Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Arusha wakiwa katika dua ya pamoja katika ukumbi wa CCM mkoa wa Arusha ili kuwaombea marehemu na waathirika wa ajali ya meli ya MV Spice Islander iliyotokea visiwani Zanzibar wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200 na kujeruhi zaidi ya 500,katika dua hiyo pia jumla ya shilingi milioni 3.6 ilichangishwa kama rambirambi ya ajali hiyo.



Na Woinde Shizza,Arusha

UMOJA wa madhehebu yote ya kidini wilaya ya Arusha imefanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi milioni 3.6 kwaajili ya kusaidia waathirika wa tukio la ajali ya meli ya MV Spice Island iliyotokea hivi karibu visiwani Zanzibar .

Akizungumza kuhusiana na michango hiyo mmoja wa viongozi wa waumini hao Ghullamhussein.R.Mukhtar alisema fedha hizo zitawakilishwa moja kwa moja kwa makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ally Idd kwaajili ya kuwafikia waathirika wa janga hilo.

Alisema fedha hizo zilipatikana kupitia michango iliyofanyika kupitia dua maalumu iliyofanywa na viongozi wa madhehebu hayo na viongozi wa kiserikali kwaajili ya kuwaombea marehemu na waathirika wa tukio hilo .

Aidha alisema katika kuhakikisha fedha hizo zinafika kikamilifu na kutumika kwa lengo lililokusudiwa wameweka mikakati mahususi ya kufikisha fedha hizo ikiwa ni pamoja na kutuma fedha hizo katika akaunti maalumu na sio kupitia kwa mtu binafsi.

Alitaja jina la akaunti inayotumika kupokea fedha hizo kuwa ni ile yenye jina Zanzibar Disaster Fund yenye namba 051103000013 na kuwasihi wale wote wenye kutaka kutoa michango yao kutuma kwenye akaunti hiyo hapo juu.

Katika michango hiyo umoja wa makalasinga Arusha kupitia kwa mwenyekiti wao walichangia kiasi cha shilingi milioni 1,kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT kupitia kwa askofu wake Thomas Laizer liliweza kuchangia shilingi milioni 1 pia.

Wengine waliochangia ni jeshi la polisi mkoa wa Arusha kupitia kwa mkuu wake wa upelelezi RCO Leonard Paul aliyetoa shilingi 200,000,Taasisi ya Hindu mkoani Arusha nayo ilichangia shilingi 500,000,Taasisi ya Suni Arusha nayo ilichangia shilingi 600,000 huku baraza la waislamu mkoa wa Arusha Bakwata likichangia shilingi 500,000 wakati jumuiya ya Khoja Shia Ithnaasheria ya shirikisho la Afrika walishachangia kiasi cha shilingi milioni 30 kwaajili ya janga hilo.

Hata hivyo Ghullam alisifu ushirikiano ulioonyeshwa na madhehebu hayo katika kufanikisha dua na michango hiyo na kusisitiza umoja huo ulioonyeshwa uendelezwe katika shida na hata raha.

Pia aliwatakia afya njema wale waliookoka katika ajali hiyo waliopo mahospitalini na kuwatakia rehma za mwenyezi Mungu marehemu wote wa janga hilo .

Katika ajali hiyo iliyotokea usiku wa jumamosi iliyopita katika eneo la Nungwi mjini Zanzibar ilisababisha vifo vya watu 204 na kujeruhi wengine 500 baada ya meli hiyo kuzama kutokana na kuzidiwa mzigo wa abiria na mizigo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Safi sana, best news of the day! Watanzania naomba tuendelee kushikamana bila kujali dini, rangi au kabila kwa maslahi ya taifa letu na vizazi vijavyo.

    ReplyDelete
  2. Ni mfano wa kuigwa. Julius.

    ReplyDelete
  3. Kwa mwendo huu tutafika Ankal. Mungu ibariki Tanzania.

    ReplyDelete
  4. hii imekaa vizuri, mwisho wa mchezo sisi wote ni wamoja.

    ReplyDelete
  5. wengine wajifundishe kukaa chini. Ni zoezi la kiyogi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...