Mtendaji Mkuu wa asasi ya Musoma Handcrafts Haroun Sabili akitoa elimu kwa Wasanii na Wajasiriamali wa Sanaa za mikono kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari wa BASATA Godfrey Lebejo akisisitiza jambo wakati akihitimisha programu ya Jukwaa la Sanaa wiki hii. Aliwataka wasanii kuongeza thamani katika kazi wanazozalisha.
Akina mama Wasanii wa Sanaa za mikono wakiangalia moja ya kazi iliyobuniwa na kuongezewa uthamani. Kazi hiyo ilikuwa imetengenezwa na malighafi kutoka masalia ya viumbe wa baharini.
Sehemu ya Wasanii na Wadau wa Sanaa za Mikono waliohudhuria kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa wiki wakifuatilia darasa kwa makini.

Na Mwandishi Wetu

Huku kukiwa na juhudi za kutambuliwa na kuthaminiwa kazi za wasanii ndani na nje ya nchi, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kuongeza thamani kwenye kazi zao ili kuzipa ubora zaidi.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari wa BASATA Godfrey Lebejo wakati akihitimisha programu maalum iliyohusu Ubunifu, Utengenezaji na Uongezaji thamani katika Kazi za Sanaa kupitia Jukwaa la Sanaa.

Alisema kuwa, ubora katika Sanaa unapatikana pia kwa Wasanii kuangalia wenzao wanafanya nini na wao kupata ubunifu mpya kwa kuongeza vionjo, uthamani na ubunifu binafsi katika kuifanya kazi ya Sanaa kwanza kupendwa na baadaye kupewa thamani kubwa sokoni.

“Ni wazi Wasanii wetu wanapaswa kuzingatia uongezaji uthamani kwenye kazi wanazozifanya. Kubuni kazi ni suala moja lakini kuongeza uthamani katika kazi yako ili ivutie wengi na kuuzika kwa thamani kubwa ni suala lingine la kuzingatia” alisistiza Lebejo.

Aliongeza kuwa, kwa sasa kuna taarifa za Wakenya kununua kazi za Wasanii wetu kwa bei ya chini na baadaye kuziongezea ubunifu, thamani na kuziuza nje kwa bei kubwa. Katika hili anasema, inatokana na wasanii wetu kutokuzingatia falsafa hiyo ya ubunifu na uongezaji thamani wa kazi zao.

“Tuna bahati ya kuwa na malighafi nyingi sana, baadhi zimeoneshwa hapa lakini suala hapa ni sisi kutumia ipasavyo malighafi hizo katika kubuni kazi zenye ubora na kuhakikisha tunazipa thamani stahiki tunapozisafirisha nje” alizidi kusisitiza.

Awali akiendesha darasa hilo maalum ambalo wiki hii lilikuwa mahsusi kwa ajili ya wasanii na wajasiriamali wa Sanaa za mikono (Handcrafts), Haroun Sabili kutoka asasi ya Musoma Handcraft alisema kuwa, Sanaa hizo zinahitaji ubunifu na umakini mkubwa kwani kinyume chake ni kutokuvutia na kupoteza uthamani.

Alitoa wito kwa Wasanii kujiunga katika vikundi na kuwa rasmi ili kuhakikisha kwanza,wanajenga mazingira ya kuwezeshwa lakini pia kupata mafunzo mbalimbali ambayo yatawafanya wazalishe kazi za Sanaa zenye ubora na thamani kubwa.

“Ni ngumu sana kuhudumia msanii mmoja-mmoja lakini mkiwa kwenye umoja ni rahisi sana kupata fursa za uwezeshaji hususan mafunzo katika kuongeza ubunifu na uthamani wa kazi zenu” alishauri Haroun.

Katika programu hiyo iliyohudhuriwa na wadau 72, elimu kuhusu ubunifu na uongezaji thamani kwenye kazi za Sanaa ilitolewa sambamba na malighafi mbalimbali na jinsi zinavyoweza kutumika kuzalisha kazi za mikono kuoneshwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...