Waziri wa Afya.Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (kushoto ) akisisitiza jambo kuhusu umuhimu wa waganga Wakuu wa Hospitali za Umma kusimamia utekelezaji wa Sera na miongozo ya Afya katika  maeneo yao ya kazi.

Na. Aron Msigwa - Dar es salaam. 


Serikali imesema kuwa haitamvumilia Mganga mkuu yeyote wa Hospitali ya Umma atakayebainika kuwatoza fedha wananchi walio katika kundi la watu wanaotakiwa kupata matibabu bure  wakiwemo wazee wasiojiweza, wajawazito na watoto  walio na umri chini ya miaka 5.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo jijini Dar es salaam kufuatia kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wananchi walio katika makundi hayo katika maeneo mbalimbali kudaiwa fedha katika hospitali hizo.

Serikali hatutamvumilia Mganga Mkuu yeyote wa hospitali ya umma anayetoza fedha kwa mwanamke mjamzito, kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 na mzee asiyejiweza, hatujabadilisha Sera " Amesisitiza Mhe.Ummy.

Amesema kwa mujibu wa Sera ya Afya ya 2007 mama wajawazito, wazee wasiojiweza na watoto walio na umri chini ya miaka 5 wanatakiwa kupata matibabu bure na kusisitiza kwamba kuwatoza fedha ni kinyume cha Sera hiyo.

Amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa ambao ndio wasimamizi wa Wakuu wa utekelezaji wa Sera na Miongozo ya Afya katika ngazi ya mikoa kutimiza kikamilifu majukumu yao kwa kushughulikia haraka kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za Afya katika maeneo yao ili wananchi waweze kufurahia huduma bora za afya.

Amesema Serikali inaendelea kuzishughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo changamoto ya uhaba wa dawa ili kuhakikisha kuwa hospitali za umma zinakuwa na dawa za kutosha kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaohudumiwa.

Katika hatua nyingine Mhe. Ummy Mwalimu ameuagiza uongozi wa Taasisi ya Mifupa (MOI) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kusitisha mara moja vitendo vya baadhi ya madaktari wa hospitali hizo kuwaandikia wagonjwa kwenda kufanyiwa uchunguzi wa vipimo katika hospitali binafsi.

 Kuanzia sasa MOI wasimamishe kupeleka wagonjwa kwenda kupima MRI katika hospitali binafsi, pale itakapotokea na tukajua na kujiridhisha kuwa MRI ya Muhimbili imekufa na haifanyi kazi wataruhusiwa kufanya hivyo

Amesisitiza kuwa kitendo cha madaktari hao kuwaandikia wagonjwa kwenda kupima vipimo vya MRI nje ni kuhujumu na kuzikosesha mapato hospitali hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...