Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza  tabia kwa baadhi ya watu wakiwemo wasanii watu wengine mmoja mmoja kutumia mavazi yanayofanana na sare za Majeshi ya Ulinzi na usalama hapa nchini likiwemo Jeshi la Polisi katika shughuli zao za kisanii au katika kazi mbalimbali, Jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za Nchi. 
Kwa mujibu wa Sheria ya kanuni za makosa ya Jinai, sura ya 16 na  marejeo yake ya mwaka 2002,  kifungu cha 178 (1) na  (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama,  kinabainisha wazi kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo  bila kibali kutoka kwa  Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufuatia  kitendo kilichofanywa na kundi la kisanii la “ Original Comedy” kuvaa mavazi yanayoshabihiana na sare za Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam linachukua  hatua za kisheria dhidi ya wasanii hao.
Aidha Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kali kwa mtu ama kikundi chochote kuacha kutumia  mavazi yanayofanana na sare zinazovaliwa na  majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini na atakayebainika hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yake.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wale wote wenye mavazi yanayoshabihiana na sare za majeshi ya ulinzi na usalama  kuzisalimisha mara moja katika vituo vya Polisi vilivyokaribu nao.

 Imetolewa na:
Advera John  Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.         

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. Binafsi nilijiuliza maswali mawili matat khasa tukizingatia hii awamu ya tano ya "HapaKaziTu!" kweli inawezekana hili likafanyika salama salimini bila ya 'kukoromewa'? Mathalan hata zisiwe original uniforms, lakini pia hazikutofautiana kabisa na vazi husika. Ikiwa kila mmoja wetu atafanya hivyo kwa namna moja ama nyingine, moja kwa moja ni kuviondolea hadhi, heshima na uthamani wake vyombo vyetu vya dola. Maana itafika pahala mavazi hayo yatazagaa hata mitaani na kuonekana kama ni 'fashion', ilhali ni mavazi rasmi ambayo yanastahili heshima, hadhi na thamani ya pekee ikiwa kama ni alama mojawapo ya utambulisho wa Taifa letu kwa vyombo vya dola. Hata hivyo afadhali angalau vyombo husika mmeweza kulibaini hilo na kulichukulia hatua kwa kufuata taratibu husika na kulitolea onyo kali kwa wengine ili tabia hiyo isiendelee tena.

    Mungu Ibariki Tanzania.

    ReplyDelete
  2. Tunakubaliana na msemaji wa Polisi kuhusu kuheshimiwa kwa sheria za nchi lakini cha kushangaza Orginal Komedi yale mavazi hayakuwa ya Polisi kuna mapungufu katika mavazi yake hakukuwa na nembo ya polisi na hata mkanda ni wa bendera ya taifa hakuna mtu anayezuiwa kuvaa mkanda wa bendera ya taifa..lakini tuangalie mahakama itaamua je?

    ReplyDelete
  3. Ujinga na ufinyu wa kifikra umetawala kila idara ya serikali...mnashindwa kukamata wahalifu mnahangaika na mavazi ..kwani baada ya harusi walitoka barabarani na kunyanyasa raia wema kama nyie?..nchi yetu ni balaa vyombo vya dola vinatumika na kuamriwa na wanasiasa kwa manufaa yao..tunahitaji sheria huru zitakazo mpa uhuru polisi ,hakimu na jaji siyo haya mnayoyaendekeza..mwisho wake unakuja hata mkibana.Hakuna uvunjifu wa amani uliotendeka hapa sote tunaelewa ni wachekeshaji tafuteni la maana la kufanya.

    ReplyDelete
  4. KWANI KUVAA MAVAZI YANAYOFANANA NA MAJESHI KUNA UBAYA GANI? MBONA KOTE DUNIANI WATU WANAVAA NA HAKUNA MATATIZO? TATIZO NI HAPA KWETU WENYE DHAMANA YA KUSHIKA BUNDUKI TULIOWAPA WANAAMUA LOLOTE WANALOLITAKA KUKANDAMIZA WANANCHI NA KUWAOGOFYA KUJIFANYA MIUNGU WATU....ACHENI UONEVU NINYI POLISI NA ASKARI WENGINE.HAKUNA TATIZO KUVAA NGUO ZINAZOFANANA NA ZENU, AU NINYI SI BINADAAM?

    ReplyDelete
  5. Ni kawaida kwa Kundi hili kutumia mavazi hayo ktk maonesho yao. Ilikuwaje siku zote wasichukuliwe hatua? Ingestahili wapewe onyo ili wasirudie maana kwa kutochukuliwa hatua siku zote ilijenga hisia kuwa hawajavunja sheria.

    ReplyDelete
  6. Nakubaliana na sheria inayozuia wasiohusika kuvaa magwanda ya jeshi ama polisi. Kwani wengine twakumbuka jamaa waliokua wakivaa mavazi ya askari wa usalama wa barabara na kubeba mafaili na kutungojea Chalinze katika mipango yao ya kujitafutia rizki (haramu) Lakini uwepo mwanya rahisi unaowawezesha wasanii kuvaa mavazi hayo, angalau kwenye stage tu. Ikiwa kibali cha kuvaa sare hizo ni lazima uende kwa raisi, hiyo ni shida kidogo.

    ReplyDelete
  7. Sheria ni sheria na lazima iheshimiwe hao watu walijua wazi hilo ni kosa labda uniambie hawakusoma darasa la siasa katika shule ya msingi wangeweza vaa vazi lolote si kwenda kukata mauno huku umevalia nguo zilizo fanana na polisi huu ni udhalilishaji wa chombo cha dola na utovu wa nidhamu ni vizuri ikawa mfano ili wengine wajifunze

    ReplyDelete
  8. Hekima na busara itumike tu katika kutatua hili tatizo...ingawa mimi sina elimu kamili kwenye hili jambo wala sijui kifungu kamili cha sheria kilichovunjwa ktk sheria za Tanzania ila hawa vijana wanaweza kukana hiyo nguo waliyovaa sio bendela ya Tanzania maana Mkemia mkuu atatakiwa kuitwa na kupima color code ya bendera ya Tanzania na kudhibitisha na uenda ikakutwa waliyotumia hao vijana sio halisi (Color code: BS 2660:1955).

    Kingine tu kama Ushauri, ningeshauri wizara husika au jeshi lingeweza kupata fursa katika Radio, TV ata magazeti na kuwa karibu na jamii kwa kutoa elimu kwa wananchi kwa mambo mbalimbali kuhusu jeshi na makosa mbalimbali ambayo wananchi hawatakiwi kuyafanya. Mfano mtoto au kijana akiweza kuona kipindi cha nusu saa tokea akiwa mdogo mpaka anapokuwa mkubwa ni vyema kijana huyu atajua sheria na kuwa raia mwema nchini.

    Kingine jeshi la Polisi au Wizara husika wangeweza kutembelea mashuleni kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka Sekondari au vyuoni na kuwafunza watoto wetu na kutoa elimu mbalimbali; nadhani ingekuwa vyema sana kujenga jamii iliyo bora zaidi. Kuna mikakati mingi sana ya kujenga Taifa lenye raia wanaofahamu sheria na mambo mbali mbali ya Jeshi la Polisi na ni moja ya mikakati mbalimbali inayotakiwa kufanywa under Security Sector Reform (SSR). Wenzetu wanafanya mfano Scotland Yard au Thames Valley Police ya Uingereza, angalia hapa https://goo.gl/O5GFIz au vile vile angalia https://goo.gl/fhZm0x

    Ni ushauri mwema kwa Taifa langu nalolipenda sana na kujivunia na nimeona bora kuutoa kwa manufaa ya Taifa langu na wala sina niha mbaya.

    Asanteni kwa kuweza kusoma maoni yangu na ni matumaini yangu kwamba jeshi langu la Polisi wataweza kufuata nyayo za wenzetu wa nje.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...