Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameishauri Serikali kufuta utaratibu wa kutoa fedha kwa kaya maskini zinazotolewa kupitia Mpango wa Kunusuru kaya maskini TASAF III na badala yake uandaliwe utaratibu wa kuwawezesha wananchi kupata ruzuku ya mbegu na pembejeo nyingine za kilimo.

Mtaka ametoa ushauri huo wakati wa zoezi la uhawilishaji wa fedha katika kijiji cha Itinje wilayani Meatu, ambapo jumla ya shilingi 2,800,000 zilitolewa kwa kaya 77 zinazonufaika na mpango huo.

Mtaka amesema Serikali inatumia zaidi ya Bilioni 400 kwa ajili ya Mpango wa TASAF nchi nzima na wakati huo baadhi ya malengo ya TASAF III yameanza kutekelezwa na Serikali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu bila malipo, utoaji wa huduma za afya bure kwa wazee na Mfuko wa Huduma ya Afya kwa Jamii (CHF) hivyo, malengo ya TASAF yamepungua.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (katikati) akizungumza na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, katika kijiji cha Itinje wilayani Meatu.(hawapo pichani), kabla ya zoezi la uhawilishaji wa fedha kwa wanufaika hao, kutoka kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani.

“Hizi shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa kwa mwaka mmoja kwa Meatu tu, zingetolewa kama ruzuku kwa wakulima wa pamba, mngeweza kupata mbegu bure, dawa bure mkalima pamba na mkapata fedha nyingi kuliko nikiwagawia hizi elfu thelathini, elfu hamsini na watu wengine humo katikati wanaiba hizo fedha, Nitakuwa kiongozi wa kwanza tena kijana kupendekeza huko mbele Serikali ifute mpango huu wa TASAF”, alisema Mtaka.

Mtaka amesema wananchi wanapaswa kusaidiwa njia sahihi za kutafuta fedha kwa ajili ya kujikwamua katika umaskini ikiwa ni pamoja na kujishughulisha na kilimo, ufugaji, ujasiriamali na kupewa fedha ambazo wanufaika walio wengi hawazitumii kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, Mtaka amesema watoto watimize wajibu wa kuwatunza wazazi wao kwa kuwa baadhi ya wanufaika wa mpango wa TASAF III ni wazee waliotelekezwa na watoto wao, hiyo wazee wawakumbushe watoto wao ili wawasaidie kuwatimizia mahitaji muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (kulia) akimkabidhi fedha mmoja wa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, katika kijiji cha Itinje wilayani Meatu, wakati wa uhawilishaji wa fedha kwa wanufaika wa kijiji hicho.

Pamoja na ushauri wake kwa Serikali Mkuu huyo wa mkoa amewataka wanufaika wa mpango huo kujiandaa na kujipanga namna watavyojipatia mahitaji yao muhimu endapo mpango huu utasitishwa na akawataka wajikite katika ufugaji na kilimo cha Pamba na alizeti.

“Nawapa hizi pesa leo ila nawashauri kila mmoja ajipange, ikitokea TASAF inafutwa leo ajue atapataje mahitaji yake ya kila siku. Natamani muwe watu mnaopenda kupata nyavu kwa ajili ya kuvua samaki badala ya kupenda kupewa samaki, hizi pesa zitawalemaza”

Nae Mkuu wa Wilaya ya Meatu Dkt. Joseph Chilongani amesema uhalisia wa utekelezaji wa mpango huo wa kunusuru kaya maskini haujakaa vizuri kwani haoni kama unamuondolea mwananchi umaskini.

Dk Chilongani ameeleza kuwa ni vema fedha hizo zitafutiwe utaratibu mzuri wa kuwasaidia wananchi kupitia vikundi vitakavyojishughulisha na shughuli za kuwaongezea kipato kuliko unavyotekelezwa kwa sasa.

Mpango wa kunusuru Kaya Maskini TASAF III Wilayani Meatu unatekelezwa katika jumla ya kaya 5727 zilizoandikishwa katika vijiji 68 kati ya 106 vilivyopo wilayani humo, ambao kufikia mwezi Agosti 2016, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imeshapokea jumla ya shilingi 1, 793,421,272.73
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza (kushoto) akizungumza na wanufaika wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Itinje wilayani Meatu (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Mratibu wa TASAF Wilaya ya Meatu (hayupo pichani) kuwasilisha taarifa ya Wilaya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Pius Machungwa (wa pili kushoto), akizungumza na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, katika kijiji cha Itinje wilayani Meatu (hawapo pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji wa fedha kwa wanufaika hao kushoto , Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.
Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Itinje wilayani Meatu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (hayupo pichani).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...