RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi. 
Katika taarifa hiyo aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Alhaj Dk. Shein kwa masikitiko makubwa aliwaarifu wananchi kuwa leo tarehe 14 Agosti 2016, Mzee Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia, msiba ambao umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni, Dar es Salaam.

Alhaj Dk. Shei alieleza kuwa Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na umri wake. 
Kwa taarifa ya Alhaj Dk. Shein, maziko ya marehemu yatafanyika kesho tarehe 15 Agosti 2016 saa 7.00 mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar, Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani. 
Aidha, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kufuatia mchango na juhudi kubwa ambazo Marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga Zanzibar pamoja na nafasi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nchi yetu imekabiliwa na msiba mkubwa kwa kigfo cha kiongozi huyu mahiri”alieleza Alhaj Dk. Shein katika taarifa hiyo. 
Kutokana na msiba huo mkubwa Alhaj Dk. Shein alitangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia kesho tarehe 15 Agosti 2016 ambapo katika kipindi hicho chote bendera zote  zitapepea nusu mlingoti. 
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe marehemu aliutoa wakati wa uhai wake. 

“Tunaungana na Wanafamilia wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Naomba kutumia nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit marehemu mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin. Inalillahi wainnailaihi rajiun” Alieleza Alhaj Dk. Shein katika Taarifa hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiun. Kwa kweli ni msiba mkubwa sana, khusuan kwa wananchi wote wa Zanzibar na Serikali nzima ya Mapinduzi ya Zanzibar kadhalika na Jamuhuri nzima ya Muungano wa Tanzania kwa jumla. Mwenyeez Mungu amughufirie kwa yote Mzee wetu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi, amjaaliye safari ya kheri, ampumzishe palipo pema peponi, ampe kauli thabit na kesho 'Yaumul Hisabu' awe ni miongoni mwa waja wake wema watakaoinga katika yake 'Jannatu Nnaeem' In Sha Allah - AMEN.

    Wawe pole watoto wote wa marehem na familia nzima kwa jumla na kila aliyekhusika ama kuguswa na msiba huu. Dunia ni mapito na sote akhera ndio maishilizio yetu. Wa kizazi hicho tutaukumbuka ule wimbo uliokuwa maarufu sana visiwani tukiimba. "..Tunamuombea Dua Raisi Baba Jumbe akalie kiti chake kwa salama na amani." Leo hii hatunae tena. Pumzika kwa Amani Pema Peponi AMEN.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...