ZIWA Ngozi ni moja ya maziwa duniani ambayo yametokana na kulipuka kwa Volicano,ziwa hilo Lililopo Wilaya ya Rugwe Mkoani Mbeya nchini Tanzania katika kijiji cha Mbeye one au mchangani ni la pili kwa ukubwa Afrika.

Asili ya jina Ngozi linatokana na jina la kabila la Wasafwa linalomaanisha kitu kikubwa ‘’LIGOSI’’ na ziwa hilo tangu zamani lilikuwa chini ya himaya ya kabila la wasafwa katika koo mbili za machifu ikiwemo ya Chifu Mrotwa Mwalingo (akitawala upande wa magharibi) na chifu Mlotwa Mwalupindi(aliyekuwa akitawala upande wa Mashariki).

Ziwa Ngozi lipo usawa wa mita 2600 kutoka usawa wa bahari na limezungukwa na misitu minene ya asili katika safu za milima ya Uporoto na kuna hekari 9,332 ambazo zimetengwa kwajili ya uhifadhi wa eneo hilo.

Ndani ya ziwa Ngozi kuna visiwa viwili vinavyovutia sana kwa muonekano na inatajwa visiwa hivyo hutumika kwajili ya mazalia ya bata pori na ndege wengine.

Ziwa hilo lina kina cha mita 74 na urefu wa kilometa 2.5 pamoja na upana wa kilometa 1.5 na eneo lake ni km za eneo 3, na pembezoni mwa ziwa hilo kuna mabonde makubwa yenye misitu mikubwa ya miti ya asili na baadhi ya mimea hiyo ni migomba ya asili na mianzi ya asili pamoja na miti mirefu na maua ya aina mbalimbali.

Umbali wa kutoka katika Kijiji cha Mbeye one au Mchangani hadi katika ziwa hilo la Ngozi ni zaidi masaa mawili kwa miguu,ingawa kabla ya kufika katika ziwa hilo kuna sehemu ya kupunzika ambayo kwa Lugha ya Kisafwa hufahamika kama NZEYENZU.

Pia sehemu ya kupunzika hutumika kwajili ya watalii wenye magari na usafiri mwingine kuyaacha hapo,na umbali kutoka sehemu ya kupumnzika hadi sehemu linapopatikana ziwa hilo ni nusu saa(30 saa) ambapo wageni na watalii hutumia muda huo kupandisha sehemu kubwa iliyoinuka.

Kuna njia nyembamba iliyotengenezwa kwa umahili mkubwa wakati wa kupandisha mwinuko huo kuelekea ziwa Ngozi,na ukiwa njiani ni kawaida kusikia milio ya ndege wa aina mbalimali pamoja na ngedere ingawa si rahisi sana kuwaona kutokana na misitu minene ya asili yenye miti mirefu na mabonde ya ajabu.

Unapofika eneo la Ziwa Ngozi utastajabu umbo la ziwa hilo,huku maji yakionekana kuwa chini kutoka sehemu uliyosimama na kwa mbali ni jambo la kawaida kusikia milio ya mara kwa mara ya bata pori ndani ya ziwa hilo.

Muonekano wa ziwa Ngozi unavutia sana bila kukuchosha wakati wa kulitazama ,ingawa ni kawaida kwa ukungu kutawala sehemu kubwa ya eneo la ziwa hilo kwa siku na kiwango cha joto katika eneo hilo ni 18 °C.

Ukiwa eneo la ziwa hilo inahitajika uangalifu wa hali ya juu kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na mapango yaliyopo pembezoni na ambayo ukikanyaga vibaya unaweza kuporomoka nakupoteza maisha na ni jambo la busara kuzingatia maelekezo ya watalaam.Maajabu mengine ni kuwa maji ya Ziwa Ngozi hubadilika rangi kila wakati zikiwemo rangi za Bluu ,nyeupe na nyeusi na ladha ya maji hayo ni ya chumvi na mbayo hutumika kwa imani za kimila.

Watu mbalimbali waliyoyafikia maji ya ziwa ngozi wanaweka wazi kuwa ni kazi ngumu ya kufika huko kutokana na kushuka chini kwa kutumia kushika mizizi ya miti kwa muda wa kati ya dk 45 hadi dk 60 na wa kupandisha kutoka chini kabisa huwa ni kazi ngumu sana.

Ndani ya ziwa hilo kuna samaki ambao ni vigumu sana kuwavua kutokana na miundo mbinu ya Ziwa hilo ,ambapo sehemu ya samaki hao wanadaiwa kuliwa na bata wa porini na ndege wengine tofauti wanaokula samaki. 

Mbali na ziwa Ngozi kuna maziwa mengine madogo sana yenye asili ya volkano yaliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ambayo ni Kisiba, Chungululu,Ikapu, Itamba, Masoko, Ilamba,Ndwati, Katubwi Itende,Lusanje na Kingili.,pia kuna ziwa Chala( Dschalla) ambalo lipo nje kidogo ya mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ndani ya Mlima Kilimanjaro..

Je wajua Maziwa makubwa duniani yenye muundo wa ziwa Ngozi(a natural lake occupying the caldera),Ziwa Toba linalopatikana eneo la Sumatra nchini , Indonesia ndiyo ziwa pekee duniani linaloongoza kwa ukubwa lina urefu wa Kilometa 100 na upana wa kilometa 30 na eneo ni km za eneo 1,130 na kina ni mita 500.

Maziwa mengine ni Pinatubo linalopatikana nchini Ufilipino lina kina cha mita 600 na upana wa km 2.5 na ziwa Heaven linalopatikana Korea ya Kaskazini lina Urefu wa mita 213 na eneo la Km 9.82,maziwa mengine ni IRAZÚ nchini Costa Rica,Cuicocha, nchini Ecuador na mengineyo.

Imeandaliwa na Ng'oko Innocent

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...