Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amemteua Profesa Mohamed Janabi (pichani) kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ( The Jakaya  Kikwete Cardiac Institute ) iliyoko katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.
Profesa Janabi, ambaye pia ni daktari Mkuu Binafsi wa Rais Mstafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alikuwa akikaimu nafasi hiyo toka kuanza rasmi kwa taasisi hiyo Septemba 2015 na inayoendelea kujizolea sifa kwa huduma zake za moyo  ambazo awali zilipatikana nje ya nchi. Tasisi hiyo hivi sasa inajitegemea.

Taasisi ya Jakaya Kikwete inatoa matibabu pamoja na  mafunzo ya Ubingwa wa juu katika fani ya Upasuaji wa Moyo , Usingizi na Tiba ya Moyo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili( MUHAS) na taasisi za moyo  mbalimbali duniani. 
Hivi majuzi Chuo cha Magonjwa ya Moyo cha Marekani (American College of Cardiology) kimemteua Profesa Janabi kuwa mwanachama (Fellow of American College Cardiology) wa taasisi hiyo yenye wanachama mabingwa 52,000 dunia nzima, akiwa mtu wa kwanza nchini kutunukiwa FCC.
Taasisi hiyo ina matawi (Chapters) dunia nzima isipokuwa Afrika. Afrika Kusini wana mpango wa kufungua Chapter ambapo ili kuianzisha tawi wanahitajika wanachama sio chini ya 20.
Kwa mujibu wa Profesa Janabi, hapa Afrika Mashariki juhudi hizo zimeanza ila kwa sasa Kenya ina Fellows wanane na Tanzania ni mmoja pekee ambaye ni  yeye Profesa Janabi. Wanahitaji fellows wengine 11 kutimiza idadi ya kuwa na tawi.
"Kuna faida nyingi sana kuwa kwenye taasisi hiyo katika kupata elimu ya magonjwa ya moyo, uwezeshaji rasilimali watu (capacity building) na kadhalika.
"Sisi tuna bahati kwani Makamu wa Rais wa ACC Profesa Mike Valentine kutoka Central Virginia Marekani aliwahi kuwa mwalimu wangu. Yeye alikuja hivi majuzi kwenye kongamanoi letu (2nd East Africa Cardiology Conference) na pia alianzisha mchakato wa wa kuanzisha chapter ya Afrika mashariki iwe hapa Tanzania kutokana na mafanikio yanayoendelea JKCI" Profesa Janabi, ambaye sasa ni  Prof. Mohamed Janabi MD., MTH., PhD., FACC,  ameiambia Globu ya Jamii.
Profesa Janabi  ni mmoja kati ya viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali ambao  waliteuliwa kushika nyadhifa July 16,  2016 na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Wengine walioteuliwa ni  Mhe. Augustino Lyatonga Mrema ambaye  ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Prof. William R. Mahalu aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Prof. Angelo Mtitu Mapunda ambaye ameteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kipindi cha miaka mitatu. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
 Wengine walioteuliwa ni Sengiro Mulebya (Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama), Oliva Joseph Mhaiki (Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Gaspar Rutaindurwa (Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Charles Rukiko Majinge (Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili) na Dkt. Julius David Mwaiselage ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...