SERIKALI imeipatia Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida zaidi ya shilingi milioni mia tisa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa daraja la mto Saiwa, uliopo katika Kijiji cha Minyughe, tarafa ya Ihanja,wilayani Ikungi ili kuwanusuru wananchi wa vijiji vya Minyughe, Majengo, Mayaha, Mtavira na Mteva wasipoteze maisha yao kwa kusombwa na maji yanayosafiri kupitia mto huo.

Kukosekana kwa daraja hilo kwa zaidi ya miaka kumi sasa kumechangia watu na mifugo kupoteza maisha, magari kusombwa na maji yanayosafiri kupitia kwenye mto huo.

Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Minyughe na Misake, tarafa ya Ihanja, wilayani hapa, Mbunge wa jimbo la Singida magharibi, Elibariki Kingu aliweka bayana kwamba gari moja la Kampuni ya vinywaji baridi la Pepsi, lilizama na kisha kudidimia kwenye mchanga ambapo mpaka leo halijaweza kutolewa.
Mmoja wa wananchi wanaosafirisha mizigo yao kwa kutumia usafiri wa baiskeli akijaribu kuvuka katika eneo la mto huo ambao kwa sasa umekauka kama alivyonaswa na kamera ya mwandishi wa wetu.

Mbunge huyo ambaye alikuwa katika ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa daraja hilo iwapo Mkandarasi wake ameanza shughuli za ujenzi wa daraja hilo.

Kwa upande wake Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri hiyo,Haruna Mbegalo licha ya kukiri Halmashauri ya wilaya hiyo kupokea fedha za ujenzi wa daraja hilo,lakini alitofautiana na Mbunge huyo kwa kudai kuwa Halmashauri hiyo imepokea zaidi ya shilingi milioni mia saba kwa ajili ya shughuli hizo.

“Tatizo la mto Minyughe au mto saiwa tunalishughulikia, Mkandarasi ameshapatikana,ameshaonyeshwa site na ameanza zile taratibu za awali na sasa hivi alikuwa anasubiri maji yapungue au mto ukauke ili aweze kuanza shughuli za ujenzi”alifafanua Mhandisi Mbegalo.
Kwa mujibu wa Mhandisi huyo kiasi hicho cha zaidi ya shilingi milioni mia saba zilitengwa katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita wa 2015/2016 na kwamba shughuli za ujenzi huo zimekwishaanza kwa kufanyika kwa upembuzi yakinifu ambapo mpaka sasa zaidi ya shilingi milioni 103 zimetumika.

Hata hivyo akizungumzia suala la fidia kwa wananchi waliokuwa wakiishi kuzunguka eneo la mto huo wanaotakiwa kuhama kupisha mradi huo,Mhandisi Mbegalo alikiri kuwa hakuna fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya kuwalipa wananchi hao.

Wakizungumzia madhara yaliyopatikana na ambayo endapo daraja hilo halitajengwa yataendelea kutokea,baadhi ya wananchi wa Vijiji hivyo waliyataja kuwa ni pamoja na kukwama kwa magari ya abiria na mizigo pamoja na binadamu na mifugo kupelekwa na maji yanayopita kwenye mto huo.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi sasa zaidi ya magari ya mizigo 15,mabasi ya abiria 5,wanyama wafugwao zaidi ya 50 walisombwa na maji huku magari yakizama kwenda chini ya maji na kushindikana kuvutwa.
Muonekano wa sasa ukiwa umekauka mto Saiwa uliopo katika Kijiji cha Minyughe,Tarafa ya Ihanja,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida ambao ni tishio kwa watu wanaopia katikati ya mto, magari ya mizigo, magari ya abiria pamoja na mifugo inayokwenda kunywa maji.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Minyughe,tarafa ya Ihanja waliokutwa wakinywa maji kwenye mto Saiwa walipokuwa wakirudi kutoka shuleni wakienda nyumbani baada ya masomo yao ya asubuhi.(Picha zote Na.Jumbe Ismailly).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Wananchi waelimishwe namna ya kupanda miti na kuitunza kwa ajili ya mazingira na uhai wao. Panda mti utunze ukutunze.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...