Na Greyson Mwase, Tanga 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa hakuna fidia yoyote itakayotolewa kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme vijijijni unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). 
Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi kutoka katika vijiji vya Kweditibile na Kamgwe vilivyopo katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga. 
Profesa Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza na wananchi. 
Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya usambazaji wa umeme vijijini ambapo iwapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kulipa fidia, inaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya REA 
“Mkumbuke kuwa iwapo fedha hizi zitatumika kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya umeme vijijini, fedha nyingi zitatumika na kukwamisha utekelezaji wa miradi ya REA,” alisema Profesa Muhongo 
Aliendelea kusema kuwa miundombinu ya umeme haihitaji eneo kubwa hivyo haiwezi kuathiri mazao kwenye mashamba kama inavyoaminika na watu wengi Alifafanua kuwa nishati ya umeme ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote nchini vinapata huduma ya umeme na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi 
Alisema kuwepo kwa nishati ya uhakika vijijini kutapelekea wanavijiji kuanzisha viwanda vya kusaga na kukoboa nafaka, kilimo cha kisasa na kuongezeka kwa ufaulu darasani. 
Hata hivyo Profesa Muhongo alitoa agizo kwa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuhakikisha kuwa wananchi waliostahili kuunganishiwa umeme kupitia REA Awamu ya pili wanaunganishiwa kabla ya mwezi Oktoba mwishoni kwa gharama ya shilingi 27,000. 
Wakati huohuo Mbunge wa Handeni Vijijini, Mboni Mhita aliishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kasi kubwa ya usambazaji wa umeme vijijini na kuwataka wananchi wa jimbo lake kuchangamkia fursa hiyo.
 Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akipokea zawadi  ya mbuzi kutoka kwa wakazi wa eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga
 Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisani kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika  kata ya Kwamgwe wilayani Handeni mkoani Tanga.
 Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akielezea mikakati ya usambazaji wa umeme vijijini itakavyotekelezwa na  Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya  Tatu katika eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga
 Mkandarasi kutoka kampuni ya Future Century Limited  ya  Tanzania Hellen Masanja (kushoto) akielezea utekelezaji wa usambazaji wa umeme  katika jimbo la Handeni Vijijini mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) katika eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga. Profesa Muhongo  yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme  vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza na wananchi.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akisikiliza maoni yaliyokuwa yanawasilishwa na mmoja  wa wakazi wa Kata ya Kamgwe wilayani Handeni mkoani Tanga. Kulia ni Mbunge wa Jimbo  la Handeni Vijijini, Mboni Mhita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...