WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa halmashauri mkoani Katavi kuwa makini na matumizi ya fedha za maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao na atakayethubutu kuzichezea zitamuunguza.

“Fedha hii tafadhali ni ya moto. Msicheze na hii ya halmashauri tunayoileta hapa halmashauri kwa ajili ya wananchi itawakunguza vidole. Tunaileta kwa madhumini, tunataka wananchi wahudumiwe,“ alisema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Agosti 21, 2016) wakati akihutubia umati mkubwa wa wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Azimio wilayani Mpanda.

Alisema Serikali imeanza kupeleka fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali hivyo ni vema kila mtendaji ahakikishe fedha hizo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi iliyokusudiwa na si vinginevyo.

Waziri Mkuu alisema ni lazima wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri wahakikisha viwango vya ubora wa miradi inayojengwa katika maeneo yao kuwa inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda wilayani Mpanda na kuangalia namna ya kuipanua hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambayo inahudumia mkoa wote wa Katavi.

Alisema hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1957 kama zahanati ambayo kwa sasa yanatumika katika kuwahudumia wananchi wate wa mkoa huo imezidiwa hivyo alimuagiza mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga kuharakisha ujenzi wa hospitali ya mkoa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa wakati mkoa ukiwa kwenye harakati za ujenzi wa hospitali ya mkoa wilaya nazo zianze ujenzi wa hospitali za wilaya ili kuhakikisha sera ya Serikali ya kuwa na hospitali katika kila wilaya inatekelezwa.

Alisema kwa sasa madaktari na wauguzi wanaofanya kazi kwenye hospitali ya Manispaa ya Mpanda wamezidiwa kutokana na kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa kuliko uwezo wao. Hivyo amewataka madaktari na wauguzi wa wilaya ya Mpanda kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzao wa Manispaa.

Awali hospitali hiyo ilikuwa chini ya uongozi wa halmashauri ya Mpanda. Hospitali hiyo kwa sasa ipo chini ya Manispaa ya Mpanda hivyo Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa huo kuboresha huduma kwa kupeleka dawa na vifaa tiba vitakavyoweza hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wa mkoa.

Mkoa umetenga sh. bilioni 1.7 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (kulia kwake) wakiwapungia wananchi wa Mpanda wakati walipowasili kwenye uwanja wa Kashaulili mjini Mpanda kuhutubia mkutano wa hadhara Agosti21, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kashaulili mjini Mpanda Agosti 21, 2016. 
Wananchi wakionyesha mabango wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasili kwenye uwanja wa Kashaulili mjini Mpanda kuhutubia mkutano wa hadhara Agosti 21, 2016. Katika hotuba yake Waziri Mkuu alizitolea majibu kero zote zilizoandikwa kwenye mabango hayo akiwahusisha watendaji wa Halmashauri, mkoa na wilaya.
Wasanii wa kijiji cha Katumba wilayani Mpanda wakicheza ngoma ya Kasimbo wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo akiwa katika ziara ya mkoa wa Katavi Agosti 21, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...