NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amewataka wakuu wa idara kwenye Halmashauri nchini kuacha kufanya kazi kimazoea kwa kuishia kukaa maofisini bila kwenda maeneo ya vijijini ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Jafo ametoa kauli hiyo ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi katika Halmashauri za Singida, Shinyanga, Uyui na Sikonge mkoani Tabora. Akizungumza na watumishi katika halmashauri hizo, Jafo amesema imekuwa ni mazoea kwa wakuu wa idara kujifungia maofisini bila kufika vijijini kukutana na wananchi ili waweze kutatua kero zao.

Hata hivyo amewaonya baadhi ya wakuu wa idara wanaowanyanyasa watumishi wa kada za chini kwa kuwapendelea baadhi yao katika mchakato wa upandishaji wa madaraja. Amewaagiza wakurugenzi kupangiana malengo na wakuu wa idara kuwa ni kitu gani kila mmoja wao atakifanya ndani ya mwaka mmoja kwenye eneo lake la kazi.

Aidha amesema na wakuu wa idara wafanye hivyo hivyo kwa watu wao wa chini ili kila mtu apimwe kiutendaji ndani ya mwaka mmoja. Jafo amekemea tabia ya wakurugenzi wa Halmashauri kupitisha malipo ya miradi ambayo inakuwa imejengwa chini ya kiwango na kwamba ni ubadhirifu wa fedha za wananchi kwa kuwa haifikii malengo yaliyokusudiwa.

“Hali kama hii imejitokeza kule halmashauri ya kondoa mkoani Dodoma serikali imefanya uchunguzi na tayari hatua zimechukuliwa kwa watendaji 8 ambao wamesimamishwa kazi na wengine kufikishwa mahakamani kutokana na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo…Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa yeyote atakayefanya vitendo kama hivi,”amesema Jafo

Naibu Waziri huyo kwa takriban wiki mbili amefanikiwa kutembelea halmashauri 15 na kutembelea miradi 63 ikiwemo miradi ya hospitali, vituo cha afya na zahanati, miradi ya elimu, maji, na miundombinu ya barabara.

Miongoni mwa Halmashauri alizozitembelea ni pamoja na Halmashauri ya Kilolo, Mufindi, Mafinga, Iringa, Chemba, Kibaha, Korogwe mji, Halmashauri ya Korogwe, Jiji Arusha, Kisarawe, Singida, Manispaa ya Shinyanga, Halmashauri ya Shinyanga, Uyui, na Sikonge .

Jafo bado anaendelea na ziara yake katika mikoa ya Katavi na Rukwa kwa lengo kutimiza matakwa ya watanzania. 

Naibu Waziri Jafo akiwa na Mbunge wa vitimaalum Mkoa wa Shinyanga, Azza Hamad walipotembelea mradi wa maji ulioanza kutoa maji katika kijiji cha Tinde Mkoa wa Shinyanga.
Jafo akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Tinde Mkoa wa Shinyanga.
Jafo akizungumza na wananchi na watumishi katika mradi wa maji kijijin cha Tinde.
Naibu Waziri Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na usalama wa Wilaya ya Shinyanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...