TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nape Nnauye
Hivi karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa karibu ya asilimia 200, kutoka sh. 70,000 hadi sh. 200,000.

Malipo hayo yaliyoibua mjadala baina ya wadau mbalimbali, ni yale yanayohusisha posho ya kikao cha bunge kwa siku.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefuatilia kwa makini suala hilo la nyongeza ya posho hiyo ya wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila na Spika wa Bunge Anne Makinda.

Kwa namna suala lenyewe linavyopewa msukumo, CCM imeona si vema kukaa kulikalia kimya na hivyo imetoa msimamo wake kama ifuatavyo:-

i. Linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu wa maisha au kupanda kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache ndani ya jamii.

ii. Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza pengo/tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.

iii. Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kwamba sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma kama alivyoainisha Spika wa Bunge, ndiyo inasababishahofu na mashaka miongoni mwa Watanzania. Na kwa kweli swali kubwa kwa Watanzania hao ni je, maisha yanapanda Dodoma pekeake na kwa wabunge tu?

Hivyo  basi CCM inashauri kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi na jamii yetu kwa ujumla, waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na swala hili, kulitafakari upya jambo hili.

Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo Walimu, askari, Madaktari na wengineo.

Ni muhimu ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.

Katika hatua nyingine,  Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawapongeza sana Watanzania kwa ujumnla wao, bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kwa kushiriki kwa amani na utulivu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Ushiriki wao kwa pamoja, umeyafanya maadhimisho hayo yafane sana. CCM inaamini kuwa maadhimisho haya ya miaka 50 yatatumika kuendelea kujenga uzalendo, umoja na mshikamano wan chi yetu katika kufikia maendeleo.

Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
11/12/2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. CCM mngekuwa na cross-sectoral committee inayochambua na kutathmini agenda kabla ya kupitishwa kwa maamuzi at micro and macro levels ingewasaidia kwa kiasi fulani kutoonekana wabaya/wasaliti mbele ya jamii. Bunge linaongozwa na CCM, na wanaopinga maamuzi ya CCM ni pamoja na wana CCM. Hii inawaathiri mbele ya jamii mnayoiongoza. Ninahisi sana kuwa kamati kama hii mnayo, ila tunarudi kule kule tena.

    Hili la wabunge ni kituko kitakachoambatana na kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru, na lina athari ya muda mrefu, mbaya zaidi kama hamtaliengua sooner than later na kupiga propaganda haraka kuwaomba radhi walipa kodi.

    J. N. Mlingo (19 yrs old).

    ReplyDelete
  2. Huyu nape nini tena, ni nani anaemstua mapema yote hii.. waacheni watunyonye vya kutosha maana vita na vurugu hatuhitaji ila hapo 2015 ndio watajua wanachokifanya sasa hivi. Mbunge mwenye kupokea 70,000 kwa mahudhurio ya siku moja anaona maisha magumu na hao wanaopokea pesa hiyo hiyo kwa mwezi watasemaje... Viongozi wetu hawapendi kufikiria zaidi ya kukubali ili waonekane wajanja

    ReplyDelete
  3. Advocate JashaDecember 12, 2011

    Kila kauli ya viongozi wa CCM na serikali kulitolea kauli swala hili la posho linaendelea kutuchanganya na kudhihirisha usanii wa CCM na serikali yake.Je Makinda sio sehemu ya CCM?Iko wapi Ikulu kulitolea tamko swala hili?Niwazi kua swala hili lilikua limekubariwa katika ngazi zote CCM ,Serikali na Rais mwenyewe JK.Na swala hili lilitaka kupitishwa kimya kimya baada ya baada ya kuibuliwa na wabunge wa CHADEMA na reaction ya jamii na wanaharakati CCM na Serikali wanatafuta mlango wa kutokea soon tutasikia kauli ya JK.AIBU MUNGU IBARIKI TANZANIA.

    ReplyDelete
  4. Mtoa maoni wa kwanza lazima utofautishe ccm kama chama na uongozi wake na serikali. Serikali haifanyi kila jambo kwa idhini ya chama. ndipo chama kimeona bunge limekosea na kinawasahihisha.sio ili uonekane umelimika ni lazima uilaumu ccm tu.kijana nape anajitahidi.

    ReplyDelete
  5. si hoja kwa bunge kuongozwa na ccm na wanaopinga ni ccm. mm nasema hapa kidogo mnataka kuonyesha njia nzuri ila tu isiwe porojo zenu kama tulivyowazoea...hili hatulitaki kabisa na kuongeza posho ya mtu mmoja kwa siku iwe sawa na mshahara wa miezi miwili wa mtu mwingine...jamani, hata mungu hammwogopi?

    hatari zaidi ya hatari

    ahsante

    sm

    ReplyDelete
  6. Duh. Nape, mmechelewa, ilitakiwa CCM mtoe tamko mapema sana, sio leo ambapo tayari posho hiyo imeshatolewa na waheshimiwa sana wametia kibindoni. Kula huku bila kunawa ndo sbb inayotufanya wengi tutelekeze fani zetu na kuingia kunako siasa ambako inaonekana 'KUNALIPA' Nani awe mwalimu halafu alipwe laki 2 kwa mwezi wakati mbunge mmoja analipwa laki hizo 2 kwa kwenda kuongea 'WABUNGE WAPIMWE AKILI' bungeni?

    ReplyDelete
  7. Bunge limechemsha big time, kwa wabunge waliozipokea hizo posho zisizo za halali wazirudishe mara moja ili kuonyesha ni wazalendo la sivyo zitawatokea puani, wananchi tunataka kuwajua ni wabunge gani wamepokea hiyo posho ili tufanye maamuzi mwaka 2015 kama tuwafukuze kazi au vipi? Bunge linatia aibu kwani tangu wameanza term hii ni drama tu zinaendelea bungeni hakuna hata la maana walilolifanya kwa watanzania! Mfumuko wa bei unazidi kuwa juu, thamani ya sarafu inazidi kushuka! kwanini maisha yasiwe magunu, hiyo pesa ya posho inatoka wapi wakati budget yenyewe ya nchi asilimia 60 inategemea misaada ya nje? Na mkuu wa nchi kakaa kimya hajazungumza lolote na ameliona hili, kwani wakati zile wafanyakazi wanadai nyongeza ya mishahara na walipotaka kugoma ilibidi aite wazee na kufikisha ujumbe haraka sana na kutoa vitisho vikali, mbona swala hili amekaa kimya! Nchi hii inahitaji usawa miaka 50 ya uhuru bado makundi fulani ndo yanapewa upendeleo. Bunge inaonekana ni sehemu ya watu kujitajirisha, kwa miaka 5 badala ya kuangalia maslahi ya nchi wanaangalia maslahi binafsi. Ila sasa dunia imebadilika itafika miaka watu watazikimbia nafasi za uongozi kama wanazitafuta kwaajili ya maslahi binafsi. Great points CCM angalau sasa hivi mnaonyesha mnatetea maslahi ya wanyonge na masikini waliowengi sio makundi tu ya watu. Nape Big Up kwa statement yako, I am very sure there is true leadership in you and God will help you, It's going to be hard but you will break through no matter what, we gat yo back !

    ReplyDelete
  8. miaka yoote mngekuwa mmeshamaliza kujenga wizara huko mngeamia dodoma, ila ndo kwanza amna hata mpango, kama vipi dar iwe mji mkuu ili bunge liwepo hapo dar kuliko hii mambo ya kwenda dodoma kila mara ni gharama sanaa, ndo sababu mnang'ang'ania mashangingi plus petrol acheni tuu lazima uchumi udorore! maana inakuwa kama mnafanya mambo kwa faida yenu!

    ReplyDelete
  9. CCM sasa mumeanza kukua, big up!

    ReplyDelete
  10. Mbona CCM sasa wanaongea kama CHADEMA?. Hii si ni hoja ya CHADEMA?. Ila waende mbali zaidi kama wanavyosema chadema: Tatizo la kula pesa za uma sio kwa wabunge peke yao, hata idara za serikali na mashirika ya uma kote ziangaliwe upya na zifutwe kwani wana mishahara yao.

    ReplyDelete
  11. Acheni wivu kazi ya ubunge inahitaji pesa mingi,ukiambiwa pesa anayopata mbunge mmoja hapa Marekani sijui mungesemaje!

    ReplyDelete
  12. asante sana Zito, endelea kutoa hoja zenye mashiko ili wazifuate.

    ReplyDelete
  13. jamani ccm hamna hata huruma na wapiga kura wenu hivi mnafanya nini mnajifanya hamjui kumbe mnajua kila kitu ipo siku yenu

    ReplyDelete
  14. 1. CCM kuongelea vya wana sisiem wenzao, wafaidika wenza, wanaodai kuwa wakifika majimboni lazima wawe na pesa za kuwapa wananchi!!
    2. Sasa Mhe. Nape kila mtu akijazwa mapesa nchini hapa si tutaishia kama Zimbabwe? elfu kumi ya sasa haina thamani kabsaaaaa,

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...