Wizara ya
Maliasili na Utalii imewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhioevu
ambayo ni makazi na mapito ya ndege wahamao kushirikiana na Serikali katika
kuwalinda ndege hao na kuhifadhi mapito na makazi yao. Wananchi pia
wanakumbushwa kuwa maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo yanafaa kwa
matumizi ya kila siku ya binadamu, wanyama na ndege, hivyo maeneo hayo yalindwe.
Taarifa hii
imetolewa na Wizara wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani
ambayo huadhimishwa kimataifa tarehe 11 na 12 Mei kila mwaka.
Aina za ndege
hao ni kama vile Heroe mkubwa na mdogo (flamingos) ambao wanahama kila mwaka
kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kutafuta malisho, maji, kukwepa
hali mbaya ya hewa na kupata sehemu salama ya kuzaliana.
Tanzania ni nchi
mojawapo yenye sehemu nyingi ambazo ni salama kwa mazalia ya ndege. Kwa mfano,
Ziwa Natron ni maarufu kwa mazalia ya ndeye aitwaye Heroe mdogo. Inakadiriwa
kuwa asilimia 80 ya Heroe mdogo kote duniani huzalia katika Ziwa Natron liliko
Kaskazi mwa Tanzania. Ziwa hilo ni
kivutio cha utalii kutokana na ndege hao.
Maadhimisho ya
Siku ya Ndege Wahamao Duniani yalianza mwaka 2006 na kuendelea kusherehekewa kila
mwaka mwishoni mwa wiki ya pili ya kila mwezi Mei. Watu duniani kote huitumia fursa hii kutoa
elimu na kufanya matembezi katika sehemu zenye Ndege hawa kwa ajili ya kusherehekea siku hii.
Ujumbe wa mwaka
huu wa Siku ya Ndege Wahamao ni: "Tuunganishe juhudi zetu katika
kuwahifadhi ndege wahamao mapito na makazi yao (Networking for
migratory birds), ". Tafsiri ya ujumbe huu ni kuwa nchi, mashirika
na watu binafsi wanatakiwa kuunganisha maeneo ya ardhioevu kwa ajili ya
uhifadhi endelevu wa ndege wahamao.
Utunzaji kwa
ndenge wahamao ni sababu mojawapo iliyofanya Tanzania kusaini Mkataba wa
Uhifadhi wa Ardhioevu (Ramsar) mwaka 2000. Ardhioevu, pamoja na maufaa mengine,
ni makazi ya ndege wahamao.
Kutokana na
Mkataba huo Tanzania imetenga maeneo ya Ramsar ambayo ni muhimu katika
kuhifadhi bioanuwai. Maeneo ya ardhioevu yaliyotengwa ni pamoja na Ardhioevu
zenye umuhimu wa kimataifa kama vile:- Malagarasi-Muyovozi ambayo ni muhimu kwa
uhifadhi wa ndege aina ya Korongo domokiatu (Shoebill stork), na eneo la Ramsar
la Ziwa Natron ambalo ni muhimu katika kuhifadhi ndege aina ya Heroe mdogo (lesser flamingo) .
Serikali imekuwa
ikiwajengea wananchi uwezo wa kuhifadhi na kutumia rasilimali za ardhioevu
nchini kwa kutoa elimu ya uhifadhi katika maeneo yanayozunguka maeneo ya Ramsa.
Maeneo hayo ambayo ni makazi muhimu ya ndege wahamao yanasimamiwa na Sheria ya
Kuhifadhi Mazingira ya mwaka 2004 na ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009.
George
Matiko
MSEMAJI
WIZARA
YA MALIASILI NA UTALII
11 Mei 2013
Asante Bwana Matiko, tumesikia na tumejifunza kitu.
ReplyDeleteSikuwa najua kama kuna siku maalumu inaitwa hivyo.