TAASISI ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es salaam jana Jumamosi  imefanya upasuaji mkubwa na  kuweka betri katika moyo wa mtu wa makamo kwa mafanikio. 
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Profesa Mohamed Janabi ameiambia Globu ya Jamii jioni hii kwamba ana furaha kwa kufanikiwa kwa upasuaji huo ambao  amesema umefanyika  mara ya kwanza  kufanyiwa  mtu wa makamo nchini Tanzania.
“Tumeweka kifaa hicho ambacho kitaalamu kinajulikana kama Pacemaker CRTD kwa mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 68 ambaye moyo wake umechoka na hivyo kushindwa kusukuma damu kwenda kwenye mishipa ili isafiri mwilini na yeye aweze kuishi,” alisema Profesa Janabi.

"Hii ni hatua muhimu kwa taasisi hii kwani mafanikio haya yanatupa hamasa ya kuongeza juhudi za kuokoa maisha ya Watanzania wengi hapa hapa nyumbani", alisema Profesa Janabi
Ameongezea kuwa hivi karibuni JKCI  ilifanikiwa kufanya upasuaji mwingine wa kwanza na  kuweka betri katika moyo wa mtoto mwenye umri wa miaka sita.
Mapema Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo hapo JKCI, Peter Kisenge, alisema taasisi hiyo kweli imefanya upasuaji mara nyingi, lakini hawajawahi kufanya upasuaji  wa kuweka betri kwenye moyo wa mtu mzima ambao misuli yake imechoka na haiwezi tena kufunguka, kusukuma damu kwenye mishipa.
 Alisema utendaji kazi wa moyo wa mgonjwa huyo ulikuwa  chini ya kiwango cha asilimia 20 ndio maana mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji huo ili betri hiyo iweze kumsaidia moyo wake kufanya kazi sawa sawa.  
 Dkt Kisenge amesema JKCI imefanya  upausaji huo kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini Kenya.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ni hatua nzuri ya kuboresha zaidi huduma za moyoni, endeleza kazi nzuri.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...