Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kuwepo ugonjwa wa Ebola ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Kanda ya Magharibi ya nchi hiyo ambapo takriban watu 20 wamepata maambukizo na kati yao, 14 wamepoteza maisha. Hadi kufikia tarehe 29 Julai 2012 kuna wagonjwa wawili waliolazwa na hali zao zinazidi kuimarika.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma na Rukwa).

Chanzo na dalili za ugonjwa wa Ebola

Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola. Dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa, na vidonda kooni. Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa damu ndani na nje mwilini.

Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 21 baada ya kupata maambukizi.

Kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola

Ugonjwa wa Ebola unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa njia zifuatazo:

Kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo

Kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu.

Kugusa wanyama walioambukizwa (mizoga na wanyama wazima) kama vile sokwe na swala wa msitu.

Tiba na chanjo ya Ebola

Mpaka sasa ugonjwa wa Ebola hauna tiba wala chanjo.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu nchini:

Kutoa taarifa ya tahadhari kuhusu ugonjwa huu kupitia kwa waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha, taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa sekta ya afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.

Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa wataalam wa Afya katika Mikoa, Wilaya na Maeneo ya mipaka. Aidha, watalaam wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu, ili endapo ugonjwa huo ukitokea uweze kutolewa taarifa mapema.

Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya.

Wito

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa hapa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu, mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.

Regina L. Kikuli
KAIMU KATIBU MKUU
31/7/2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Tuombe Mungu sana!

    Mungu apitishie mbali!!!

    Hili Dubwana ni balaa zaidi wakati Kipindupindu tu kinatutoa kamasi!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...