Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akifafanua jambo katika eneo la Lwenge, Nyamikoma ambalo ni moja ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhi magwangala.

Na Greyson Mwase, Geita

Mgogoro uliodumu kwa muda mrefu katika mkoa wa Geita kuhusu upatikanaji wa magwangala na eneo la kuhifadhi magwangala hayo, umepatiwa ufumbuzi baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kukutana na mkuu wa mkoa wa Geita, uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), watendaji wa halmashauri ya mkoa huo na wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Profesa Muhongo alifanya ziara katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania John Magufuli lililotolewa Julai 31 mwaka huu la wachimbaji wadogo kupatiwa magwangala pamoja na maeneo ya kuhifadhi magwangala hayo ili kuchenjua na kupata dhahabu.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita. Kulia ni mkuu wa mkoa huo, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga.

Akizungumza katika kikao kilichokutanisha watendaji kutoka Mkoa wa Geita, Wizara ya Nishati na Madini, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Profesa Muhongo alisema maeneo ya awali yaliyopatikana kwa ajilli ya kuhifadhi magwangala hayo ni pamoja na Lwenge- Nyamikoma, Kasota B na Samina B yaliyopo mkoani Geita.

Aliagiza Ofisi ya Madini Mkoani Geita kutoa leseni za uchenjuaji madini mara moja kwa vikundi vyote vya wachimbaji madini ili waanze kazi mara moja ya uchenjuaji madini kwa kutumia magwangala hayo.

“Ninaagiza Ofisi ya Madini Mkoani Geita kutoa leseni za uchenjuaji madini kwa vikundi vilivyoundwa kupitia halmashauri mara moja bila vikwanzo vyovyote ili waanze na shughuli za uchenjuaji madini mara moja,’ alisema Profesa Muhongo. Akizungumzia suala la usafirishaji wa magwangala katika maeneo hayo Profesa Muhongo alisema ni jukumu la vikundi vilivyopewa magwangala hayo kusafirisha kutoka kwenye mgodi hadi kwenye maeneo yaliyoainishwa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga (mbele) akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kubaini maeneo kwa ajili ya kuhifadhia magwangala mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Halmashauri ya Geita.

Aliongeza kuwa iwapo vikundi vitakosa uwezo wa kusafirisha magwangala hayo, halmashauri inaweza kufanya mazungumzo na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa ajili ya gharama ya kusafirisha magwangala hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...