THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

Halmashauri zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa sasa kubanwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe.George Simbachawene akikata utepe kuzindua rasmi gati ya kisasa katika kisiwa cha Songosongo jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe.Godfrey Zambi na nyuma ya Mkuu wa mkoa ni Mhandisi Gilbert Mwoga, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi.

Na Mathew Kwembe, Lindi

Serikali imesema kuwa halmashauri zinazodaiwa na bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa na ambazo zimeshindwa kurejesha malimbikizo ya madeni inayodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa hazitaruhusiwa kukopa katika taasisi nyingine za kifedha hadi zikamilishe kwanza deni llinalodaiwa na Bodi hiyo.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.George Simbachawene wakati alipotembelea maonyesho ya wakulima ya nane nane yanayofanyika kitaifa mkoani Lindi.

Waziri Simbachawene alisema kuwa halmashauri zote zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa hataziruhusu kuomba mkopo wa fedha kutoka taasisi nyingine zozote hadi kwanza zikamilishe deni walilokopa kutoka katika Bodi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe.George Simbachawene akiangalia bustani ya mbogamboga inayomilikiwa na Shirika la SUMA JKT.

Waziri Simbachawene alisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha kuwa fedha zote zilizokopwa na halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo zinarejeshwa ili mfuko huo uwe endelevu na kuzipa fursa halmashauri nyingine kukopa fedha kutoka kwenye Bodi hiyo.

Aidha Waziri Simbachawene ameitaka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kuandaa utaratibu maalum utakaoziwezesha halmashauri zinazokopa fedha kupitia taasisi hiyo zinarejesha fedha zake moja kwa moja benki bila ya kukumbushwa mara kwa mara.

Hatua hiyo ya Waziri Simbachawene inafuatia maelezo ya Mhasibu wa Bodi hiyo Bwana Mourice Kobalogira kumweleza Waziri kuwa Halmashauri nyingi zilizokopa fedha kupitia Bodi hiyo zimekuwa zikikwepa kurejesha fedha kwa visingizio mbalimbali hali inayosababisha chombo hicho kushindwa kuzikopesha halmashauri nyingine.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe.George Simbachawene akifurahia baada ya kushuhudia bustani ya mboga mboga aina ya bilinganya ambayo imestawi vyema katika eneo la maonyesho ya Nanenane mkoani Lindi. Bustani hiyo inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia shirika lake la SUMA JKT.

Bwana Kobalogira alimweleza Waziri Simbachawene kuwa hali ya urejeshaji mikopo imekuwa ya kusua sua mno ambapo hadi kufikia sasa maombi mapya ya halmashauri zinazotaka kukopa kupitia bodi hiyo yamefikia bilioni 49 lakini Bodi imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni tisa tu.

“Tatizo Mhe.Waziri ni kuwa halmashauri hazizingatii urejeshaji kulingana na mikataba yao waliyoombea mikopo, mfano mtu kama aliomba mkopo kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi, basi fedha za urejeshaji zitoke katika mapato ya stendi, au kama halmashauri iliomba mkopo kwa ajili ya ujenzi wa soko, fedha za urejeshaji zitokane na mradi huo, lakini halmashauri nyingi zimekuwa hazifanyi hivyo,” alisema bwana Kobalogira.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Simbachawene aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha kuwa inaweka kipengele katika mkataba wa mkopo utakaozibana halmashauri hizo kurejesha fedha ilizoombea mkopo kulingana na masharti yaliyowekwa na bodi hiyo, tofauti na ilivyo sasa ambavyo halmashauri nyingi zilizopewa mkopo zimekuwa zikikwepa kutekeleza suala la marejesho.
Mhasibu kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa Bwana Mourice Kobalogira akimweleza waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe.George Simbachawene wakati alipotembelea banda la Ofisi katika Maonyesho ya Nane nane yanayofanyika kitaifa mkoani Lindi.