Na Ankal
Nilipopata tarifa kuwa Blogger mkongwe Bi. Arianna Huffington (pichani) anastaafu
kutoka Mtandao wa Jamii ama blog ya Huffington Post
(BOFYA HAPA) ili kuanzisha mtandao wa Thrive Global unaohusiana na staili za maisha na afya (BOFYA HAPA), nilistuka sio kidogo maana daima amekuwa kichocheo changu kikubwa katika tasnia hii ya habari za mtandaoni.
(BOFYA HAPA) ili kuanzisha mtandao wa Thrive Global unaohusiana na staili za maisha na afya (BOFYA HAPA), nilistuka sio kidogo maana daima amekuwa kichocheo changu kikubwa katika tasnia hii ya habari za mtandaoni.
Bi. Huffington alianzisha mtandao wake huo wa Huffington Post
mwaka 2004 (Globu ya Jamii ilianza mwaka 2005) baada ya Rais George W. Bush
kuchaguliwa kuongoza Marekani kwa mara ya pili, na wakati huo huo vita ya Iraq
ilikuwa ikiendelea.
Blog hiyo ilianza kiutani-utani kwa taarifa za kawaida na
michango hii na ile kutoka kwa marafiki zake, kabla ya sio tu kuwa moja ya blog
kubwa duniani bali pia kampuni kubwa ya
habari mtandao duniani yenye matawi katika
nchi 15 kwa jina la Huffington Post Media Group.
Kampuni hiyo hivi sasa inaajiri watu 850 kila pembe ya dunia
na imeendelea kuwekeza katika kusaka na kutoa habari mtandao kwa picha, maandishi
na video na kujizolea tuzo kibao ikiwemo ya Pulitzer Prize ambayo ni kubwa
kuliko zote.
Japokuwa Bi. Huffington
amekuwa akijihusisha na maswala ya siasa
muda wote, ikiwemo kumpinga waziwazi mgombe urais Donald Trump tokea atangaze azma
yake hiyo , pia amekuwa akitumia muda
wake mwingi katika maswala ya afya na maisha kwa kuandika kitabu kuhusiana na mambo hayo mwaka 2014 kiitwacho
Thrive na mwaka huu kuandika kingine kiitwacho The Sleep Revolution. Mnamo mwezi wa June mwaka huu akatangaza
kuanzisha mtandao wa Thrive Global.
Katika mahojiano, Bi. Huffington anaripotiwa kusema kuwa hawezi kujenga kampuni
mpya kama kazi ya pembeni, hasa katika wakati huu ambapo wawekezaji wameshaanza
kuwekeza mamilioni ya dola kwenye kampuni ya Thrive Global.
Majukumu yake yamewahi kubadilika mara moja huko nyuma,
hususan pale kampuni ya AOL kuinunua blog
ya Huffington Post mwaka 2011 kwa dola milioni 315. Katika makubaliano hayo Bi. Huffington alibakia kuwa Mhariri Mkuu na
wakati huo huo Rais wa Huffington Post Media Group.
Kuondoka kwake katika kampuni hiyo kumekuja wakati kampuni
ya Verizion ilipoinunua kampuni ya AOL kwa dola bilioni 4.4, na kutangaza pia kutaka
kuinunua Yahoo kwa dola bilioni 4.8. Ila yeye alikana kuwa kuondoka kwake
kunahusiana na manunuzi hayo, bali alisema muda ni muafaka wa kuanza mambo
mengine.
Nilipata bahati ya kukutana ana kwa ana na Bi. Arianna
Huffington huko Davos, Uswisi, mnamo Januari 26 mwaka 2012 (BOFYA HAPA) na kubadilishana naye
mawazo pembezoni mwa mkutano wa dunia wa
uchumi. Nilifarijika sana pale mama huyo nguli wa habari za mitandaoni
aliposema anaifahamu Michuzi Blog nami nikamfurahisha
kwa kumwambia nafuatilia kila hatua anayopitia.
Nikikumbuka kukutana kwetu huko Davos na kuifikiria kauli
hiyo, mie pia sasa nimeanza kujiuliza
endapo kama sasa ni muda muafaka wa kuachana na Globu ya Jamii na kuendeleza Libeneke kwa njia
zingine?
Jibu nitalitoa ifikapo Septemba 8, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya
miaka 11 ya Globu ya Jamii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...