Ndugu zangu,

Mwandishi mTanzania Shaaban Robert ni mmoja wa wanafalsafa wa kujivunia waliopata kutokea barani Afrika

Mwandishi huyu mahiri aliweza kuyaona mengi mbele ya wakati wake. Mathalan, kupitia vitabu vyake kama vile Kusadikika na Adili na Nduguze tunaona jinsi Shaaban Robert alivyokuwa mbele ya wakati wake.

Na kwenye moja ya maandiko yake ya kifalsafa, Shaaban Robert anasema; “ Ujana ni nusu ya uwendawazimu”. Kuna ujumbe mzito kwenye mtazamo huo wa Shaaban Robert.

Na swali tunalopaswa kujiuliza ni hili; kama ujana ni nusu ya uwendawazimu, je, uzee ni nusu au ukamilisho wa jambo gani katika maisha?

Naam, katika ulimwengu huu mwenye miliki ya ujana ni kijana. Ujana hauwezi kuwa wa mzee. Lakini, mzee ndiye mwenye uzoefu na werevu wa nini maana ya kuwa kijana. Maana, mzee alishaupitia ujana. Hutokea, kuwa kijana hajui kama anao ujana maana hajatambua kuwa anaishi katika ujana.

Mzee atakaa na kujiuma vidole akijilaumu kwa kutofanya hili na lile wakati wa ujana wake. Wakti utakuwa umeshamtupa mkono. Hawezi tena kuurejea ujana.

Mwone nahodha mzee kwenye jahazi kongwe linalokaribia kuzama majini. Nahodha huyu atachukua darubini yake. Kwa kutumia darubini ataangaza majini na kuangalia chombo kingine kilichojaza abiria. Atawaita wasaidizi wake wakiwamo mainjinia wa chombo.

Atawaambia; ” Oneni jahazi lile. Ni la juzi tu, lakini lenda mbio vile na limesheheni abiria . Kwanini jahazi letu lina abiria wachache ili hali ni la siku nyingi na sie ni wenye uzoefu sana? Halafu, nasikia mwungurumo usio wa kawaida kwenye injini. Je, kuna hitilafu?”

Yumkini, wasaidizi wa nahodha watampamba nahodha kwa kile wanachodhani nahodha wao anataka kusikia.

” S’tie shaka nahodha, mwungurumo huo ni wa kawaida tu, na sie tutafika salama. Abiria hao watakuja kutambua kuwa sie ni bora kuliko wengine wote!”

La hasha, wasaidizi wa nahodha wanamwongopea nahodha wao. Kumbe, kama jahazi linakimbiwa na abiria swali la kwanza kujiuliza ni ’ kwa nini?’. Yumkini kuna hitilafu. Kinachopaswa kufanywa ni kutafuta njia ya kurekebisha hitilafu na si kuukimbia ukweli wa tatizo lililopo.

Na ilivyo majini, kila jahazi huwa na panya wake. Jahazi linapokaribia kuzama, basi, panya wake huwa wa kwanza kurukia majini.

Ni ipi basi hatma ya panya mzee jahazini?

” Nawe unajiandaa kurukia majini?” Anauliza nahodha.

”Hapana nahodha wangu. Natamani ningekuwa na miliki ya ujana. Mie ni mzee sana kuweza kurukia majini. Nimeamua kubaki jahazini. Tutazama wote!”

” Hivi , si wewe uliyesema nahodha us’tie shaka?!”

Naam, kama ujana ni nusu ya uwendawazimu, uzee ni nini?

Shaaban Robert hatunaye. Swali hilo ni letu.

Maggid,
Iringa.
Jumatano, Nov 16, 2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. UZEE NI UWENDAWAZIMU KAMILI FULL STOP

    ReplyDelete
  2. ujumbe huo uwe maalum kwa mheshimiwa Rais (JK) na wasaidizi wake.

    ReplyDelete
  3. wewe mwenyewe naona unachanganyikiwa bora ustaafu kuandika.

    ReplyDelete
  4. Nampinga kabisa huyo asemaye uzee ni uwendawazimu.Miye najiita mzee, nimekula chumvi muda mrefu sasa,katika muda wote huo nimejifunza njia na maarifa ya kudeal na matatizo na maafa tunayotupiwa na maisha. I am smarter than most young people, I must admit not all of them.Allow me to quote Horace "Eram quad es,eris quad sum" Yaani asema na, nawaambia vijana,"I was what you are, and you will become what I am"

    ReplyDelete
  5. Asante Mjengwa. Tafsiri yangu ni kuwa tukiwa vijana mara nyingi tunakuwa na mtazamo wa kukidhi matamanio ya wakati huo huo hapo hapo. Lakini kadri umri unavyosonga mbele, ndio unaanza kujua kuwa uko katika maisha ya mpito tu hapa duniani na mtazamo wako unakuwa wa kufikiri matokeo ya vitendo vyako kabla hujatenda kitendo chochote.

    ReplyDelete
  6. Uzee ni hitimisho la uendawazimu, kifuatacho ni kifo!

    ReplyDelete
  7. huyo Nahodha mwenyewe anajua anadanganya au hajui? Anafanya nini kama anajua? Kwa nini anaendelea kuhodhi jahazi kama hajui?

    ReplyDelete
  8. Some pipo bwana..! Mwandishi,!? Ua ckleva inafu. hii meseji imfikie JK popote alipo, Washauri wake popote walipo, BUNGELETU TUKUFU na wabunge wetu popote walipo.

    ReplyDelete
  9. Michuzi bwana na wewe jiuzulu naona wewe wa kizamani sana,bado ni TANU au CCM sana unavyoonekana kwani wewe kama ukiona kuna veto yoyote kuhusu CCM , basi hutoi kwa nini?

    mdau HongKong

    ReplyDelete
  10. ukifika uzee vijana wanakudharau wanajuwa huwezi kitu, hawajui na wao si muda mrefu watakuwa wazee kwa maisha yanavyokwenda mbio kwa hiyo Dunia inatudanganya!! kwani hao waliokuwa wazee walipokuwa vijana walijiona hawatokuwa wazee kwani watachukuwa muda mrefu, kumbe wapi ukiwauliza watakwambia kwa siku zilivyokwenda wanaona kama juzi tu walikuwa vijana na sasa washakuwa wazee!!!. kwa hiyo kijana ''TAFAKARI'' haya. mdau Leicester.uk

    ReplyDelete
  11. kijana ndo mtu mzee ni akiba ya mauti.

    ila uendawazimu wa vijana uko palepale, kama kutegemea zali.

    ReplyDelete
  12. ..............
    UZEE siyo UWENDAWAZIMU hata kidogo,
    ia Anonymous said Wed Nov 16, 07:16:00 AM 2011
    NI FOOL STOP

    ReplyDelete
  13. Hayo ndiyo viongozi wetu wanapenda kusikia, hawataka kuambiwa ukweli hususan kama maamuzi yao ndivyo sivyo, wanataka waambiwe kila kitu kiko sawa. Gaddafi alikuwa anapenda kusikia mazuri tuu, na waliomzunguka wakatumia udhaifu huo kumwambia kila kitu kiko sawa ili wamridhishe bosi wao matokeo yake "panya" wakachukua nchi. Vivyo hivyo viongozi wetu wa Africa ndio style wanayopenda kusikia mazuri tuu kumbe kwa wananchi walio wengi kunawaka moto na mambo sio mazuri. Well said Shaaban Robert!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...