Na Grace Michael

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kazi nzuri na kubwa ya upimaji wa afya za wananchi iliyofanyika katika maonesho ya Kitaifa ya Nane Nane mkoani Lindi.

Pongezi hizo alizitoa wakati alipotembelea banda hilo katika kilele cha maonesho hayo ambapo alisema kuwa kazi inayofanywa na Mfuko inawasaidia wananchi kutambua afya zao lakini pia elimu ya kuepukana na maradhi yasiyoambukizwa.

“NHIF nawapongeza sana kwa kazi kubwa mliyoifanya mahali hapa, nimepata taarifa zenu kwamba mnapima afya za wananchi bure...hongereni sana na fursa hii iwafikie na wengine” alisema Makamu wa Rais.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga akitoa maelezo ya huduma zilizotolewa na Mfuko katika maonesho ya Nane Nane mkoani Lindi kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu wakati alipotembelea banda hilo. Kati kati ni Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda. 

Katika maonesho hayo, Mfuko ulitoa huduma mbali zikiwemo za elimu ya namna ya kunufaika na huduma za Mfuko, usajili wa wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii, upimaji wa afya kwa wananchi ikiwemo saratani ya matiti, hali lishe, sukari na shinikizo la damu pamoja na elimu ya kuepukana na magonjwa hayo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda alitoa mwito kwa Watanzania kuhakikisha wanatumia fursa zinazotolewa na Mfuko ikiwemo kujiunga na huduma za Mfuko ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote.
Meneja wa Mkoa wa Lindi Fortunata Raymond akitoa maelezo ya huduma kwa Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda alipotembelea kuona huduma zinazotolewa. 

Alisema kuwa Mfuko umejipanga kuhakikisha unahudumia idadi kubwa ya Watanzania hivyo ni vyema wakachangamkia huduma zilizopo kwa kuwa zinagusa makundi mbalimbali yakiwemo ya Watoto, wanafunzi, watu binafsi, wajasiliamali na makundi mengine.

“Nawahamasisha tu Watanzania kujiunga na huduma za Mfuko huu kwani zimezingatia mahitaji ya kila Mtanzania na huu ndio mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa kwenye Mfumo wa Bima ya Afya,” alisema Mama Makinda.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko Bw. Bernard Konga aliwahakikishia Watanzania kuwa, Mfuko uko imara na umejipanga kutoa huduma bora ambazo zitakidhi mahitaji yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene akizungumza na Meneja wa NHIF Lindi baada ya kuona huduma zinazotolewa na Mfuko huo. 

Alisema kuwa Mfuko unaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika huduma zake kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya wananchi ili kuwezesha mpango wa Serikali wa afya bora kwa wote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...