Upangaji makundi ya mechi za mchujo kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil ulifanywa jana (Julai 30 mwaka huu) karibu na ufukwe wa Copacabana jijini Rio de Janeiro nchini Brazil ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Jerome Valcke.
 
Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kundi C Kanda ya Afrika ambalo lina timu za Cote d’Ivoire, Morocco na Gambia. Lakini kabla ya kuingia katika kundi hilo Stars italazimika kucheza raundi ya kwanza ya mchujo dhidi ya Chad.
 
Stars ikifanikiwa kuitoa Chad baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini zitakazochezwa kati ya Novemba 11-15  mwaka huu ndiyo itaingia katika kundi hilo la C. Pia mshindi wa kundi C ndiye atakayeingia katika raundi inayofuata kabla ya kupata tiketi ya kwenda Brazil.
 
Stars ni miongoni mwa timu 29 ambazo kwenye viwango vya ubora vya FIFA vya Julai mwaka huu katika Afrika ziko chini ya timu 24 bora, hivyo kulazimika kuanzia hatua hiyo ya kuchujana zenyewe kabla ya kuingia hatua ya makundi ambayo itachezwa kuanzia Juni 1, 2012 hadi Septemba 10, 2013.
 
Kwa mujibu wa viwango vya FIFA vya Julai mwaka huu, Tanzania iko katika nafasi ya 127 wakati Chad ni namba 158. Kwa upande wa Afrika, Tanzania ni namba 33 na Chad 43. Nchi 52 kati ya 53 za Afrika zimeingia katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia. Ni Mauritania pekee ambayo haikuthibitisha ushiriki wake.
 
Timu 10 za juu kwa ubora barani Afrika ambazo zimeongoza makundi 10 ya Afrika katika upangaji ratiba ni Afrika Kusini, Tunisia, Cote d’Ivoire, Ghana, Burkina Faso, Nigeria, Misri, Algeria, Cameroon na Senegal.
 
Afrika ina nafasi tano kwenye fainali za Kombe la Dunia, huku Ulaya ikiongoza kwa kuwa nazo 13.
 
Boniface Wambura 
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 31, 2011

    Duh! tukiipiga Chad, then kugombania nafasi ya kwanza na Moroco na Ivory Coast. Nahisi safari ya Brazil 2014 imekufa kabla ya kuianza.

    ReplyDelete
  2. Wambura ebu weka habari sawa.Niliangalia "Live "Hiyo droo kwenye SSport 3.Nilivyoelewa mimi ni kwamba tukifanikiwa kuitoa Chad bado tunatakiwa kucheza na Mshindi kati ya Burundi Vs Lesotho..Tukipita hapo ndiyo kwenda kwenye Makundi..Hii ni changamoto kwa timu yetu kujitahidi angalau kuwa kwenye timu 20 bora za Africa ili kukwepa hii adha ya Mitoano.

    David V

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...