THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

TANZANIA YAFANIKIWA KUPUNGUZA IDADI YA WAGONJWA WA TRAKOMA


Na. Aron Msigwa - ARUSHA.

Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Trakoma (Vikope) kufuatia kupungua kwa idadi ya wagonjwa na maeneo yaliyokuwa yakipata dawa za kutibu ugonjwa huo chini ya Kampeni ya utoaji wa dawa kwa watu wengi (Mass Drug Administration) iliyoanzishwa mwaka 1999.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye ufunguzi wa Mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini Arusha, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara hiyo Dkt. Magreth Muhando amesema Tanzania imepata mafanikio hayo kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Sasa hivi wilaya 22 tumeziacha kati ya 56 zilizokuwa zikipata dawa chini ya mpango wa kutoa dawa kwa watu wengi ulioanza mwaka 1999, hii kutokana na kupata mafanikio mazuri na tunategemea kupata mafanikio zaidi kwa kuendelea kuzipunguza zilizobaki Amesema.

Ameeleza kuwa kupungua kwa idadi ya wagonjwa Trakoma nchini Tanzania mwaka hadi mwaka kunatokana na juhudi za Serikali na wadau kupitia afua mbalimbali chini mpango ujulikanao kama SAFE unaohusisha huduma za Upasuaji, utoaji wa dawa za Antibayotiki mapema, kampeni ya kuhamasisha wananchi kuosha uso pamoja na uzingatiaji wa usafi wa mazingira.

Dkt. Muhando amebainisha kuwa Trakoma umekuwa chanzo cha upofu na umasikini pale mgonjwa anapochelewa kutibiwa mapema na kusisitiza kuwa lengo la nchi hizo kukutana nchini Tanzania ni kuweka mkakati wa pamoja wa ushirikiano juu ya namna bora ya kudhibiti maabukizi ya ugonjwa huo kutoka sehemu moja hadi nyingine kutokana sababu za kijiografia na mwingiliano wa watu kutoka nchi moja moja hadi nyingine hali inayoweza kuchangia kusambaza ugonjwa huo.

Amesisitiza kuwa bado watanzania wanalojukumu la kuhakikisha ugonjwa huo unatoweka katika maeneo yao kwa kuzingatia na kufuata kanuni za afya, kufanya usafi wa mwili hususan uso kila siku kwa maji safi na sabuni pamoja na kufanya usafi wa mazingira ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara hiyo Dkt. Magreth Muhando akizungumza kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye ufunguzi wa Mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini Arusha.
Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Upendo John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya kupambana na Trakoma (International Trachoma Initiative) Dkt. Paul Emerson akizungumza katika Mkutano huo ambapo ameipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha ugonjwa wa Trakoma unatokomezwa.

Washiriki wa mkutano huo kutoka nchi 7 za Bara la Afrika wakiwa katika picha ya pamoja.