HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE UZINDUZI WA AWAMU YA PILI YA PROGRAMU YA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA, DAR ES SALAAM, TAREHE 28 JANUARI, 2008
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma;
Waheshimiwa Mawaziri;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Waheshimiwa Wabunge;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Viongozi wenzangu wa Siasa;
Wageni Waalikwa na
Ndugu Wananchi:
Awali ya yote napenda kukushukuru wewe, Mheshimiwa Waziri kwa kunialika na kunipa heshima hii kubwa ya kuzindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuboresha Utumishi wa Umma. Nafurahi kujumuika nanyi leo katika tukio hili muhimu linalotupeleka katika hatua ya juu zaidi katika jitihada zetu za kuboresha utumishi wa umma nchini.
Tangu miaka ya tisini (1990s) Serikali imekuwa ikifanya maboresho ya sekta ya utumishi wa umma. Maboresho hayo yamekuwa yakilenga katika kuubadili utumishi wa umma ili uwe mhimili imara wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika nchi yetu, badala ya kuwa kero na kizuizi cha jitihada za Serikali za kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Waziri;
Kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako, mipango yote ya kuboresha utumishi wa umma iliyokwishatekelezwa imezaa matunda yanayoonekana. Programu ya Kuboresha Utumishi Serikalini (Civil Service Reform Programme) imefanikisha lengo lake kuu la kuwa na Serikali ndogo, yenye ufanisi wa hali ya juu na inayolenga kutoa huduma bora kwa wananchi. Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuainisha upya majukumu yake.
Tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, hivi sasa Serikali imebakia na majukumu yake ya msingi yanayohusu utawala, ulinzi na usalama na usimamizi wa uchumi wa nchi. Maboresho hayo pia yamesaidia sana katika kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali. Ajira holela na ajira hewa Serikalini zimedhibitiwa.
Hali kadhalika, maslahi ya watumishi wa umma yamekuwa yanaboreshwa kwa kutambua ujuzi na uzoefu wa watumishi pamoja na kuzingatia uwezo wa Serikali kiuchumi. Muundo wa Serikali umeboreshwa na madaraka zaidi yamepelekwa kwenye ngazi za chini waliko wananchi wengi.
Hatua hizi zimesaidia katika kuimarisha na kuboresha utendaji wa Serikali pamoja na utoaji wa huduma muhimu kama vile maji, afya, elimu na nyinginezo.
Mheshimiwa Waziri;
Katika hotuba yako pia umeelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Programu ya Kuboresha Utendaji Kazi Katika Utumishi wa Umma (Public Service Reform Programme). Programu hiyo ilizinduliwa rasmi mwezi Juni, 2000 na kumalizika Desemba, 2007.
Mafanikio yaliyopatikana ni makubwa na ya kujivunia. Napenda kuitumia nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Waziri na watumishi wote wa Ofisi yako kwa kazi nzuri mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya.
Mafanikio yaliyokwishapatikana yametokana na juhudi zenu hivyo niruhusuni niseme hongereni sana na ahsanteni sana.
Ni jambo la kuleta faraja kuona mifumo ya kuboresha utendaji kazi katika taasisi za umma imewekwa na upangaji wa mipango na bajeti za Wizara, Idara na Wakala za Serikali nao umeboreshwa. Maslahi na mazingira ya kazi ya Watumishi wa Umma yameboreshwa na matumizi ya teknolojia ya kompyuta katika shughuli za Serikali yameongezeka. Mfumo wa wakala wa Serikali umeanzishwa kwa shughuli kadhaa za serikali na sekta binafsi imekuwa inahusishwa kwa baadhi ya shughuli. Mambo haya yameipunguzia serikali mzigo na kuongeza ufanisi.
Suala la maadili ya utumishi wa umma limepewa uzito stahili. Kanuni za maadili ya utumishi wa umma zimeandaliwa na mafunzo yamekuwa yanatolewa.
Mheshimiwa Waziri,
Wageni waalikwa;Lakini, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Licha ya jitihada zetu za kuboresha huduma tunayoitoa kwa umma bado kuna mapungufu ambayo hatuna budi kuendelea kuyatafutia ufumbuzi. Kwa mfano, bado kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu huduma zisizoridhisha kwa baadhi ya Idara za Serikali.
Pia yapo malalamiko yahusuyo ubabaishaji na vitendo vya rushwa. Mengi ya malalamiko hayo yanaelekezwa kwenye sekta za elimu, afya, usalama wa raia, utoaji haki, mambo ya ndani na ardhi.
Vile vile bado kuna tatizo la tija duni katika utumishi wa umma. Baadhi ya sababu zinazosababisha kuendelea kwa hali hii ni kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa uwajibikaji katika ngazi zote za taasisi za Serikali, uchache wa watumishi wenye sifa na uzoefu wa kutosha na uongozi usiokuwa mbunifu.
Mheshimiwa Waziri na Wageni Waalikwa;
Nimefurahi kusikia kwamba matatizo haya na mengineyo ambayo sikuyataja yamezingatiwa katika uandaaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu hii.
Nimetiwa moyo, kusikia kwamba kwa kiwango kikubwa uendeshaji wa programu hii utaamuliwa, kuendeshwa na kusimamiwa na taasisi za umma zenyewe na kwamba maboresho yatakayoidhinishwa yataingizwa kwenye mipango na bajeti za taasisi hizo kwa ajili ya utekelezaji. Matarajio yangu ni kuwa kila taasisi ya umma itachambua kwa makini maboresho yanayoihusu na kuyaainisha kwenye mipango yake na kuyatekeleza kwa ukamilifu ili kuboresha zaidi huduma kwa umma.
Nimefurahi pia kusikia kwamba tatizo la kutowajibika litashughulikiwa katika awamu hii ya maboresho. Hii ni pamoja na kuandaa utaratibu wa uwajibikaji wa taasisi zote za umma katika ngazi zote. Ombi langu kwenu ni kuwa tuharakishe uandaaji wa utaratibu huo ili ukamilike mapema. Tusichukue muda mrefu sana kwa kazi ya uandaaji. Naamini kuwa utaratibu huu tukiutekeleza vizuri utasaidia sana katika kuimarisha utendaji wa Serikali na kutoa huduma kwa wananchi kwa jumla. Ndugu Viongozi na Wageni waalikwa;
Jambo lingine ambalo napenda kulisisitiza hapa ni haki ya wananchi kupata huduma nzuri kutoka kwa watumishi wa umma na haki yao kudai huduma hiyo. Utumishi wa umma upo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Huduma itolewayo ni haki yao, siyo fadhila. Hivyo kila mwananchi anayo haki ya kudai kupatiwa huduma iliyo bora.
Na watumishi wa umma wanao wajibu wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ni kwa msingi huo nimefarijika kusikia kwamba mpango huu unalenga katika kuwawezesha wananchi na wateja kwa ujumla kuwa na uelewa wa upatikanaji wa huduma za umma na kufahamu haki zao za kupata huduma bora. Hili ni jambo jema, naomba tuliimarishe. Nafurahi pia kusikia kwamba katika awamu hii ya Programu kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na kujenga utumishi wa umma wenye nidhamu na unaozingatia maadili.
Hili nalo ni jambo muhimu sana. Hakuna mafanikio bila nidhamu kazini. Na mtumishi wa umma asiyezingatia nidhamu na maadili ya kazi yake hawezi kuwa na ufanisi. Naomba suala la nidhamu na maadili tulipe uzito mkubwa zaidi ili kujenga uadilifu wa hali ya juu katika utumishi wa umma hapa nchini.
Mheshimiwa Waziri, Wageni Waalikwa;
Kuhusu kuboresha maslahi ya watumishi wa umma napenda kusisitiza mambo mawili. Kwanza, kwamba tumemekuwa tunayaboresha kwa nyakati mbalimbali lakini lazima tuendelee kuboresha. Pili, kwamba msingi wake ni tija yaani tija ya mtumishi mmoja mmoja na tija ya wengi katika taasissi na nchi nzima kwa jumla.
Sote tunatambua kuwa maslahi bora yanategemea sana kukua kwa uchumi wa nchi yetu. Pia yanategemea ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Uchumi unaokua kwa kasi na umakini katika ukusanyaji wa kodi ndivyo pekee vitakavyoiwezesha Serikali kuwalipa watumishi wake vizuri. Lazima tufanye hayo.
Hivyo, nawasihi ndugu zangu wote tuliomo kwenye utumishi wa umma tujitume zaidi, tufanye kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Kila moja wetu atimize wajibu wake ipasavyo, tena kwa wakati. Tusikwepe wajibu wetu na kwamba tuache tabia ya kutoa visingizio visivyokwisha kwa kutokutimiza malengo tuliyojiwekea.
Naamini sote tukiyafanya hayo nchi yetu itapiga hatua kubwa na ya haraka. Hii itatuwezesha kuboresha zaidi maslahi ya watumishi wa umma nchini mwetu.
Mheshimiwa Waziri, Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa;
Nafurahi kuona kwamba Mpango huu mpya umelipa umuhimu stahili suala la kuimarisha uongozi katika utumishi wa umma. Nchi yetu inahitaji viongozi makini, wabunifu, wanaoona mbali na wachapa kazi hodari.
Viongozi walio makini katika kusimamia utekelezaji wa mipango na maamuzi mbalimbali ya Serikali yahusuyo maeneo yao ya uongozi. Kwa sababu hiyo nimependezwa na uamuzi wa kuanzisha mfumo wa kutambua na kuandaa viongozi kupitia utaratibu wa mafunzo ya mara kwa mara. Bila ya shaka utaratibu huu utasaidia sana katika kujenga kada ya viongozi na watendaji bora wanaohitajika sana katika utumishi wa umma. Nawaomba muangalie uwezekano wa kuanzisha Chuo cha Taifa cha Uongozi kitakachotoa mafunzo kwa viongozi na watendaji kama njia mojawapo ya kuimarisha uongozi na utendaji Serikalini.
Mheshimiwa Waziri;
Ili Mpango wa kuboresha utumishi wa umma uweze kufanikiwa kuna mambo kadhaa ambayo hayana budi yafanyike. Kwanza, Ofisi yako lazima iendelee na kazi ya kuwaelimisha watumishi wa umma kuhusu umuhimu wa kubadilika kifikra na kimtazamo.
Hii inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya maboresho ya utumishi wa umma yanalenga katika kubadilisha taratibu, tabia na utamaduni wa kazi uliozoeleka kwa muda mrefu. Hivyo kubadilika kifikra na kimtizamo ni jambo la lazima. Lazima sisi tulio katika utumishi wa umma tubadilike.
Tuache umangimeza na kujiona kuwa sisi ni mabwana mkubwa na wananchi si lolote. Tutambue kuwa tupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na siyo vingenevyo. Hivyo kazi ya kuwaelimisha watumishi ili kutambua wajibu wao huo iwe ni ya kudumu.
Nawaomba msichoke kuifanya. Pili, hakikisheni kuwa raslimali watu kwa maana ya watumishi wa umma, inaendelezwa. Shirikianeni na taasisi nyingine za umma katika kubuni na kutekeleza mipango ya mafunzo kwa kada mbalimbali za watumishi wa Serikali. Mazingira ya kazi duniani yanabadilika kila siku. Kila kukicha kuna mambo mapya. Hivyo watumishi wa umma nao wanastahili kujengewa uwezo utakaowawezesha kwenda na wakati.
Tunahitaji kuwa na watumishi wa umma wenye uwezo na ujuzi wa kutosha. Watumishi ambao wanajua wanalolifanya na siyo kubahatisha. Tujipange vizuri kuwawezesha watumishi wa Serikali kupata mafunzo stahiki yatakayowawezesha kufanya kazi zao kwa kujiamini na ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Waziri, Wageni waalikwa;
Tatu, hapana budi kuongeza kasi ya kuanzisha na kutumia teknolojia za kisasa za habari na mawasiliano katika shughuli za Serikali. Katika dunia ya leo mambo mengi yanaendeshwa kwa kutumia mtandao wa kompyuta. Serikali nyingi duniani zinaendesha mambo yake mengi kupitia mtandao wa aina hiyo (serikali mtandao).
Nasi hatuna budi kufanya hivyo kwani itasaidia sana katika kuboresha na kurahisisha mawasiliano ndani ya Serikali na baina ya Serikali na wananchi. Pia itapunguza urasimu ambao bado ni moja ya vikwazo vya ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Vilevile, itasaidia katika vita dhidi ya rushwa kwa sababu vitu vingi vitakuwa wazi na havihitaji mazungumzo ya ana kwa ana baina ya mtoa huduma na mpokea huduma.
Mheshimiwa Waziri na Wageni Waalikwa;
Programu hii tunayoizindua leo itakuwa ya manufaa kwa wananchi ikiwa tu mabadiliko tunayoyakusudia yataongeza ubora katika utoaji wa huduma kwa umma. Hivyo lengo letu kubwa liwe ni kuimarisha ubora wa hudumu tunazozitoa kwa Watanzania. Kama nilivyosisitiza katika hotuba yangu ya kuhitimisha sherehe za siku ya utumishi wa umma za mwaka jana, watumishi wa umma lazima tudhamirie kuhakikisha kuwa huduma za leo ni bora kuliko za jana na zile za kesho ziwe bora zaidi kuliko za leo.
Naamini tukifanya hivyo tutaweza kabisa kufikia lengo letu la kujenga utumishi wa umma mahiri, utumishi wa umma ulio adilifu na sikivu na utumishi wa umma unaoweka mbele maslahi ya umma. Nawasihi wote tuitumie programu hii ya maboresho kama nyenzo ya kutufikisha kwenye lengo letu hilo.
Hitimisho
Mheshimiwa Waziri; Viongozi na Ndugu Wananchi Wenzangu;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kuwashukuru wale wote waliojitolea kuchangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa Programu hii.
Wenzetu hao ni pamoja na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali za Uingereza, Canada, Denmark, Ireland na Japan. Aidha nawashukuru wengineo wote waliofanikisha Programu hii kwa namna moja au nyingine. Kwao wote nasema asanteni sana. Tunathamini sana mchango wao. Tunawaomba wandelee kutuunga mkono.
Baada ya kusema hayo, sasa ninayo heshima ya kutamka kwamba Awamu ya Pili ya Programu ya Kuboresha Utumishi wa Umma imezinduliwa rasmi.
Vile vile natamka kwamba Jengo la Mtandao na Tovuti Mpya ya Utumishi vimezinduliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza!!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Hotuba na maneno mengi kwenye hii blogu vipigwe marufuku...TUNATAKA PICHA!!!! wewe mwenye hii blogu si mpichapiga????sasa kwanini unaendekeza maandishi?? maandishi na mahotuba kama haya yaende kwenye blogu nyingine!!

    ReplyDelete
  2. MICHUZI jamani tuwekee picha achana na mambo ya mahutuba ambayo hayatusaidii chochote,blah blah za hao maraisi tushachoka nazo.Tafadhali picha,tuondolee hivi vitu au wamekupa kitu kidogo nini?Inaudhi ukifungua blogu unakutana na mijiandishi mingi kama hii.

    ReplyDelete
  3. Your right,kazi kutumalizia ukurasa tu.

    ReplyDelete
  4. bwana michuzi wewe ni kiboko aisee, unafikisha ujumbe wa kila mtu, mungu akubariki sana sana, kaka michuzi, pia jk naona anataka kujirekebisha ni vizuri akiheshimu haki za watanzania wote, maana na yeye ni binadamu pia, siku akipatwa na mkumbo atatuhitaji na sisi, kama kuna matatizo afanye mazungumzo na kumaliza.

    ReplyDelete
  5. jk amejitahidi kwa speech hii, maana watumishiw engine wa umma,wanajisahau sana, nikitoa mfano wa sehemu moja ughaibuni sitaji jina, wana tabia za ajabu, kutumia ofisi ya serikali kujinufaisha wao wenyewe, na kusahau madai ya watanzania, wakiwa na shida, kwani hawashiirikani, natoa mfano kwa lililonipata. Jk hapa amejitahidi.

    ReplyDelete
  6. michuzi mi naona wewe speeches zako poa, hilo lispeech likubwa mno, nani aliliandika????

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...