THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

Tanzania kuachana na nguo za mitumba ifikapo mwaka 2018

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Serikali imeazimia kuachana na biashara ya kuingiza nguo za mitumba kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2018.

Maazimio hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama katika uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi ya ushonaji nguo katika kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Company, Ltd.

Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kwamba ifikapo mwaka 2018 soko la Afrika Mashariki halitaingiza nguo za mitumba kutoka nje. 
 Ameongeza kuwa kwa kutekeleza azimio hilo Serikali imeandaa  mafunzo ya kuhakikisha vijana wengi wanapata stadi za kushona nguo nchini ili kuwawezesha kufanya kazi katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zetu wenyewe na kuacha kutegemea bidhaa kutoka nje.

“Tumejipanga kutekeleza azimio hili na kwa kushirikiana na kiwanda hiki tunategemea kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za kubuni mitindo, kukata, kushona na kumalizia nguo” alisema Mhe. Jenista.

Aidha Waziri huyo amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwani mafunzo hayo yatawasaidia kuendana na viwango vya soko la kimataifa na mahitaji ya soko la nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kubuni mitindo, kukata na kushona nguo zenye ubora wa kimataifa.

“Imani yangu kuwa wataalamu waliopo katika kiwanda hiki watawapa ujuzi wa kutosha na wengine wataweza kupata ajira katika kiwanda hiki tumieni fursa hii mliyoipata ni ya pekee kwani mmebahatika kuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza kupata mafunzo chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini. 
Mhe Jenista amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatawezesha vijana kupata ajira katika Viwanda, kujiajiri na hata kutoa ajira kwa wengine hivyo vijana watumie fursa hiyo kutengeneza mtaji na kujiunga katika vikundi vitakavyowawezesha  kufungua viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza nguo na kuendelea kukuza ujuzi waliopata. 

Pia Waziri Jenista ametoa wito kwa viwanda vingine kushirikiana na Serikali kukuza ujuzi kwa vijana kupitia mafunzo ya uanagenzi na kuwahakikisha kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha Vijana kupata mafunzo ya aina hiyo.

“Napenda niwahakikishie kuwa Serikali iko bega kwa bega nanyi, fungueni viwanda vingi sehemu mbalimbali katika nchi yetu, sisi kama Serikali tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha rasilimali watu ya kuendesha viwanda hivi inapatikana” 

Mbali na hayo Serikali inayo mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na kuwa na uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Serikali iliingia makubaliano na kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za kubuni mitindo, kukata, kushona na kumalizia nguo jumla ya vijana 1,089 waliomba nafasi ya kupata mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa awamu tatu na kwa sasa jumla ya vijana 430 wanapata mafunzo hayo.


Kuna Maoni 3 mpaka sasa.

  1. HK Anasema:

    Sina nia ya kubeza au kudharau mpango huo katika maazimio hayo. 2018 panapo uhai na uzima In Sha Allah, nadhani haipo mbali endapo maazimio hayo yamedhamiriwa. Binafsi nadhani itakuwa sio rakhisi kuzuwia kwa ghafla moja, kwani si kama nguo zote za mitumba ni kwamba chakavu au hazifai, la khasha! Ispokuwa pia kumekuwepo tu na mazowea ya kawaida khususan kwa vijana wetu kwenda na wakati katika mavazi yao ambapo 'viwalo' vingi na ambavyo ni 'trend' unakuta kwa wale wenye kipato cha wastani au cha chini, wamekuwa wakiponea huko huko mitumbani ambako hujipatia varieties ya mavazi yao mbali mbali zikiwemo nguo mbali mbali na hata viatu. Wasi wasi wangu juu ya mpango huo mzuri wa kukomesha uingizaji wa nguo za mitumba ifikapo muda huo 2018 ni kwamba, je tutakuwa tayari tumezalisha products za kutosha kulingana na mahitaji ya watumiaji? Je, tutaweza kuwa na varieties mbali mbali zenye kiwango na ubora wa hali ya juu ili kushawishi kukoma kwa uingizaji huo toka nje au tumejiandaaje na hilo maana muda ulioazimiwa ni mfupi sana. Isijekuwa almuradi tu nguo zinazalishwa katika nchi zetu na za kutoka nje zimeshapigwa marufuku huku tukijikuta tunavalishana sare nchi zima huenda kwa pengine kwa kutofikia malengo, mahitaji, ubora na viwango vya product zetu.

  2. Anonymous Anasema:

    Maghufuli na serikali yake wanaweza amethibitisha si mara moja au mbili wanaobeza waache wabeze. Tanzania lazima ijivishe wenyewe ili kuzalisha ajira.

  3. Anonymous Anasema:

    Mdau wa pili hapo juu, hakuna yeyote anaebeza au alosema hawezi na wala aliyepinga suala hilo, kilichoongelewa hapo na mdau wa kwanza ni kuhusu huo muda uliotolewa ambao lazima uendane na kasi ya uzalishaji, ubora na viwango ili soko la nje likitakapofungwa nchi husika ziwe tayari zimeshajitosheleza kukidhi mahitaji ya wananchi wake na si vinginevyo. Muhimu kufikia malengo katika muda ulioazimiwa kwani matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.