Kamanda wa Majeshi ya UNAMID- Luteni Generali Patrick Nyamvumba (kulia) akiwa na Maj.  Wilbert Ibuge, Mwambata Jeshi wa Tanzania katika  Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa wakati Maj Ibuge alipotembelea Darfur mwaka jana  viliko vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ)
Na Mwandishi Maalum
New York

Kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) kinachoshiriki katika operesheni ya kulinda amani katika  jimbo la Darfur, nchini Sudani – yaani Tanzania Battalion (TANZBATT) kama kinavyojulikana huko Darfur na Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York - kimeonesha ushupavu mkubwa, licha ya kukabiliwa na mazingira magumu na ya hatari kioperesheni, likiwemo suala la uhaba wa zana za kisasa za kijeshi.

Hayo yameelezwa na Kamanda Mkuu anayeongoza Vikosi vya Mseto vinavyoundwa kwa pamoja na  Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa maarufu kama UNAMID, Luteni Jenerali Patrick Nyamvumba wakati alipokuwa akizungumza  mwishoni mwa wiki na wajumbe wa Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Amani (maarufu kama C-34) katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

 Wajumbe wa C-34  ni wale ambao ama nchi zao zinatoa wanajeshi, polisi, askari magereza au raia wao kama waangalizi katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UM). Tanzania ni mwanachama wa Kamati hiyo.

Mkutano huo uliwashirikisha pia makanda wakuu wengine (15) wanaoongoza vikosi vya  kulinda amani vya UM katika maeneo mbalimbali duniani.  Baadhi yao makamanda hao pia walitoa taarifa kuhusu maeneo yao ya majukumu.

Luteni Jenerali Nyamvumba, ambaye ni raia wa Rwanda, aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa TANZBATT ni kati ya vikosi katika uongozi wake ambavyo vimeonesha umahiri mkubwa na ueledi wa hali ya juu sana katika kutekeleza majukumu ya kulinda amani Darfur, likiwemo jukumu zito la kuwalinda raia wasiokuwa na hatia ambao daima hujikuta ni wahanga wa migogoro na machafuko.

“Waheshimwa wajumbe,  niseme kwamba  kwa kweli wanajeshi wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana.    Kwa mfano mwishoni mwa mwaka jana,Wanajeshi wa Tanzania, licha ya  mazingira magumu na ya hatari, uhaba wa zana za kisasa za mawasiliano katika eneo lao la majukumu huku wakikabiliwa na taarifa duni za kiintelejensia kutokana na mazingira magumu ya kioperesheni Darfur, bado waliweza kufanya kazi kubwa yenye kutukuka ya kuwalinda raia na mali zao katika eneo la Khor Abeche”. Akaeleza  Luteni Jenerali Nyamvumba.

Eneo la Khor Abeche ndipo yaliyopo Makao Makuu ya  TANZBATT. Mwisho mwa mwaka jana kulitokea mapigano makali yaliyodumu kwa muda wa takribani siku 10.

Mapigano hayo yalihusisha wanajeshi wa serikali  ya Sudan na  kikundi cha wapiganaji  kijulikanacho kama  SLA- MINI MINAWI kinachoipinga Serikali ya Sudani.

Mapigano hayo  yalikilazimisha kikosi cha Tanzania kuingilia kati kuwaokoa raia ambao licha ya  wengi wao kuuawa na wengine  kujeruhiwa lakini pia nyumba na mali zao zilichomwa moto.

Kwa ushupavu mkubwa, TANZBATT kiliingia katika maeneo ya wananchi, licha ya uhaba wa taarifa za kiintelenjesia na mawasiliano na Makao Makuu ya Sekta ya Kusini yaliyoko Nyala, hivyo kujiweka katika hatari kubwa wao wenyewe, lakini wakiwa na nia ya kuwaokoa na kuwalinda raia waliokuwa hatarini.

Kwa ushupavu mkubwa, kikosi hicho siyo tu kilisaidia kuzuia mapigano yasiendelee kati ya pande mbili husika, lakini pia kiliokoa maisha ya raia na mali zao zilizoweza kuokolewa, kuwapatia hifadhi na huduma za  malazi, chakula na madawa na kuhakikisha usalama wao ndani ya kambi yao.

Kamanda Mkuu wa  Vikosi vya UNAMID, Jenerali Nyamvumba, anasema kuwa  vikosi vya  UNAMID  ambavyo kwa asilimia 85 vinaundwa na wanajeshi kutoka nchi za afrika, vinakabiliana na uhaba mkubwa wa vitendea kazi kama vile vyombo vya mawasiliano vya kisasa pamoja na vya ukusanyaji habari za kiintelejensia.

“Vikosi vyangu vinaundwa na Waafrika, na pengine  hii inachangia sana kuwa na tatizo kubwa la vifaa, labda kama kungekuwa na wazungu ndani yake hali ingekuwa tofauti…” Anasema Luteni Jenerali Nyamvumba kwa masikitiko makubwa.

Akaongeza kuwa licha ya dhamana ya awali ya vikosi vya UNAMID ya kulinda amani kwa hali ya kawaida,  vikosi hivyo vimeongezewa dhamana nyingine nzito ya kuwalinda raia, kama waliyolazimika kukabiliana nayo TANZBATT. Na hii inatoa changamoto nyingine kubwa kwa vikosi hivyo.

Jenerali Nyamvumba alisema kuwa  dhamana hiyo ya kuwalinda raia ni mpya ambayo inawahitaji askari wake kubadilika  kimtazamo na  kiutendaji  na kujielekeza hilo jipya la jukumu la  kuwalinda raia, jukumu ambalo kwa hakika ni nje ya majukumu yao ya msingi na asilia.

“Hii ni dhana mpya ambayo haikuwamo katika makubaliano ya awali. Pia ni changamoto kubwa sana kwetu, kwa sababu sasa vikosi vyetu vinalazimika kwenda katika  makazi ya watu yanapotokea machafuko ili kuwalinda”. Anasema Jenerali Nyamvumba.

Akaongeza pia kwamba, kibaya zaidi, vikosi vyake  vinakuwa havina taarifa za kutosha za kiintelejensia, kwa kuwa hawana vifaa vya kisasa hivyo kufanya majukumu yao kuwa magumu zaidi.  Kama kwamba hiyo haitoshi, hata vifaa vya kisasa vya mawasiliano hawana.  Hili ni tatizo kubwa sana.

Akielezea changamoto nyingine zinazovikabili vikosi vya  kulinda amani  chini ya mwamvuli wa UNAMID, Kamanda huyo anazitaja kuwa ni pamoja na  mafunzo zaidi kwa askari na maafisa wanaopelekwa katika operesheni hizo.

Anafafanua zaidi kwa kusema kuwa, operesheni za kulinda amani hivi sasa zimebadilika mno na zinachangamoto kubwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Ni lazima tubadilike kifikra na kimtazamo. Mabadiliko haya lazima yaanzie katika Idara ya Operesheni za Kulinda Amani ya UM (maarufu kama DPKO), ndani ya nchi zinazotoa askari wao na kwa askari wenyewe na maafisa. Operesheni hizi zimebadilika sana, changamoto ni nyingi na kubwa. Hivyo, ombi langu ni kwamba askari na maafisa wanaopelekwa kwa ajili ya operesheni hizi wapatiwe mafunzo zaidi yakiwamo yale yanayohusu  ugaidi na  masuala ya intelejensia.

Tanzania ina kikosi kimoja katika UNAMID chenye askari na maafisa 800 na nyongeza ya Kombania ya wahandisi 75   wenye jukumu la ujenzi wa  makambi katika UNAMID.

Kikosi hicho kimegawanyika maeneo mawili: yaani Khor Abeche (yaliko Makao yake Makuu) na eneo la Muhajeria walipo wanajeshi wengine. Kombania ya wahandisi wa kijeshi wanalo jukumu la ziada kufuatia maombi ya UM ya kuhudumia eneo zima UNAMID kwa ujenzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 31, 2011

    huyo jamaa ndie mkuu wa majeshi yakulinda amani sudan kutoka rwanda.luteni jenerali atrick nyamvumba. endelea kuiwakilisha nchi yako vema rwanda na vijana wote ambao wako chini ya uongozi wako. mkooo juu vijana.

    mdau kigali makazi boxini kusaka chake

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 31, 2011

    halafu hao wapuuzi wa UN wanatoa vifaa kupelekea waasi wa Libya!

    ReplyDelete
  3. Kazi Nzuri Kaka Wilbert Ibuge. Asante kwa kuiwakilisha vema Tanzania. Big up kaka.
    Mdau Korea.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...