Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimtunuku shahada ya heshima ya Uzamivu PhD Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua mchango wake katika Jamii, kitaifa na kimataifa pamoja na kufanikisha kuanzishwa kwa Taasisi hiyo kwenye Mahafali ya pili  iliyofanyika leo  jijini Arusha.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimtunuku shahada ya PhD ya Sayansi Uhandisi na Hesabu Bw. Jonas Petro Senzige kwenye Mahafali ya pili ya Taasisi hiyo iliyofanyika leo jijini Arusha.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia kwenye Mahafali ya 2 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyofanyika leo jijini Arusha.
 Sehemu ya wahitimu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela 
Wahahitimu w PhD  katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanmzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika maandamano na viongozi wa Taasisi hiyo pamoja na wahitimu, wakati wa Mahafali ya 2 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika leo  jijini Arusha.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal na wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Shahada ya Uzamili na Uzamifu kwenye Mahafali ya 2 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyofanyika leo jijini Arusha. 
Picha na OMR


HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AKIPOKEA SHAHADA YA HESHIMA YA UZAMIVU (HONORIS CAUSA) YA CHUO KIKUU CHA NELSON MANDELA CHA SAYANSI NA TEKNOLOJIA, TAREHE 18 DESEMBA, 2014, ARUSHA

Shukrani kwa Kutunukiwa Shahada
Mheshimiwa Dkt. Gharib Mohamed Bilal, Makamu wa Rais na Mkuu wa Chuo;
Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Sayansi na Teknolojia; Mheshimiwa Profesa David Homeli Mwakyusa, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo;
Profesa Burton Mwamila; Makamu Mkuu wa Chuo;
Mheshimiwa Gatechew Engida, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO;
Mheshimiwa Daudi Felix Tibenda; Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Wanajumuia wote wa Chuo;
Wahitimu;
Mabibi na Mabwana.
Nasimama mbele yenu kwa unyenyekevu mkubwa kupokea Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Honoris Causa) mliyonitunuku leo hii. Nashukuru kwa maneno mazuri yaliyosemwa juu yangu wakati wa kunitunuku Shahada hii. Kutunukiwa kwa shahada hii ni heshima kubwa kwangu na Watanzania wote. Heshima hii mliyonipa ni deni kubwa kwangu na kwa Serikali yetu kuendelea kutimiza azma yake ya kutekeleza mapinduzi ya sayansi na teknolojia katika sekta zote.  Kwa kufanya hivyo, tutatimiza matarajio yenu na kulinda hadhi na heshima ya Shahada hii. Nasi hatutarudi nyuma na tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kufikia lengo hilo jema.
Wakati nakubali Shahada hii natambua mchango mkubwa wa wana-sayansi, wanawake na wanaume Watanzania ambao juhudi zao zimetuwezesha kupiga hatua hii ya kuridhisha ya matumizi ya sayansi na teknolojia. Napokea heshima hii na kuitoa kwa Watanzania wote ambao mchango wao umewezesha nchi yetu kupiga hatua ya kutia moyo katika kuendeleza sayansi na teknolojia. 
Pongezi kwa Uongozi wa Chuo
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Wanajumuia wote wa Chuo;
Niruhusu nikupongeze wewe, Mkuu wa Chuo, na uongozi mzima wa Chuo chetu hiki muhimu kwa mafanikio makubwa mliyoyapata katika kipindi kifupi cha uhai wake. Haya ni mahafali ya pili tokea Chuo hiki kianzishwe, Inatia moyo kuona chini ya uongozi wenu Chuo kinapata mafanikio makubwa. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 44 wa shahada ya uzamili mwaka jana hadi 91 mwaka huu. Hali kadhalika idadi ya wanaohitimu kwa wakati nayo imeongezeka kutoka asilimia 83 hadi asilimia 93. Nawapongeza sana wanafunzi na wahadhiri wa Chuo hiki walioshinda tuzo za kimataifa zinazotolewa na Bill and Belinda Gates Foundation, Shirika la Chakula Duniani (FAO) na Royal Academic of Engineering. Ushindi wenu ni ushahidi tosha wa ubora wa Chuo chenyewe. Ndio maana pia kunakuweko na muitikio wa mashirika ya ndani na ya kimataifa yanayojitokeza kufadhili wanafunzi wanaosoma katika Chuo hiki na kufadhili programu za Chuo hiki. Nawaomba muendelee kushirikiana na wadau wengine wa ndani na nje ili kuongeza wigo wa wadau kutoka vyuo vya kimataifa mnavyoshirikiana navyo sasa. 
Chuo hiki ni sehemu ya mtandao wa vyuo vya Nelson Mandela vya Sayansi na Teknolojia katika Bara la Afrika. Chuo hiki cha Arusha ni mahsusi kwa ajili ya kanda ya Afrika Mashariki. Ndiyo maana Hati Idhini (University Charter) niliyokipa Chuo hiki inaeleza bayana kuwa Chuo hiki kinapaswa kuwa chenye hadhi maalum (special status). Hadhi hii yapaswa pia ionekane katika ubora wa elimu inayotolewa hapa.  Aghalabu jambo hilo ni matokeo ya ubora wa wahadhiri wake, programu zake na miundombinu yake. Nimesikia changamoto zinazowakabili katika kufikia lengo hilo. Makamu Mkuu wa Chuo amezungumzia mahitaji ya miundombinu na fedha kwa ajili ya uendeshaji na ufadhili wa wanafunzi. Napenda kuwahakikishieni kuwa serikali inayo dhamira ya dhati ya kutatua changamoto hizi na kwamba tutafanya kila tuwezalo tuwe wa msaada.
Wakati nilipokuwa nazindua Chuo hiki, nilizindua pia Mfuko Maalum wa Dhamana wa Chuo yaani Endowment Fund for Excellence. Niliahidi kuuchangia na leo natangaza kuwa Serikali itatoa shilingi milioni 200 za kuanzia na tutaendelea kuchangia mara kwa mara. Nimefarijika kuona nanyi mmeanza kufanya juhudi za kuanzisha mpango wa ubia na sekta binafsi wa Nelson Mandela Public Private Partnership (NM-PPP). Huu ni uamuzi sahihi kabisa kwani kuhusisha sekta binafsi katika uendelezaji wa Chuo hiki ni jambo la manufaa makubwa.
Umuhimu wa Sayansi na Teknolojia Katika Kufanikisha
Dira ya Taifa 2025
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Ni utamaduni uliozoeleka na kukubalika kwa muda mrefu kuwa Mtunukiwa wa Shahada ya Heshima ya Uzamivu hupewa fursa ya kutoa nasaha zake. Imekuwa ni kama wajibu unaombatana na haki ya kupata Shahada yenyewe kiasi kwamba kukubali kimoja yakupasa ukubali na kingine. Madhali nimekubali Shahada hii ya heshima, nawajibika na sina budi kupokea heshima hii kwa kuzungumza. Mimi sio mwanasayansi kitaaluma, lakini ni muumini na mshabiki mkubwa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni muumini wa dhati wa dhana kuwa, bila ya kuendeleza sayansi na teknolojia, hakuna mapinduzi endelevu ya kimaendeleo. Hivyo basi kuendeleza Mapinduzi ya sayansi na teknolojia si suala la hiyari, bali ni la lazima kwa jamii yoyote ile inayotaka kujiletea maendeleo endelevu, kuondokana na umasikini na kuzishinda changamoto zake.
          Jamii zote zilizopiga hatua kubwa za maendeleo zimefanya hivyo kwa kuwekeza katika sayansi na teknolojia. Tanzania siyo kisiwa cha upweke.  Tunatambua kuwa hakuna maendeleo bila kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia.  Dira ya Taifa ya Mwaka 2025 imetamka bayana kuwa Tanzania inalenga kuwa nchi ya uchumi wa kati, ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia kwenye lengo hilo adhimu kunahitajika mapinduzi katika uzalishaji, hususan kilimo na viwanda, mapinduzi katika utoaji wa huduma na mapinduzi katika uendelezaji wa rasilimali watu. Kichocheo cha mapinduzi hayo kufanyika si kingine bali ni maendeleo na  matumizi ya sayansi na teknolojia. 
Uhusiano wa Sayansi, Teknolojia na Maendeleo
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Historia imetufundisha kuwa nchi zilizoendelea zilianza na mapinduzi ya kilimo, kisha mapinduzi ya viwanda na hatimaye mapinduzi ya huduma. Kichocheo kikubwa cha mapinduzi hayo ilikuwa ni mabadiliko ya sayansi na teknolojia.  Hivyo ndivyo ilivyofanyika kwa wenzetu wengine walioendelea, nasi hatuna budi kufuata mkondo huo. Wenzetu hao waliopiga hatua kubwa sasa wameanza safari ya kujenga uchumi unaotegemea sio viwanda (industrial economy) pekee, bali ujuzi (knowledge based economy). Uchumi huu unasukumwa zaidi sasa na ujuzi na ugunduzi (knowledge and innovation) sio tena na uzalishaji (production) pekee. Wameelekeza sasa tafiti zao kutafuta majawabu si tu ya sasa bali na hata yale ya wakati ujao. Wanafikiria na kutafiti juu ya maisha katika sayari nyingine nje ya dunia tunayoishi. Huko ndiko dunia inakoelekea, sisi hatuwezi kufanya kinyume chake.  Hatuwezi kubaki nyuma. Jawabu pekee ni kuwekeza katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.  Kuwa na chuo kama hiki ni uamuzi na hatua sahihi.
Ripoti ya Ugunduzi Duniani ya 2014 (Global Innovation Index) yenye kuhusisha nchi 143 zilizopimwa kwa vigezo vinane, imezitaja nchi za Usiswi, Uingereza, Sweden, Finland, Uholanzi, Marekani, Singapore, Denmark, Luxemburg na China (Hongkong) kuwa ni nchi zinazoongoza kwa ugunduzi duniani. Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya 123 na nchi ya 24 kati ya 33 za Afrika. Ripoti inazitaja, nchi 25 zinazoongoza kwa ugunduzi duniani kuwa ni nchi za uchumi wa kipato cha juu (high income). Nchi za kipato cha kati na chini hazimo katika kundi hilo kutokana na uwekezaji mdogo katika sayansi na teknolojia. Ukweli huu unadhihirishwa zaidi na ripoti ya Global Research and Development Funding Forecast ya 2014 inayoonyesha kuwa katika mwaka 2014, Marekani imepanga kutumia Dola Billioni 465 (asilimia 2.8 ya Pato la Taifa), China Dola bilioni 284 (asilimia 2 ya pato la Taifa) na Japan Dola bilioni 165 (asilimia 3.4 ya pato la Taifa) kwa ajili ya shughuli za utafiti.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Takwimu nilizozitoa zinaonyesha, pasipo na chembe ya shaka, kuwa uko uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya rasilimali katika sayansi na maendeleo makubwa. Somo tunalolipata hapa ni kwamba hakuna mazingaombwe wala njia ya mkato ya kujipatia maendeleo ya juu.  Hatuna budi kuwekeza katika kuendeleza sayansi na teknolojia nchini kama tunataka kutoka hapa tulipo. Hatuna budi kuwekeza zaidi kwenye  kufundisha wanasayansi, na katika tafiti na ujenzi wa miundombinu ya kuwezesha wanasayansi kufanya tafiti zao.  Kwa muda mrefu sana hili ni eneo ambalo hatukulipa uzito unaostahili. Tumefundisha na kuwekeza sana katika kuwaandaa vijana wetu katika fani za sayansi za jamii, uongozi, siasa, sheria na biashara. Pamoja na kada hizo kuwa muhimu, lakini wanasayansi ni muhimu zaidi.
Hatua za Serikali
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mimi na Serikali ninayoiongoza tumechukua hatua kadhaa kurekebisha kasoro hizi za kihistoria. Wakati naingia madarakani, nimekuta hali katika eneo hili la sayansi na teknolojia ikihitaji msukumo wa pekee. Idadi ya wanafunzi wa sayansi ilikuwa ndogo na wanafunzi wengi hawakupenda kusoma masomo hayo maana hapakuwa na mazingira ya kuvutia kusoma masomo ya sayansi shuleni na ya kimaisha kwa wale waliohitimu masomo ya sayansi. Hapakuwa na ufadhili wa masomo ya sayansi hivyo ilikuwa pia vigumu kwao kujiendeleza. Walimu wa sayansi nao walikuwa wachache, maabara za sayansi katika shule zetu zilikuwa haba na katika shule nyingine zilikuwa zimechakaa.  Vituo vya utafiti vingi vilikuwa vina miundombinu iliyoharibika na ajira za watafiti zilikuwa zimesitishwa. Hapakuwa na fedha zinazotengwa mahsusi kwa ajili ya utafiti. Hali kadhalika gharama za matumizi ya simu na intaneti nazo zilikuwa juu sana.
Tumefanya maamuzi ambayo wakati mwingine yamestaajabisha wengi. Tumepanua udahili wa wanafunzi wa masomo ya Sayansi kutoka wanafunzi 32,899 mwaka 2008/2009 (10,619 wakiwa wanawake) hadi wanafunzi 51,840 kwa mwaka 2012/2013. Ongezeko hili limechangiwa na uamuzi wetu wa kutoa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi ambapo fani za Sayansi ya Tiba, Uhandisi, Sayansi za Asili (natural sciences) na Kilimo zimepewa kipaumbele. Pia limewezekana kwa kufanya uamuzi wa kupanua udahili katika vyuo vyetu vikiwemo Chuo Kikuu kipya cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Madaktari Muhimbili.  Halikadhalika tumekifanya Chuo cha Ufundi Dar es Salaam na Chuo cha Ufundi cha Mbeya kuwa vyuo vikuu yaani Dar es Salaam Institute of Technology na Mbeya University for Science and Technology. Tukafanya pia uamuzi wa kuanza kujenga Kampasi mpya ya Kufundishia ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila ambapo kitakapomalizika kitadahili wanafunzi wa udaktari 12,000 kwa mwaka. Wakati tunapanua elimu ya sayansi katika ngazi ya vyuo vikuu, tumefanya hivyo pia katika ngazi ya mafundi mchundo (technicians) kwa kupanua elimu ya vyeti na stashahada katika elimu ya ufundi. Tumeongeza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi (VETA) kutoka 21 mwaka 2005 hadi 28 hivi sasa. Kutokana na upanuzi huu udahili wa wanafunzi katika vyuo hivi umeongezeka kutoka wanafunzi 13,650 mwaka 2005 hadi kufikia 49,329 hivi sasa.  Aidha, katika kipindi hiki pia tunasomesha ndani na nje ya nchi zaidi ya wanafunzi 100 masomo ya gesi asilia na mafuta kwa ajili ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kusimamia sekta ya gesi na mafuta. 
Uandaaji wa Wanasayansi Katika Ngazi ya Awali
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Ndugu Wahitimu;
Tatizo tulilolibaini katika uendelezaji wa sayansi nchini ni msingi dhaifu tuliokuwa nao wa kuwaandaa wanasayansi katika ngazi za awali za elimu yetu. Tukajiuliza kwa nini wanafunzi wetu wanayakimbia masomo ya sayansi na hisabati na ufaulu wamasomo haya unashuka? Tukabaini matatizo matatu: Kwanza, upungufu wa waalimu wenye sifa za kumudu kufundisha masomo ya sayansi; pili, uhaba wa vitabu vya masomo ya sayansi katika shule zetu za sekondari, na tatu ukosefu wa maabara. Tathmini ilionyesha tulikuwa na upungufu wa waalimu ya sayansi 23,500 mwaka 2013 wakati uwezo wa vyuo vyetu ni kuzalisha waalimu 2,500 tu kwa mwaka.  Tumechukua hatua za kuongeza kasi ya upatikanaji wa walimu wa sayansi kwa ajili ya shule zetu.  Hatua mojawapo ambayo tumechukua ni kuongeza nafasi 5,000 za wanafunzi wa kusomea stashahada maalumu ya ualimu wa masomo ya sayansi kwa mwaka 2014/2015 katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Tumefanya uamuzi wa kuwawezesha wanafunzi hao kupata mikopo ya Serikali.
Kwa upande wa vitabu, nilielekeza Wizara ya Elimu kuainisha fedha za vitabu katika bajeti yake na kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kwa ajili ya vitabu. Aidha, niliwaomba marafiki zetu wa Marekani na wakakubali kutuchapishia vitabu milioni 2.1 vya sayansi na hisabati ambavyo vilikwishasambaza mashuleni katika awamu ya kwanza.  Katika awamu ya pili wametuchapishia vitabu milioni 2.5 ambavyo Wizara imekwishavipokea na nimeagiza visambazwe mara moja mashuleni.  Baada ya kugawiwa kwa vitabu hivi tatapunguza tatizo la vitabu vya sayansi kutoka wastani wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne (1:4) mwaka 2009 hadi kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili (1:2).  Lengo letu ni kufikisha wastani wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja (1:1). 
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kuhusu tatizo la maabara, mwezi Novemba, 2012 nilifanya uamuzi wa kujenga maabara za masomo ya kemia, fizikia na baiolojia katika shule zetu za sekondari ili kuwezesha wanafunzi wetu kusoma kwa vitendo. Huku nako kulikuwa na changamoto kubwa sana. Wakati tunapanua elimu ya sekondari kupitia Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES) na hasa ujenzi wa sekondari za Kata tuliongeza idadi ya shule kutoka 828 mwaka 2004 hadi shule 3,551 hivi sasa. Nyongeza hii kubwa imetokana na mchango wa wananchi.  Wamechangishana chochote walichokuwa nacho na kujitolea nguvu za kujenga madarasa, ofisi za shule na nyumba za walimu.  Bahati mbaya tulipokuwa tunahimiza ujenzi wa shule za sekondari za kata  tulikazania kujenga madarasa tukasahau ujenzi wa maabara. Tukajikuta kati ya shule 3,551 za sekondari, ni shule 88 tu (hizi ni zile shule za kongwe) ndiyo zilikuwa na vyumba vitatu vya maabara za kemia, baiolojia na fizikia kila moja. Hivyo tathmini ilionyesha kuwa tunahitaji kujenga maabara kwenye shule 3,463 yaani vyumba vya maabara 10,389. Ujenzi uliendelea lakini haukuwa na kasi ya kuridhisha. Ndipo Novemba, 2012 nikatoa agizo la kila shule ya sekondari ya kati iwe imejenga maabara za fizikia, kemia na bailojia ifikapo mwezi Novemba, 2014.
Agizo langu hilo limewazindua wananchi na viongozi na kuongeza msukumo wa ujenzi wa maabara za sayansi. Taarifa za awali nilizopata wakati nikisubiri taarifa ya tathmini kutoka TAMISEMI inaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 7, 2014, vyumba 3,867 vya maabara sawa na asilimia 37.2 vilikuwa vimekamilika, vyumba 5,891 sawa na asilimia 56.7 vilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na vyumba 631 tu sawa na asilimia 6.1 ndiyo ambavyo ujenzi wake ulikuwa haujaanza. Natoa pongezi za dhati kwa viongozi na wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya.  Kwa ajili ya kumaliza palipoishia nawaongezea miezi sita.  Tumechukua  hatua pia kwa upande wa vitabu vya kiada ambako tulikuwa na upungufu mkubwa kutokana na kutotengwa kwa bajeti za vitabu.
Utafiti
Ndugu Mkuu wa Chuo,
Eneo jingine ambalo tulilazimika kulipa msukumo maalum ni kwenye utafiti, maana sayansi bila utafiti haiwi kamilifu. Hapa tulikumbana na changamoto tatu kubwa.  Kwanza, upungufu wa watafiti katika vyuo na vituo vya utafiti; pili, ukosefu wa fedha za utafiti na uchakavu wa miundombinu ya vituo vya utafiti; na tatu, kukosekana kwa mfumo na utaratibu wa kuwatambua na kuwazawadia wagunduzi, na kuzifikisha tafiti kwa watumiaji ili zitumike kuongeza tija na ufanisi. Nilipotembelea vituo vya utafiti nchini nikakumbana na tatizo la uhaba wa watafiti linalotokana na waliopo kustaafu, kutoajiri wapya kwa sababu ya kusitishwa kwa ajira, na motisha ndogo isiyovutia watafiti vijana.
Kwa kutambua umuhimu wa watafiti na mahitaji yetu ya watafiti kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini na sekta nyingine, nikafanya uamuzi ufuatao: niliagiza waliofikia umri wa kustaafu wapewe mikataba ya kuendelea na kazi. Nilielekeza kuwa vituo vipatiwe kibali cha kuajiri watafiti wapya na kuweka lengo la kutenga asilimia moja ya bajeti ya serikali kila mwaka kwa ajili ya shughuli za utafiti. Kwa upande wa kutambua wagunduzi na watafiti tulianzisha nishani maalum. 
Fedha za utafiti zimekuwa zinapelekwa kwenye Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kupanga mipango ya kufadhili tafiti na kugharamia mafunzo ya watafiti.  Uko mfumo pale COSTECH wa utotoaji teknolojia (technological incubators) ambapo vijana wadogo wanafanya maajabu katika eneo la TEHAMA. Tukaamua pia kulinda haki za wagunduzi kwa kuanzisha sheria namba 7 ya mwaka 1999 kuhusu hati miliki (patent) za wanasayansi wetu.
Ujenzi wa Miundombinu ya Sayansi
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Pamoja na jitihada zetu za kujenga msingi wa sayansi kwa maana ya wanasayansi, tumefanya hivyo pia kwa miundombinu muhimu kwa maendeleo ya sayansi. Miongoni mwa hayo ni ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano (fibre optic) utakaofika kwenye Wilaya zote nchini.  Mkongo huu ndiyo uti wa mgongo wa kubebea maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo TEHAMA ina nafasi maalum. Tumeshakamilisha kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara na mkongo wa taifa, kwa sasa ujenzi unaendelea kuunganisha mikoa ya Zanzibar.  Aidha, tunaendelea na ujenzi wa mkongo wa taifa hadi tuunganishe wilaya zote nchini. 
Mkongo wa taifa wa mawasiliano umewezesha gharama za simu kushuka kwa asilimia 57 kati ya mwaka 2009 hadi 2013 na gharama za intaneti kupungua kwa asilimia 75 kati ya kipindi hicho pamoja na kuongeza kasi ya mtandao kuendana na viwango vya kimataifa. Hii imewezesha urahisi na unafuu katika utoaji wa huduma za kimtandao zikiwemo huduma za elimu, afya, fedha na mawasiliano hususan simu ambazo gharama zake zimepungua sana kutokana na matumizi ya mkongo huo.
Hali kadhalika tumeboresha miundombinu ambayo itasaidia wataalamu wetu kutoa huduma walizokuwa hawawezi kuzitoa na kwa ubora zaidi.  Tumejenga Kitengo cha Kisasa cha Maradhi ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambacho kina uwezo wa kulaza wagonjwa wa moyo 100 na kufanya operesheni za moyo,  tumejenga Kituo cha Utafiti wa Magonjwa (Diagnostic Centre) pale Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho kimemalizika kinasubiri uwekaji wa vifaa hiki kitajihusisha pia na tiba ya magonjwa ya figo na sasa tunajenga Kituo cha Kisasa cha Magonjwa ya Mishipa ya fahamu pale Muhimbili kitakachokuwa na uwezo wa kufanya upasuaji na kutoa tiba ya magonjwa ya mishipa ya fahamu.Hitimisho
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Tumefanya mengi sana katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo pamoja na sayansi na teknolojia nchini. Nyote ni mashahidi wa juhudi zetu hizi. Idadi ya madaktari, wahandisi, watafiti na wataalamu wa fani nyingine za sayansi imeongezeka sana. Hata hivyo hatujaridhika bado maana safari yetu ni ndefu. Tukijitazama wenyewe ni kweli tumepiga hatua, ila tunapojitazama kwa kujilinganisha na wengine bado tuko nyuma sana. Tunapaswa kukimbia wakati wenzetu wanatembea. Chuo hiki cha Sayansi na Teknolojia kina nafasi muhimu katika utekelezaji wa dhamira yetu hiyo. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itashirikiana nanyi na kila mdau katika kukuza sayansi na teknolojia nchini. Naamimi kwa dhati kabisa inawezekana, tena matokeo yanaweza kuonekana katika kipindi cha uhai wetu.
Kwa maneno hayo mengi, nawashukuruni tena kwa heshima kubwa mliyonipa ya kunitunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela.  Sitawasahau kwa wema huu na imani hii mlioionyesha kwangu na Serikali ninayoiongoza. Mmetambua juhudi zetu na kutuvika taji. Kwa kweli mmetutia moyo na kutuongezea ari ya kufanya maradufu ya ilivyo sasa. Tutafika safari yetu ya mwaka 2025 tena ikiwezekana kabla ya mwaka huo.  Nia tunayo, sababu tunayo na uwezo tunao.

Asanteni kwa kunisikiliza. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...