Na Greyson Mwase, Shinyanga
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ameitaka
kampuni ya Pangea Minerals Ltd ya Canada inayofanya shughuli za
utafutaji wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Mwakitolyo Mkoani
Shinyanga kuachia sehemu ya Leseni yake ili eneo hilo litengwe na
kumilikishwa Wachimbaji Wadogo.
Akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na Wawakilishi
wa Wachimbaji Wadogo pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Pangea
Minerals Ltd mkoani Shinyanga, aliitaka kampuni hiyo ambayo imeanza
mazungumzo ya kuuza eneo hilo kwa kampuni ya Busolwa Mining Ltd,
kuachia sehemu ya leseni yake yenye namba PL 5044/2008 ambayo kwa
sasa wananchi wanaokadiriwa kufikia 3000 wanajishughulisha na
uchimbaji mdogo wa dhahabu katika eneo hilo tangu mwaka 2011.
Alifafanua kuwa ili kuepuka mgogoro huo ambao umedumu kwa muda
mrefu kati ya kampuni hiyo na wananchi hao, ni vyema kampuni hiyo itoe
ushirikiano kwa kijiji hicho kwa kuachia sehemu ya leseni yake ili wananchi
nao wapate maeneo ya kufanyia shughuli za uchimbaji wa madini.
Dk. Kalemani aliitaka kampuni hiyo kuachia eneo hilo kwa Kamishna wa
Madini ifikapo Agosti 17, 2016 ambapo eneo hilo litaanza kugawanywa
kwa wananchi kuanzia Septemba 2, 2016.
Wakati huohuo Naibu Waziri Kalemani aliwataka wachimbaji wadogo
kuheshimu sheria za nchi na kukubali kuhamia eneo litakalotengwa kwa
ajili yao ifikapo tarehe 2 Septemba, 2016.
Naye Mwakilishi na Mkurugenzi kutoka kampuni ya Pangea Minerals
Limited Ltd, Deo Mwanyika alikubali maamuzi hayo na kueleza kuwa
kampuni ipo tayari kukabidhi sehemu ya leseni hiyo ili iweze kutumiwa na
wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga aliipongeza serikali kwa mikakati yake
ya kusaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo ya kujiajiri kwa ajili
ya kujiongezea kipato.
Aliwataka Wachimbaji Wadogo kutojihusisha na vitendo vya kiharakati na
kuwarubuni baadhi ya wachimbaji na kupinga juhudi za Serikali kwa
kuchochea vurugu migodini badala yake wayatumie maeneo hayo
waliyotengewa kwa shughuli za kiuchumi.
Eneo la Mwakitolyo ni kati ya maeneo yenge utajiri wa dhahabu hapa
nchini yanayomilikiwa na kampuni ya Acacia kupitia kampuni yake tanzu ya
Pangea Minerals Ltd.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akisisitiza jambo
katika moja ya vikao vyake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...