Na Prof Joseph Mbele
Kuenesha blogu sio kazi rahisi. Kuna changamoto nyingi. Kwa mfano, wakati mwingine unashindwa kujua uandike nini. Huna wazo kichwani. Wakati mwingine unaandika ukijiuliza kama kweli uchapishe hicho unachoandika. Unajua fika kuwa chochote unachochapisha, kinasambaa duniani dakika hiyo hiyo.

Kuna pia upande wa wasomaji, yaani hao tunaowaita wadau wa blogu. Binafsi, nawakaribisha wadau wanaotembelea blogu yangu. Unapoandika makala kwenye blogu yako, huwezi kujua watu wataipokea vipi. Kila mtu ni tofauti na mwingine. Kinachomridhisha au kumpendeza huyu kinaweza kumuudhi mwingine. Ufanyeje hapo?

Huwezi kumridhisha kila mtu, na kwa upande wangu siandiki kwa lengo la kumridhisha yeyote. Najaribu tu kuelezea kilichomo akilini au moyoni mwangu wakati ninapondika. 

Kuna pia wadau wanaoandika maoni. Hapo pana changamoto. Kuna watoa maoni ambao wanamshambulia au kumbeza mwendesha blogu. Je, ni sahihi kwa mwendesha blogu kuyafuta maneno yao yasionekane kwenye blogu? Binafsi, naona ni bora watu wawe na fursa kamili ya kujieleza. Tatizo tu ni jinsi wengi wao wanavyojificha chini ya kivuli cha anonymous. Mimi mwenye blogu najitambulisha wazi, na hata ninapoancika maoni kwenye blogu za wengine ninajitambulisha wazi, hata pale ninapoandika jambo linalowaudhi watu. Sielewi kwa nini wengine wasifanye hivyo hivyo. 

Lakini je, mdau akiandika matusi dhidi ya mtu mwingine, au akimdhalilisha mtu mwingine, ni sahihi kuruhusu hayo kwenye blogu yako? Suali hili lilijitokeza katika kikao changu na MwenyekitiMjengwa siku chache zilizopita. 

Nilijifunza mawili matatu kutoka kwake. Ninajua kuwa endapo blogu yangu itaendelea na kuwa maarufu kama ya Mjengwa, changamoto za aina hii zitanipata.

Nakaribisha uzoefu na maoni ya wanablogu wengine, na ya wadau.



Chanzo: HAPA KWETU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...