Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin wakwanza kushoto.(Katikati ni mkalimani)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Agosti, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb(TUS) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga ambapo Rais Magufuli ameipongeza Jumuiya ya Dawoodi Bohra kwa juhudi kubwa inazofanya katika kutoa huduma za kiroho na pia kushiriki katika maendeleo.
Dkt. Magufuli amewakaribisha wana Jumuiya hiyo kuwekeza hapa nchini hususani katika sekta ya viwanda na pia amewakaribisha katika Maadhimisho ya Jumuiya ya Dawoodi Bohra duniani yanayotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam Mwezi Oktoba 2016.
"Tanzania ni nchi nzuri, tumekuwa na ushirikiano mzuri sana na wenzetu wa Jumuiya ya Bohra, hivyo njooni mfanye biashara na Tanzania,  tumepanga katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 Tanzania iwe nchi ya viwanda, kwa hiyo tunawakaribisha kuja kuanzisha viwanda vya kutosha" Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali yake ya awamu ya Tano, na pia ameahidi kuwa Jumuiya ya Dawoodi Bohra ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika maendeleo.
Aidha, Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb amemkabidhi Rais Magufuli hundi ya Dola la Marekani Elfu Hamsini na Tatu (USD-53,000) sawa na Shilingi Milioni 116 za Kitanzania kwa ajili ya kuchangia utengenezaji wa madawati ya wanafunzi kwa shule mbalimbali hapa nchini na pia amekabidhi hundi ya Dola za Marekani Elfu Ishirini na Moja (USD-21,000) sawa na Shilingi Milioni 46 kwa ajili ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Saharawi Mhe. Brahim Ghali iliyowasilishwa na Mjumbe Maalum wa Rais huyo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Bachir Moustapha Sayed.Pamoja na kupokea barua hiyo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiarabu ya Saharawi na pia itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi wa Saharawi kupata haki ya kuamua hatma yao.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
17 Agosti, 2016.
 Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin akimuombea dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na  Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin wengine katika picha ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir,  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga pamoja na viongozi wengine wa BAKWATA na wa madhehebu ya Bohora.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na  Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin wengine katika picha ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir pamoja na viongozi wengine wa Madhehebu ya Bohora.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuagana na  mgeni wake Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin.
PICHA NA IKULU.
KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...