THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

KAIRUKI AIBUA MADUDU MAPYA YA WATUMISHI WA UMMA MKOA WA KAGERA

 Editha Karlo,wa blog ya jamii,Kagera.

Jumla ya watumishi 3,374 kutoka katika halmashauri zote na sekretarieti ya Mkoa wa Kagera wamebainika kuwa na taarifa chafu, kufuatia uhakiki wa watumishi unaoendelea katika maeneo mbalimbali Mkoani hapa.

Taarifa ya watumishi hao ilitolewa na waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Angella Kairuki, baada ya kupokea taarifa ya Mkoa kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Kagera meja jenerali mstaafu Salum Kijuu, katika ofisi ya mkuu wa mkoa huo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.

Waziri Kairuki alisema kuwa watumishi hao walibainika kutokana na majina wanayoyatumia kazini kutokuwa sahihi, kutoonekana kwa taarifa zao za kielimu, vyeo vyao havijaainishwa, wenye umri wa miaka 60 na wengine hawana akaunti za benki.

“Kuna watu zaidi ya mmoja wameonekana wanatumia cheti kimoja kwenye sekta tofauti hapa Kagera,cheti hicho hicho utakuta ni muuguzi, mwingine mwalimu na mwingine yuko katika ajira nyingine, au mtumishi anakutwa hana akaunti ya benki ina maana mshahara wake anapokelea wapi?alihoji Kairukia.

Akitoa mchanganuo wa watumishi hao alisema kuwa katika sekretarieti ya mkoa kuna watumishi ambao data zao ni chafu wapatao 21 wakiwamo 20 wanaotumia majina yasiyo sahihi na mmoja anayeonekana kuwa na umri wa miaka 60 ambapo anatakiwa awe amestaafu.

Alisema halmashauri ya wilaya inayoongoza ni Missenyi iliyobainika kuwa na watumishi wa wenye taarifa chafu ambao ni 1,608, wakiwamo wenye majina yasiyo sahihi 838, ambao taarifa zao za elimu hazionekani 761 na wanne vyeo vyao havijaainishwa.

Kairuki alisema halmashauri ya wilaya inayofuatia ni Ngara ikiwa na watumishi hao 454, ambao majina yao siyo sahihi ni 438, wasio na taarifa za kielimu watano, ambao vyeo vyao havijaainishwa ni watatu na wawili hawana akaunti za benki.

Nyingine ni halmashauri ya wilaya ya Bukoba ambayo imebainika kuwa na watumishi hao 429, wakiwamo wanaotumia majina yasiyo sahihi 83 na wasio na taarifa za kielimu 346, huku halmashauri ya wilaya ya Biharamulo ikiwa na watumishi 296 wakiwamo wa majina yasiyo sahihi 11 na wasio na taarifa za kielimu 285.

Waziri huyo alisema kuwa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa wamebainika watumishi hao 234, ambao wanatumia majina yasiyo sahihi ni 206, wasio na taarifa za kielimu 26 na wawili vyeo vyao havijaainishwa. Katika halmashauri ya Karagwe waliobainika ni 211, ambao wanatumia majina yasiyo sahihi ni 205, wawili taarifa zao za elimu hazionekani na watumishi wanne vyeo vyao havijaainishwa.

Kairuki alisema katika manispaa ya Bukoba ni watumishi 70 wakiwamo 60 wanaotumia majina yasiyo sahihi na kumi hawana taarifa za kielimu, huku halmashauri ya wilaya ya Muleba ikibainika kuwa na watumishi 51 wakiwamo wa majina yasiyo sahihi 47 na ambao taarifa zao za elimu hazionekani wanne.
 Waziri wa ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora,Mh.Angella Kairuki akiongea na watumishi wa serekali kutoka idara  mbalimbali za Mkoa wa Kagera juu ya kero zao kwenye ukumbi wa ELCT
 Baadhi ya watumishi wa serekali  kutoka idara mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma Angella Kairuki(hayupo pichani) wakati akisikiliza kero zao