Mwandishi wa makala haya Maggid Mjengwa (kushoto) akiwa na Profesa Issa Shivji
Ndugu zangu, 

Yamepita majuma kadhaa sasa bila kuwasilisha fikra zangu kupitia ’ Neno la Leo’, ’ Uchambuzi wa Habari’ au ’ Tafsiri Yangu’. 


Kwa mwanadamu ni vema wakati mwingine kukaa chini; kusoma na kusikia ya wengine huku ukitafakari. 


Katikati ya taarifa ya habari ya televisheni jana usiku nilianza kujiuliza; ” Hivi nchi hii hatuna televisheni nyingine ’ Ya Kitaifa zaidi’?” Mimi nilitarajia, kuwa katika siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo kule Arumeru tungeletewa habari moto moto kutoka huko, ikiwamo uchambuzi pia. Wapi?

Niliposikia kuwa ’ Sasa tunawaletea habari za Afrika Mashariki’ nili-tune BBC News!


Kwenye taarifa ile ya habari jana usiku nilimsikia Rais Jakaya Kikwete akizungumzia juu ya tasnia ya uandishi wa habari hapa nchini. Kati ya mambo mengine, JK aliweka wazi, kuwa ameambiwa kuwa waandishi wengi hawana ajira ya kudumu. 
Kwamba wanafanya kazi kwa kupokea posho tu- These journalists can easily become mercenaries- anasema JK. Kwamba waandishi wa aina hii wanaweza kiurahisi kugeuka mamluki.

JK akaonyesha hofu yake ya kufa kwa taaluma hii. Naam, JK yuko sahihi. Na alipokuwa akiyatamka hayo kuna makofi yaliyokuwa yakipigwa, japo si ya ukumbi mzima. Kuna ambao waliguswa na ukweli huo, si tu wanahabari, bali wamiliki wa vyombo vya habari.


Na ukweli huo wa hali ya wanahabari wetu unafahamika. Lakini, kama taifa, tunafanya nini wakati “ Fourth Estate”- mhimili wa nne wa dola unaundwa na vibarua wapokea posho za siku wakati Wabunge wanakamata laki tatu na zaidi kama posho ya siku kukaa bungeni?


Huko nyuma nimepata kuanzisha mjadala wa umuhimu wa kuwepo kwa ruzuku kwa vyombo vya habari ili navyo viweze kupata nguvu ya kuendesha shughuli zao ikiwamo hata uwezo wa kuwasafirisha wanahabari wao kwenye matukio badala ya gharama hizo za usafiri kutegemea ‘ bahasha’ za wanasiasa na wamiliki wa makampuni ya biashara, ambao , masharti yasiyoandikwa ya wao kutoa bahasha zao, ni namna wanahabari hao watakavyoripoti habari za kuwapamba na zitakazowafurahisha watoa bahasha. 

Vinginevyo, kwa mwandishi asiyejua kumpamba mtoa bahasha, na badala yake akamchafua, ana hatari ya kushushwa njiani, hata kama ni katikati ya pori la mbuga ya wanyama ya Mikumi. Maana yake? Akome ubishi! 
Si tuliambiwa shuleni , kuwa ubepari ni unyama, ongeza sasa, na ufisadi pia. 

Naam, wanahabari unganeni. Huu si wakati wa kulilia huruma za watawala ikiwamo wanasiasa. Huu ni wakati wa kupambana kudai ruzuku ya Serikali kwa vyombo vya habari. Ni ruzuku, pamoja na mauzo ( kama ni magazeti) na matangazo ndivyo vitakavyowafanya muwe huru. Vinginevyo, mtaendelea kuachana na jukumu la kuutumikia umma wa Tanzania na badala yake mtabaki kuwatumikia wanasiasa, wafanyabiashara na makampuni makubwa. 

Yumkini, kwa mwanahabari kumtumikia kafiri yaweza kuwa na maana ya kuwaangamiza ndugu zake kwa mamilioni. Na kwa maana ya JK, mwanahabari wa aina hii atakuwa amegeuka mamluki- 
mercenary.

Katika kitabu chake, " The Intellectuals At The Hill" ( Wasomi wa Mlimani); Profesa Issa Shivji alipata kuandika yafuatayo juu ya uandishi wa habari; " Uandishi wa habari huenda usifikiriwe kuwa ni taaluma adimu. 
Na pengine usipewe kipaumbele katika kamati za mipango. Lakini bado, mwanahabari, kama mwasilisha wa taarifa, aweza pia akawa mwangamizaji katika jamii ya kidemokrasia. ( Au, waweza wakawa wasaidizi wa tawala za kidikteta kama wawasilishi wa taarifa potofu.) 

Lakini katika nchi zetu demokrasia ni suala la kuhubiri zaidi kuliko vitendo wakati wanahabari si kitu chochote zaidi ya kuwa maofisa uhusiano kwa "kigogo" huyu au yule. Ni nadra kwa yeyote yule ( wakiwemo wanahabari wenyewe ) wenye kuchukulia kazi ya uanahabari kwa umakini, achilia mbali kwa uwajibikaji." Prof. Issa Shivji ( The Intellectuals at the hill, Uk 176) (Tafsiri hiyo ni yangu) 


Na 
kuna wakati Rais Yoweri Museveni alipata kuulizwa; " Mheshimiwa Rais unapoamka asubuhi unafanya nini kabla ya kwenda ofisini? Museveni alijibu;" Mimi huanza siku kwa kufungulia taarifa ya habari ya BBC London!".

Hata kama ni jibu la kusikitisha, lakini, namwelewa kabisa Yoweri Kaguta Museveni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Professor Shivji alikuwa mwalimu wangu UDSM mlimani. Namheshimu sana kwa uwezo wake mkubwa wa uchambuzi na ufundishaji.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...