa katika makala ile (iliyochapishwa na gazeti hilo Oktoba 14, mwaka jana) hayana ushahidi na hayawezi kuthibitika, na tunataka kumwomba radhi, bila kificho chochote, Waziri Mkuu kwa tahayari yoyote iliyosababishwa kwake na habari hiyo."

Kunradhi hiyo kwa Lowassa inafuatia barua ya Wakili Erick Ng'maryo wa Moshi, kwa niaba ya Mhe. Lowassa aliyeandika barua kwa Mhariri wa The Sunday Standard akitaka "makala hiyo ya kashfa ikanushwe bila ya masharti yoyote na kwa dhati na kwamba mhisika aombwe radhi".

Barua hiyo ya Novemba 5, 2007 pia ilitumwa kwa mwandishi wa makala huyo, Ernest Mpakanjira; Mchapaji wa The Sunday Standard na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayochapisha gazeti hilo, The Standard Group Ltd.

"Endapo, hata hivyo, matakwa haya hayakutimizwa, maelekezo niliyonayo kutoka kwa mteja wangu ni kufungua kesi ya madai Mahakama Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kulipwa fidia na kupewa tuzo nyingine," barua ya wakili ilieleza.

Habari hiyo ya kuomba radhi pia ilitoa historia iliyolifikisha gazeti hilo kwenye hatua ya kuomba radhi, baada ya kuwa limeandika habari za uzushi dhidi ya kiongozi huyo.

Liliandika gazeti hilo: "Oktoba 14, mwaka jana, tulichapisha habari ikiwa na kichwa cha habari "Pressure on Kikwete to act on graft" (Shinikizo kwa Kikwete kuchukua hatua dhidi ya ufisadi) iliyofuatiwa na madai kadhaa ya rushwa yaliyomhusisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa."

Liliongeza gazeti hilo: "Habari hiyo ilisema kuwa Rais Jakaya Kikwete anaweza kulazimika kufanya jambo lisilofikirika, la kumtosa rafiki yake mkubwa, Lowassa."

Kwa namna ya ajabu sana, gazeti hilo liliendelea kuandika, kama lilivyoeleza lenyewe kwenye makala yake ya kuomba radhi:

"Kwamba umma ulikuwa unamwona Waziri Mkuu kama kielelezo cha ufisadi katika Serikali, ambao Rais hawezi kuudhibiti ingawa amekuwa chini ya shinikizo katika miezi miwili iliyopita kuyatosa "mayai viza" kutoka kwenye boma lake."

Linazidi kusema gazeti hilo katika kuomba radhi: "Kwamba gazeti (Sunday Standard) lilikuwa limepata habari kuwa kutafanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri wakati wowote, ambako washirika wa karibu wa Rais, akiwamo waziri mkuu, wataondolewa madarakani."

Linazidi kueleza gazeti hilo: "Kwamba viongozi wa upinzani wanasema kuwa katika kujikinga dhidi ya athari zozote (Lowassa) alimtumia na kumshirikisha mtoto wa Rais katika moja ya kashfa kubwa zaidi za kifedha, ambako mlipaji kodi alipoteza kiasi kikubwa mno cha fedha, kupitia tenda zenye utata za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa ajili ya ununuzi wa mashine za dharura za kuzalisha umeme mwaka jana (sasa mwaka juzi)."

Linaongeza: "Mashine hizo ghali mno, zilithibitika kuwa ni mitumba, na zilishindwa kufanya kazi miezi michache tu baada ya kuwa zimezinduliwa, na hivyo kuitumbukiza nchi katika kiza na kupunguza saa za uzalishaji."

The Sunday Standard linaongeza kueleza nini gazeti hili liliandika katika makala iliyolilazimisha kuomba radhi:

"Kwamba huo ulikuwa uzoefu mpya kwa Dar Es Salaam, ambayo ilikuwa imeanza kupata joto la jiwe baada ya wafadhili kuwa wametaka kuwapo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha za umma."

"Madai haya (ya wafadhili) yalikuwa yamepelekewa na utengenezaji na usambazaji wa "List of Shame" (Orodha ya Aibu) na wapinzani iliyomhusisha Lowassa, mtoto wa kiume wa Kikwete na mkewe, mfanyabiashara na mbunge Rostam Aziz aliyefadhili uchaguzi wa Kikwete mwaka 2005."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Hivi wakenya haya matatizo walio nayo kwao hayawatoshi mpaka waanze kutafuta "beef" na PM wetu .. !!???

    ReplyDelete
  2. Some people likes to stick their nose everywhere !!!!
    they should get a life and finish their own issues first.
    wao hawayaoni ya kwao kwanza !!
    pilipili wasioila sijui yawawashia nini!!!! loh !
    harusi si yako waivalia kanzu
    mmmfyoooo!@$#$@%

    mtanzania namba moja

    ReplyDelete
  3. Hawa jamaa wa Kikenya wanabidi watatueutitiri wa mamtatizo yao kabla ya kunusanusa ya watu!watuache wenyewe hatuna haja ya genocide kama ya kwao!sisi tunajua jinsi ya kutatua matatizo yetu bila ya mapanga!kama tukihamua kuchapisha hiyo list of shame Kenya si itakuwa ndio nchi namba moja kwa ufisadi uliokithiri...watuache....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...