Na Hilali
Ruhundwa, COSTECH
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce
Ndalichako (pichani) , anatarajiwa kufungua kongamano la tano la Sayansi, Teknolojia na
Ubunifu linaloandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),
litakalofanyikia Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Hassan Mshinda,
kongamano hilo la siku tatu litawakutanisha watafiti, wanasayansi, na
wabunifu ambapo uwasilishaji wa matokeo ya tafiti mbalimbali na maonesho ya
kazi za kisayansi na ubunifu vitakuwa sehemu kubwa ya kongamano hilo.
Amesema dhima ya kongamano
hilo ni “Utafiti Wenye Msukumo wa
Kibiashara ni Kichocheo Kuelekea Ukuzaji na Maendeleo ya Viwanda”, ikiwa ni kuunga mkono jitihada
za serikali ya awamu ya tano kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa
2025 katika kuimarisha uchumi wa Taifa unaosukumwa na maendeleo ya viwanda.
Katika kongamano hilo pia,
watafiti waliobobea kwenye taaluma mbalimbali, wabunifu, , watunga sera na
wadau wengine kutoka sekta za umma na binafsi watajadili kwa kina na kutoa
majibu ya namna sayansi, teknolojia na ubunifu vinavyoweza kukuza maendeleo ya
viwanda kwa kasi zaidi.
Dkt. Mshinda pia ameeleza kwamba katika kongamano hilo,
watafiti wa nchini Afrika ya Kusini na watafiti wa Kitanzania watawasilisha
matokeo ya miradi kumi na mitano iliyofadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya
Afrika ya Kusini, kupitia Mfuko wa Taifa hilo wa Urafiti (NRF) na serikali ya
Tanzania kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia
(MTUSATE), uliopo COSTECH.
“Miradi hiyo ilianza kufadhiliwa kwa ushirikiano wa nchi hizo
mbili tangu mwaka 2013 na ilipata ufadhili wa miaka miwili ambapo kila nchi
ilichangia zaidi ya shilingi milioni mia tano. Matokeo ya tafiti zao kweli
yanatupa fursa ya kuwashirikisha watanzania ili wafahamu kinachoendelea katika
nyanja ya utafiti,” amesema Dkt. Mshinda .
“Tunawaomba Watanzania kwa ujumla kutembelea tovuti ya Tume
ambayo ni www.costech.or.tz kupata
taarifa zaidi za kongamano hilo”, ameongeza.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka
1986, COSTECH ambayo ni mshauri mkuu wa serikali katika matumizi ya sayansi na
teknolojia kwa maendeleo ya Taifa, imekuwa ikifadhili tafiti katika maeneo
mbalimbali hususani kilimo, afya, ufugaji, uvuvi, TEHAMA, na ubunifu huku
ikishirikiana na wadau mbalimbali kama Shirika la Maendeleo la Swideni (Sida),
Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID) kupitia Mfuko wa Ubunifu
na Maendeleo ya Watu (HDIF).
Itafanyika tarehe ngapi. manake hata kwenye website yao hakuna tarehe.
ReplyDelete