Mama mpendwa,ilikuwa siku kama yale leo,miaka minne iliyopita,uliondoka hapa duniani wakati tunakuhitaji sana.Japo miaka minne inaweza kuonekana ni muda mrefu kusahau machungu,kwangu mwanao imeshindikana.Kila siku ya Mungu ninaposali kukuombea pumziko na raha ya milele huko ulipo,hujikuta napatwa na uchungu usioelezeka.Kwa kifupi,mama mpendwa,kila siku baada ya kifo chako-siku kama ya leo miaka minne iliyopita,imeendelea kuwa ni hudhuni na majonzi yasiyoelezeka.

Mama mpendwa,ulikuwa ni zaidi ya mama kwangu,kwa mumeo-Baba Mzee Chahali,na kwa wanao wote na ndugu na jamaa.Nakumbuka mwaka 2005 nilipokuja likizo nyumbani,ulirukaruka kwa furaha,ukanikumbatia na kunipakata mwanao,ukaniandalia maji ya kuoga,ukanifanya nijsikie kama mtoto mchanga.Sikujua kuwa furaha ile ya mzazi kumwona mwanae waliopoteana kitambo kidogo sintoipata tena maishani.Inaniuma sana.

Nakumbuka wakati huo ambapo wewe na Baba mlikuwa mnasherehekea miaka 50 ya ndoa yenu,ulinipa mafundisho mengi kuhusu maisha,ndoa,upendo na zaidi ni kumweka mbele Mungu katika kila ninalofanya.Kabla ya kifo chako,nilikuwa nauangalia mkanda niliowarekodi wewe na Baba,na kila nilipofanya hivyo niligundua kuwa nina bahati ya pekee kuwa na wazazi wanaonipenda kiasi hicho.Sikujua kuwa mahojiano yale ndio ulikuwa wosia wako kwangu mwanao.Kwa sasa sina nguvu ya kuangalia video hiyo,kwani kila nikijaribu naishia kububujikwa na machozi.

Nakumbua nilipokwenda chumba cha maiti na kukuona umelazwa kwenye zile friji wanzohifadhia maiti.Nilikugusa mama,nilitaraji muujiza kwamba ungeamka na ndoto ile mbaya ingeisha.Hukuamka hadi leo hii.

Mama,inaniuma sana kwani nilipokuja kukuuza Februari 2008 ulikuwa umeshapoteza fahamu.Ulipokuwa Muhimbili na baadaye St Francis,Ifakara,nilikuwa najaribu kukusemesha.Kama vile ulifahamu mwanao nimekuja kukuuguza,kuna nyakati ulikuwa unatoa tabasamu lako lenye mwanya ulionirithisha.Nikategemea utaamka na kunieleza japo neno moja.Kwa bahati mbaya hadi unafariki hukuweza kuniambia chochote.Inaniuma sana mama.

Inauma zaidi ninapopiga simu nyumbani.Nilizowea kuwa nikmaliza kuongea na Baba anakupa simu wewe tupige stori.Sasa,kila ninapompigia mzee huwa najikuta nataka kumwambia Mzee akupe simu niongee nawe,kisha nakumbuka kuwa hauko nasi.Kila simu ninayopiga nyumbani inanirejeshea kumbukumbu hizo na kuniacha mpweke,mkiwa na mwenye uchungu mkubwa.

Nyakati nyingine baadhi ya watu wangu wa karibu (ninao wengi kutokana na malezi bora uliyonipatia) huwa wananiona kama dhaifu ninapowaeleza uchungu nnilio nao takriban kila siku tangu ufariki.Siwalaum,kwani wanachojitahidi kufanya ni kunishawishi nikubali ukweli kuwa haupo nasi na haiwezekani kukurejesha.Kuna wakati wananichukiza kwani najihisi kama hawaelewi jinsi kifo chako kinavyoniathiri.Lakini baadaye akili hunirejea na kutambua wanachofanya ni kujaribu kunisaidia tu.

Mama mpendwa,sijui nisemeje.Rafiki zako wakubwa,wanao vitinda-mimba,Kulwa na Doto,ndio wananitia uchungu zaidi,kama ilivyo kwa Baba.Watatu hao pamoja na wewe mlikuwa kama marafiki.Nakumbuka siku zile nawapigia simu na kuwasikia mnacheka,mnataniana na kunipa kila aina ya faraja.Kwa sasa imebaki kumbukumbu tu.

Mama mpendwa,siku ya mazishi yako Padre alituambia maneno haya: "Mama Adelina alikuwa mtu wa watu,na kila anayemjua anafahamu hilo.Japo mnaomboleza kifo chake,lakini mnapaswa kupata faraja kuwa kutokana na matendo yake mema,Baba Yake wa Mbinguni Ameamua kumchukua.Sote tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi,na ndio maana amemchukua." Maneno hayo ndio nguvu pekee inayonisaidia kumudu kufanya mambo mengine maishani.

Basi naomba nikuage tena mama kwa kumwomba BWANA AKUPATIE PUMZIKO LA MILELE NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE,UPUMZIKE KWA AMANI AMEEN.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 29, 2012

    Pole sana brother kwa kufiwa na kifo cha mzazi tena akiwa mama ni pigo kubwa sana,maumivu unayoyazungumza ni sawa kabisa na yangu,miaka mitatu iliyopita tulipoteza mama,pengo lake ni kubwa.Kwa maana hiyo kaka tujipe moyo wapendwa mama zetu wapumzike kwa amani,Till we meet again.Amen

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...