THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

Rais Kikwete aomboleza msiba wa Mzee Alfred Tandau


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea kushtushwa na kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha aliyekuwa Mweka Hazina wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kiongozi wa miaka mingi wa wafanyakazi na Waziri wa muda mrefu wa Serikali, Mheshimiwa Alfred Tandau ambaye ameaga dunia jioni ya siku ya  Aprili 30, 2013.

Katika salamu zake kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Abdulrahaman Kinana, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM amesema:

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mzee Alfred Tandau ambaye nimejulishwa kuwa amepoteza maisha jioni ya leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu ya kansa ya tumbo.”

“Nilimfahamu Mzee Alfred Tandau kwa miaka mingi. Alikuwa kiongozi hodari na mwaminifu ambaye katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wake wa umma alithibitisha uadilifu na uzalendo wa kiwango cha juu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Katika uongozi wa Chama cha Wafanyakazi cha NUTA na baadaye JUWATA, Mzee Tandau alijipembenua kama mtetezi halisi na mkweli wa maslahi ya wafanyakazi. Katika Serikali ambako alitumia kwa miaka mingi kama Waziri alikuwa mwaminifu na mtii kwa Serikali yake, kwa viongozi wake na kwa wananchi aliowatumikia. Katika nafasi yake ya Mweka Hazina wa CCM aliendeleza sifa hizo hizo alizokuwa nazo tokea nyuma. Tutakosa sana busara na ushauri wake.”

Ameelezea Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Kinana salamu zangu za dhati za rambirambi kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako nawatumia rambirambi viongozi na wanachama wote wa CCM kwa kumpoteza kiongozi na mwanachama mwenzao.”

Amesisitiza: “Aidha, kupitia kwako, naomba unifikishie salamu nyingi za pole kwa familia kwa kuondokewa na kiongozi na mhimili wake. Wajulishe kuwa niko nao katika kuomboleza kifo cha kaka yetu na kiongozi mwenzetu na naelewa machungu yao katika kipindi hiki. Napenda wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya marehemu. Amina.”  

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM


Hoja moja imeshachangiwa mpaka sasa.

  1. Anonymous Anasema:

    Poleni sana familia ya mzee Tandau.