Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Agosti, 2016 amewatembelea na kuwajulia hali Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samuel Malecela Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kuwajulia hali, Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone na kupata nguvu haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida katika ujenzi wa Taifa.Akizungumza na Rais Magufuli nyumbani kwake Salasala Jijini Dar es Salaam spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai amemshukuru Rais Magufuli kwa kumtembelea, kumjulia hali na kufuatilia kwa ukaribu wakati wote alipokuwa akipata matibabu nchini India hadi aliporejea hapa nchini.

"Kwa kweli nimefarijika sana, kwanza naomba nimshukuru sana Mhe. Rais kwa sababu nilipopata matatizo haya ya maradhi alikuwa karibu sana na mimi nikiwa hapa nchini na hata nilipopelekwa nchini India alinipigia simu mara kwa mara na kunifariji sana, na hapa amekuja kuniona kwa niaba ya watanzania kwa kweli namshukuru sana na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa moyo huu wa kuwajulia hali wale wenye matatizo mbalimbali"Lakini niwahakikishie Watanzania, kwamba kwa sasa nina nafuu kubwa sana, naweza kufanya kazi nyingi tu sasa lakini tuendelee kuombeana" Ameeleza Mhe. Ndugai alipokuwa akizungumzia hali yake kwa sasa.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samuel Malecela pamoja na kumshukuru Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli kwa kumtembelea amesema afya yake inazidi kuimarika na pia amewashukuru Madaktari wanaompatia matibabu.

"Mheshimiwa Rais nakushukuru sana, namshukuru pia Mama Janeth Magufuli kwa kunitembelea na kunifariji, naendelea vizuri na matibabu na afya yangu imeimarika kwa kiasi kikubwa" Ameeleza Mhe. Malecela.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es Salaam

16 Agosti, 2016.
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana kwa furaha na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai mara baada ya kuwasili nyumbani kwake Sala sala nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mke wake Mama Janeth Magufuli kushoto akizungumza jambo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai nyumbani kwake Sala sala jijini Dar es Salaam walipokwenda kumjulia hali. Kulia ni mke wa Spika Dkt. Fatma Mganga Ndugai.
 Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akisalimiana na  Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai mara baada ya kuwasili nyumbani kwa Spika Sala sala jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimjulia hali Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela ambaye anapata matibabu jijini Dar es Salaam. 
 Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa pamoja na Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza Sala ya kumuombea Waziri Mkuu mstaafu John Samwel Malecela pamoja na mkewe Anne Kilango Malecela. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na mke wa Spika Dkt. Fatma Mganga Ndugai huku Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiagana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai mara baada ya kuwajulia hali nyumbani kwao Sala sala jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...