SERIKALI imetaja manufaa na faida ambazo wanatarajia kuzipata wananchi wa Mtwara pamoja na Lindi endapo gesi itasafirishwa kwenda Jijini Dar es Salaam.

Imesema Mkoa wa Mtwara ndipo utakapo jengwa mtambo mkubwa wa kusafishia gesi hiyo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa matumizi ya uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja viwandani.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Radio One jijini Dar es Salaam.

Naibu waziri huyo ameweka wazi kuwa mkoani Mtwara licha ya Serikali kupanga kujenga viwanda vingine kadhaa, inajenga mtambo wa megawati 250 ambao utakuwa ukizalisha umeme na mwingine kujengwa mkoani Lindi eneo la Somanga Funga utakao kuwa ukizalisha megawati 520.

Akifafanua zaidi Simbachawene alisema eneo la Mikindani katika Kijiji cha Msijute mkoani Mtwara kinatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha saruji Afrika Mashariki na Kati chenye uwezo wa kutoaji ajira kwa watu 6000 jambo ambalo ni manufaa ya Wanamtwara.

Alisema pia tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya mbolea wamejitokeza kujenga viwanda mkoani Mtwara na Serikali itaviacha vinu vya kuchimba na kusindika gesi eneo hilo jambo ambalo bado ni manufaa makubwa kwa wananchi.

“Viwanda vya kusindika gesi hii vimepangwa kujengwa maeneo ya Lubasi, Kishere, Mchinga Bay, Lindi, Sudi Bay, Airport pamoja na Mikindani…viwanda vyote hivi vitatoa ajira kubwa sana,” alisema Naibu Waziri.

Alisema licha ya manufaa hayo, gesi itakapopelekwa Dar es Salaam itazalisha umeme wa uhakika pamoja na kutumika moja kwa moja viwandani jambo ambalo litailetea taifa tija kubwa ikiwa ni pamoja kupunguza ukali wa maisha.

“Ni kweli gesi imepatikana Mtwara lakini ni lazima uipeleke sokoni ili iweze kupata soko (wateja)…Dar es Salaam ndio kwenye soko, huwezi ukaiacha Mtwara ambako hakuna soko; mbali na kuzalisha umeme kuna viwanda 37 na hoteli kadhaa zinataka ziitumie moja kwa moja ni lazima iletwe huku, Mtwara pale hakuna soko,” alisema.

Aidha alitolea mfano kuwa zipo nchi mbalimbali ambazo zimegundua gesi lakini zimelazimika kuisafirisha kwa mabomba kwenda eneo la soko. Alibainisha kuwa nchi ya Urusi inasafirisha gesi yake hadi nchini Ujerumani huku Iran ikisafirisha hadi India gesi yake kutafuta soko lilipo.

Alisema miundombinu mikubwa ya umeme ipo jijini Dar es Salaam hivyo kuna kila sababu ya gesi hiyo kuletwa jijini humo ili iweze kuzalisha umeme na matumizi ya viwandani moja kwa moja pamoja na matumizi mengine, ambapo tayari wateja wamepatikana.

Aidha aliongeza kuwa uzalishaji umeme wa kutosha kwa kutumia gesi utapunguza bei ya umeme na kuuzwa kati ya senti 6 na 8 za Marekani jambo ambalo litapunguza ugumu wa maisha na pia bei ya bidhaa nchini.

Pamoja na hayo amevitaka baadhi ya vyama vya siasa na taasisi zisizo za Serikali (NGO’s) zinazowapotosha Wanamtwara juu ya mradi huo kuacha kitendo hicho kwani hakuna asiyejua umuhimu wa gesi hiyo kuja Dar es Salaam.

“Hivi ni nani asiyejua kuwa tatizo la kutokua na umeme wa uhakika nchini ndilo linalokwamisha uchumi wa nchi…Tanzania inapoteza bilioni 4.5 kwa ajili ya kununua mafuta ya kuzalisha umeme kwenye mitambo yake, sasa gesi itaokoa fedha hizi,” alisema Simbachawene.

Hata hivyo amesema Serikali haiwezi utekeleza mradi huo kwa nguvu bali itaendelea kuwaelimisha Wanamtwara umuhimu na manufaa ya gesi hiyo kuletwa Dar es Salaam na inaimani wataelewa na malumbano kumalizika.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Somo limeeleweka:

    Isipokuwa:

    1.Mtatuhakikishia vipi kuhusu matekelezo hayo ya ahadi?

    2.Tulipata tetesi (kutoka gazetu la la Kenya la The East African la wiki hii) ya kuwa Gesi ikifika Dar itaunganishwa kwenda Mombasa-Kenya, hadi Uganda na Rwanda, je vipi hapo?

    Ni kuwa hawa majirani zetu wanaweza kunufaika sana na gesi hiyo ghafi zaidi yetu, hivyo kama watazalisha bidhaa zinazotokana na gesi MKATABA LAZIMA UWEPO TOFAUTI uwepo Mkataba wa PSA-Production Sharing Agreement na badala ya kuishia kwenye mauzo pekee!

    ReplyDelete
  2. Tatizo sio manafaa haya ambayo yatasababishwa na gesi, watueleze
    1. Ni kwa nini Mtwara na lindi ni masikini kuliko mikoa mingine?

    2. Ni kwa nini Changombe ilifanywa chuo kukuu na sio Mtwara TTC wakati tayari DAR kuna vyuo vikuu vya serikali zaidi ya 10? Mfano UDSM, Ardhi, Muhumbili, OUT, IFM, CBE, TIA, Tanzania Institute of Social work, Chuo cha KUMBUKUMBU YA mWAL Nyerere, DIT, National Institue of Transport, DUCE Etc.

    3. Kwa nini haijengwi barabara na reli toka mtwara hadi Songea ili bandari ya mtwara itumike kwa bidhaa za Malawi, Zambia, Kongo nk. kwa sababu ni karibu kufika nchi hizo kuliko kutoka Dar

    4. Ni kwa nini wanataka kujenga bandari mpya Bagamoyo wakati ipo pua na mdomo na Dar na sio Lindi

    5. Ni kwa nini wanapanua bandari ya Dar na sio Mtwara?

    6. Inawezekanaje Dar yenye watu mil 4 itoe asilimia 80 ya mapato kwa nchi yenye watu mil 45

    Nani alipelekea Dar iwe ndio soko la gesi na sio Mbeya ama Songea?

    ReplyDelete
  3. Kwanini siku zote hamkutoa ufafanuzi? Dharau sio? Na kwanini hamuendi kuongea na wenye gesi mnaongelea Dar es salaam? Ahadi zilikuwepo na zitaendelea kuwepo, wapeni gesi yao waifaidi. Hizo ahadi zenu za kujenga viwanda pelekeni kwingine.

    ReplyDelete
  4. Watawala wa siku hizi kila ni wabinafsi sana.ukienda ardhi utashangaa pwani imefanywa ndo hub ya viwanda.katavi ndo imekuwa speed ya kila kitu.Kila anaeingia madarakani anaangalia usawa wake.Tanzania ni kubwa na ni yetu sote mipango ya umangimeza itawatokea puani.ni vema maendeleo yakasambazwa nchi nzima.kwani nani alisema mtwara haiwezi kuwa soko.wananchi wana ukweli na bado.

    ReplyDelete
  5. Natamani watu wangewaza badala ya kujenga viwanda ambavyo atafaidi mtu mmojammoja ama kwa kufanya biashara na viwanda au kuajiriwa na kiwanda (ambacho kwa utaalam unaohitajika nina shaka kama wananchi wa mtwara wana sifa) badala yake uanzishwe mfuko (fund) kutokana na mapato ya gesi na kazi yake iwe ni kugharimia huduma za jamii kwa maeneo ya mtwara. maeneo ya kipaombele kiwe ni barabara, shule, zahanati, scholarships na hata dawa au pembejeo.
    Njia inayotumika sasa haifai kwani wajanja wachache tu ndio waakaofaidi!!!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...