Nimeandika machache yafuatayo baada ya vishindo vinavyosikika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kuhusu gurupu au magurupu ya watu fulani kuingiziwa haki zao kwenye Katiba ya Tanzania.

Watanzania wenzangu, pamoja na viongozi wa siasa nchini, kwa nia njema na kwa faida yetu sote na vizazi vijavyo, nasisitiza tusije tukaingia kwenye mtego wa kuanza kubainisha na kuainisha makundi ya watu kuwa na haki kadhaa wa kadhaa ndani ya Katiba mpya ya Tanzania.

Makundi ya watu yako mengi na yana mahitaji mbalimbali, lakini hatuwezi kuyabainisha moja baada ya moja na kuyapa HAKI kwa kuandika mahitaji ya magurupu hayo au gurupu lolote linalopendekeza haki zao ziandikwe ndani ya katiba ya Tanzania, hiyo itakuwa si Katiba yetu adhimu, bali tutakuwa tunachapisha kitabu cha haki za binadamu.

Tukifanya hivyo, kila kundi na taasisi zao wataomba haki zao kubainishwa na kuainishwa kwenye Katiba, mfano wa makundi hayo ni kundi la Wanaume, Wanawake, Watoto, Wazee, Vilema wa macho, miguu, mikono, masikio n.k.

Ingawa makundi yote haya ni ya kibinadamu na wana haki zao za KIBANADAMU (bila ya kuvuka mipaka ya Utamaduni wa Kitanzania na mipaka ya Kidini yenye kumgusa kila Mwanadamu na jamii kwa ujumla), mbiyu yetu ya Tanzania inayosema ‘Binadamu wote ni sawa’, ni mbiyu ambayo tumeifuata, imetutosheleza na imeleta mifano dhahiri ya kimaendeleo ambayo ipo wazi na ya kuonekana.

Lakini, tukianza kubainisha magurupu ya watu kwenye Katiba, italeta utata wa kijamii na tukae mkao kula kubadilisha Katiba kila miaka kumi kuridhisha magurupu ya watu watakaotaka haki zao kuwemo kwenye katiba.

Tusipoangalia, yatakuja kuzuka makundi mengine kwenye uhai wetu au kizazi kijacho ambayo yataleta mparaganyiko wa kijamii ambayo yataombelewa haki zao kuwamo kwenye Katiba na kuwacha taifa letu kwenye hali mbaya ya mipasuko na ghasia mitaani, kwa madai kuwa, ikiwa tumeweza kuandika gurupu fulani kwenye katiba, kwanini tusiandikiwe gurupu letu kwenye katiba hiyo na sisi ni Watanzania?

Nataraji sote tumefaidika na haya machache na samahani kama nimekosea na huu ni mchango wangu.

Ndugu yenu,

Saleh Jaber.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. magurupu ni nini? Tumia kiswahili.

    ReplyDelete
  2. Ndugu Saleh Jaber,mimi nakupongeza sana kwa kutoa hii tahadhali mapema kabla ya mchakato kuanza.


    Waandaaji nadhani wamesikia na waache dharau katika hili.Umetoa hoja ya msingi sana tena ya kizalendo mno.Maana kuna watu hawana uoga wala aibu ya kuingiza mambo na maslahi binafsi katika maswala ya nchi na ya vizazi na vizazi.

    Kuna watu wako tayari kubadali taratibu au sheria za jamii kwa kukidhi haja ya mtoto wake au watoto wake au familia yake.Kasoro zikija kutokea halafu tulie wote.

    Tuwe macho katika katiba hii na wala hatuna sababu ya kwenda mbio mbio.Ni jambo muhimu na ni la vizazi na vizazi.Kila mmtu aridhike na kila upande uridhike kwa kiasi fulani ambapo wengi waridhike.

    Hongera sana Saleh kwa uzalendo wako,watu wasikie na waache ubinafsi na kutanguliza au kulenga maslahi katika kutengeneza katiba mpya.Na si lazima tuondoe yote yaliyoomo kwani yamo mema zaidi na mazuri katika hii ya zamani.

    ReplyDelete
  3. Afadhali ulioona. Wengine kama mimi nikiona lugha za uchanganyaji usiokuwa na lazima huwa ninapoteza kabisa hamu ya kusoma habari husika. Na ndicho kinachoniny'ong'onyeza kusikiliza kwa muda mrefu baadhiya radio!
    Sesophy

    ReplyDelete
  4. Kuna watu na vikundi wana malengo, wanafikiri wao ndio watanzania peke yao.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...