Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Anna Tibaijuka ( Mb) akikambidhi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari Bw. Sergei Tarassenko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai nyongeza ya maili 61,000 nje ya eneo la maili 200 la Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari katika hafla iliyofanyika siku ya jumatano katika ofisi za Idara hiyo zilizopo katika Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani.
Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika furaha kubwa na Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari Bw. Sergei Tarassenko na maofisa wake ,mara baada ya makabidhiano ya Andiko la kudai nyongeza ya eneo la maili ya 61,000 za bahari lililowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa. katikati ni Boksi ambalo ndani yake mnamakabrasha na nyaraka nyeti zinazo husu Andiko la madai hayo, Andiko ambalo mchakato wake umechukua miaka mitano kuuandaa. Tanzania imewasilisha Andiko hilo kwa mujibu wa Sheria ya kimataifa ya masuala ya bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4 ambayo inatoa ruksa kwa nchi ambayo iko kando kando ya bahari kudai nyongeza ya eneo la bahari endapo itakidhi vigezo vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa. Tanzania inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha dai hilo.
Kutoka kulia ni Mhe. Zakhia Meghji ( Mb), Bw. Sergei Tarassenko ambaye ameshika sehemu ya nyaraka za Andiko la kudai eneo la maili 61,000 za bahari, Mhe. Waziri Anna Tibaijuka ( Mb), Mhe. Ombeni Sefue, aliyekuwa Balozi wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa ambae sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Abulrahman Hassan Shah (Mb) na Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Ardhi, Makazi na Madini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alimwakilisha Waziri wake katika hafla hiyo.

NA MWANDISHI MAALUM

NEW YORK

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imewasilisha katika Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai eneo la nyongeza lenye ukubwa wa maili 16,000 nje ya eneo la sasa la maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) ndiye aliyewasilisha Andiko hilo, kwa niaba ya serikali, katika hafla fupi na ya kihistoria iliyofanyika siku ya jumatano katika ofisi za Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari.

Andiko hilo limepokelewa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bw. Sergei Tarassenko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. ambaye aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kwamba Idara yake kupitia, Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya baharí italifanyika kazi Andiko hili.

Aidha Mkurugenzi huyo ameielezea Tanzania, kama moja kati ya nchi inayoheshima sana na yenye historia nzuri katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha Andiko hilo, Waziri Anna Tibaijuka, amesema kwa kuwasilisha Andiko hilo, Tanzania si tu kwamba imefanya kazi ya uhakika ya maandalizi na hatimaye uwasilishaji lakini ni hatua kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania.

Akabanisha kwamba mchakato wa maandalizi ya Andiko hilo ambao umechukua miaka mitano, umewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje , ikiwa ni pamoja na kuzihusisha nchi ambazo zinapakana kibahari na Tanzania.

Akizungumza manufaa ya kudai nyongeza ya eneo hilo, Waziri Tibaijuka anasema. “ Tanzania itanufaika kwa kuongeza ukubwa wa eneo la mipaka ya nchi lakini la msingi zaidi ni unufaikaji wa rasilimali zikiwamo za mafuta na gesi na madini ambazo zitakuwamo katika eneo hilo jipya, rasilimali ambazo kwa sasa zinaelekea kutoweka katika eneo la maili 200”.

Eneo ambalo Tanzania inadai liongezwe la maili 61, 000 ukubwa wake ni sawa na eneo la mikoa mitatu ikiunganishwa kwa pamoja.

Aidha kuongezwa kwa eneo hilo kutaisaidia pia serikali katika masuala ya ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki ambacho vitendo vya uharamia wa baharini vikiwa vimeongeza katika eneo la bahari ya Hindi.

“ Pamoja na kuwasilisha Andiko hilo, lakini nchi yangu inapenda pia kutoa ombi la pekee kwa idara yako, kuangalia uwezekano wa kuharakisha mchakato wa kupitia nyaraka na vielelezo tulivyowasilisha katika Andiko letu, kwani itatusaidia sana katika ulinzi wa eneo la mipaka yetu dhidi ya uharamia” akasisitiza Waziri .

Na kuongeza kwamba Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo zinaendelea zinatajitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwamo Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya bahari na sheria ya bahari katika kuukabili uharamia.

Faida nyingine ukiacha za kiuchumi ni kwa wataalamu wa fani mbalimbali kuwa na fursa ya kufanya utafiti katika eneo hilo hapo litakapokuwa limeridhiwa rasmi na kuwa sehemu ya Tanzania.

Baada ya kuwasilisha Andiko hilo, hatua inayofuatia ni kwa Tanzania kupitia wataalamu wake, itatakiwa kulitetea Andiko hilo mbele ya Makamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Mipaka ya Bahari utetezi huo utafanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Tanzania imewasilisha Andiko hilo kwa kuzingatia Sheria ya kimataifa ya Bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4, sheria hiyo inaziruhusu nchi ambazo ziko kando kando ya bahari kudai eneo la nyongeza iwapo zitakidhi vigezo vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa.

Mchakato wa kuanda Andiko hilo ulianza mwaka 2007 ukiwashirikisha wataalamu wa kada mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Ardhi na Mazingira, Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Shirika la Maendeleo ya Petroli ( TPDC).

Sehemu kubwa ya Mradi imefadhiliwa na Serikali Kuu na kwa kusaidiwa na Serikali ya Norway.

Hafla ya kuwasilisha Andiko hilo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue, na waheshimiwa wabunge, Zakhia Meghji na Abulrahman Hassan Shah ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Wengine waliohudhuri hafla hiyo ni baadhi ya wataalamu waliohusika na maandalizi ya Andiko hilo ambao ni Dr. Sellasie Mayunga, Prof. Evelyne Mbende, Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Kelvin Komba na Bi. Verdiana Mashingia.

Tanzania inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha Andiko la kudai nyongeza ya eneo la bahari na ikiwa ni nchi 10 kutoka Afrika kufanya hivyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. Tanzania nakupenda tanzani, na mwelekeo wako sasa sijauelewa kabisa, nchi yangu tanzania kumbuka tumekutoa wapi na tunaelekea wapi na leo hii sasa umeanza kutambaa jana tuu leo unataka kimbia, nchi yangu tanzania kama unakumbuka wakati uko mchanga kabisa au hata ujazaliwa nilikusimulia vitu hivi Cod Wars kati ya uingereza na iceland, pia Beaufort Sea kati ya marekani na canada na usisahau ugomvi wa bahari kati ya mrusi na nnorigian ambao tumeumaliza juzi mwaka 2010 na shangazi yako migiro akitia saini, sijui shangazi yako hakukuonya au ni kiburi chako cha kuota meno ya utoto, hebu soma mgogoro huu wa nchi za asia na tatizo lake ni hilohilo ambalo unalita la Gas na Oil we tanzania we.
    The East China Sea is one of the last unexplored highpotential resource areas located near large markets. But the
    development of oil and gas in much of the area has been prevented for decades by conflicting claims to boundaries and
    islets in the area by China, Taiwan, and Japan. Competition
    between China and Japan for gas resources in the East China
    Sea is intensifying and hampering improved relations. However, conflict is not inevitable. A compromise—joint development—is motivated by the realization that a positive ChinaJapan relationship is simply too important to be destroyed by
    these disputes.
    haya Tanzania nakupenda lakini, ila naomba iwe kwa manufaa ya walio kukomboa na kukulea na sio kwa wale waliokuteka na kukukoloni.
    MUNGU IBARIKI TANZANIA
    BABU YAKO

    ReplyDelete
  2. Wadau naomba mnisaidie. Leo nimesoma katika magazeti kwamba Ndg zetu Wazanzibari jana kwenye kikao cha baraza la wawakilishi ilizuka hoja kwamba kwa nini serikali ya muungano imefanya huo mchakato peke yake wakiwa na wasiwasi kwamba ombi hilo litakuwa na athari kwao!
    Sasa hapa naona waziri wa serikali ya mapinduzi yuko kwenye msafara na waziri Tiba.
    Hii imekaaje?
    Msaada tafadhali.

    ReplyDelete
  3. Hayo mambo ya Andiko ni daganya toto tu, kilichowapeleka huko ni siri yao moyoni.

    ReplyDelete
  4. Huu ni upuuzi tu, the existing area has not been utilized to the maximum, majangiri wanavua wanavyotaka na kuondoka, bahari haisaidii wananchi kiasi cha kutosha kukuza uchumi wao badala yake imekuwa sehemu ya kupunga upepo tu. hili eneo zaidi ni kwa faida ya nani wakati ardhi ya kutosha hata haitumiki mpaka majirani wanatutanami. Hapa mimi naona ambitions za makampuni ya uchimbaji wa mafuta tu. and thats not a real issue kwa mtanzania, kama hatujarekebisha kiasi cha kutosha sheria za uchimbaji madini hata wakipata mafuta huko yatakuwa yale yale.

    I love Tanzania and God is at work, mafisadi wote watatoka tu.

    Mungu ibariki Tanzania

    ReplyDelete
  5. Hii habari ya lini? "Andiko hilo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue"

    ReplyDelete
  6. Mbona nasikia export ya samaki zaidi ya asilimia 95 inatoka lake Victoria? Mchango wa bahari ya hindi nasikia ni kama 2%.

    Sasa tunaomba maji mengine ya nini wakati haya tuliyonayo hatuyatumii?

    ReplyDelete
  7. Hilo eneo la Maili 61000 ni za mraba au? au umbali kutoka nchi kavu? Maana ni kubwa sana kama ni umbali, inatosha kuzunguka dunia mara kadhaa... nadhani kuna tatizo kwenye hizo namba

    ReplyDelete
  8. per diem hizi , mbona wameenda wengi sana

    ReplyDelete
  9. KWELI TUMEROGWA!!SASA HILO ENEO MLILONALO SASA HIVI MNALIFANYIA NINI?LINAWAFAIDISHA NINI WATANZANIA WA KAWAIDA?AU JAMAA WA KUTAFUTA MAFUTA WAMESHAWATUMA KUFANYA HIVYO NA MKAPEWA NA KITU KIDOGO BASII MBIO HADI UN.HAYA BWANA WATAFUTIENI ENEO WAYAPATE MAFUTA WATUIBIE TU KAMA WANAVYOIBA KWENYE MADINI.ILA KUNA SIKU MTAYAKIMBIA MAGOROFA YENU HAYO MKAISHI UHAMISHONI.FANYENI MCHEZO TU

    ReplyDelete
  10. Wadau hii ni kwa ajiri ya wajukuu zenu sisi tumeshindwa wao huenda wakaweza. Binafsi nampongeza waziri sababu maslahi yatakua kwa vizazi vijavyo pengine sio sisi hivyo haina sababu ya kumkejeri waziri.

    ReplyDelete
  11. Wazanzibari linawahusu nini tukiomba kuongezewa eneo? kwani wao walikatazwa kuomba? walikuwa wamelala wapi? kila siku kelele hawana wanachokifanya zaidi ya uhodari wa kupinga kila kitu hata kile ambacho hakiwahusu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...