WANANCHI zaidi ya 265 wa mtaa wa Upendo, Mbezi Salasala wilayani Kinondoni wamelishukuru Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), kwa kuwafikishia huduma ya Majisafi waliyoipatia shida kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja wa serikali za mitaa na DAWASCO, Mjumbe wa mtaa wa Upendo Bw. Robert Massawe amepongeza juhudi zilizofanywa na Dawasco za kuwapatia huduma ya Maji wananchi wa eneo lake na kwamba juhudi hizo zinaendana na kauli ya serikali ya awamu ya tano inayosema hapa kazi tu.

Akieleza historia fupi ya eneo hilo Bw. Massawe alisema tangu watu waanze kuhamia eneo hilo huduma ya Maji ilikuwa ni ya kununua kutoka mtaa mwingine wa mbali ambao ulikuwa umefikiwa na huduma hiyo ya Maji.

“Ilifikia kipindi gharama ya kununua Maji ni kubwa kuliko gharama ya chakula, na wananchi wengi walikuwa wakitumia muda wao mwingi kuhangaika kutafuta Maji jambo ambalo lilikuwa likikwamisha kutekeleza majukumu mengine ya kujenga nchi” alisema Massawe.

Nae mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Bi. Sofia alisema; “Kweli DAWASCO imemtua mama ndoo ya Maji kichwani, sisi akina mama ndio tuliokuwa tukiteseka zaidi na suala la Maji, lakini akina mama wa mtaa huu tulijitoa ili kupambana na janga la Maji ambalo lilikuwa likitukabili, na hatimaye tumefanikiwa kupata huduma ya Maji”

Kwa upande wa Dawasco, Meneja wa Mkoa wa Tegeta, Bw. Alpha Ambokile amewataka wakazi wa mtaa huo kujitokeza kwa wingi kufanya maombi ya kuungiwa huduma ya Maji kwa kuwa tayari huduma hiyo imefika katika makazi yao, baada ya kuhangaika kwa muda mrefu wakisaka huduma hiyo, na ameahidi kuwaunganishia huduma Maji mapema na kwa uharaka zaidi, mara tu baada ya kupokea maombi yao ya kuungiwa huduma.

“Ninawaomba mjitokeze kwa wingi ili kwa pamoja tuweze kuwaunganishia huduma ya Maji, nitawatengea siku yenu maalum ambayo timu yangu ya ufundi itakuja kuwafanyia maunganisho ya Maji, ambao bado hamjafanya maombi, fanyeni haraka ili tuweze kuwaunganishia wote kwa pamoja huduma ya Maji” alisema Ambokile.
Sehemu ya wakazi wa mtaa wa Upendo, Mbezi salasala wakiwa na Mjumbe wa mtaa huo, Bw. Robert Massawe (aliyevaa shati ya bluu), wakisikiliza kwa makini katika kikao cha pamoja na uongozi wa Shirika la Maji safi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO) kutoka mkoa wa Tegeta, baada ya mtaa huo kufikiwa na huduma ya Majisafi na salama kwa mara ya kwanza tangu waanze kuhamia katika makazi hayo, jijini Dar es salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...