Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imezitunuku kampuni 86 leseni na vyeti vya ubora baada bidhaa wanazozalisha kukidhi matakwa ya viwango vya shirika.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Egid Mubofu amesema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa sasa kampuni hizo zina fursa zaidi ya kupanua masoko ndani na nje ya nchi.
“Alama hizi hutolewa kwa bidhaa zilizopimwa na kuthibitishwa na kukidhi matakwa ya viwango,” alisema Dkt. Mubofu.
Kampuni zilizopatiwa vyeti hivyo ni za wazalishaji wakubwa, kati na wadogo.  Alama hiyo ni uthibitisho kuwa bidhaa zao  ni salama kwa mlaji na uhifadhi wa mazingira.
Kampuni zilizopata alama hiyo zinatoka katika sekta mbalimbali zikiwemo za usindikaji wa vyakula, uhandisi mitambo na umeme, kemikali, ujenzi na nguo.
Alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuona wazalishaji wadogo na wa kati nao wanakuwa ni sehemu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Alitoa wito kwa wazalishaji ambao bado hawajapata leseni na vyeti vya ubora waendelee kufuata taratibu za shirika ili nao waweze kupata alama hiyo kwa ajili ya usalama wa mlaji na kuyafikia masoko ya ndani na nje.
Afisa Masoko wa Kampuni ya Waja Mabati, Bw. Donasian Massawe alisema cheti cha ubora ni fursa kwao. 
“Alama yetu tumeipata bila ya usumbufu kutokana na huduma nzuri za shirika hili,” alisema Massawe.  Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Watanzania kiko eneo la Kisemvule wilayani Mkuranga, mkoa wa Pwani.
Alifafanua kwamba uchumi wa viwanda unawezekana na kwamba jambo la msingi ni kwa wajasiriamali kujitokeza na kufuata taratibu za kiserikali ili kufanya kazi zao kwa uhuru zaidi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Nafaka Nzima Bakery LTD, Bi. Hesperance Kilonzo alilishukuru shirika hilo kwa kumpatia alama ya ubora na kusema kuwa ataweza kuzalisha na kuyafikia masoko kwa urahisi zaidi.
“Natumia nafaka zisizokobolewa kuzalisha bidhaa kama mikate na keki ambayo ni muhimu kwa afya na maendeleo bora ya ubongo kwa watoto na kujenga afya kwa ujumla,”alisema.
TBS ina jukumu la kuandaa viwango vinavyotakiwa kufikiwa na wazalishaji mbalimbali kabla ya kuingiza bidhaa zao sokoni.

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango (TBS), Dkt. Egid Mubofu (wa pili kushoto) akimkabidhi cheti cha ubora Afisa Masoko wa kampuni ya Waja Mabati, Bw. Donasian Massawe (kulia) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Udhibiti Ubora, Mhandisi Tumaini Mtitu na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Bi. Ashura Katunzi.  Jumla ya kampuni 86 zilikabidhiwa vyeti vya ubora. 
Wazalishaji wa bidhaa mbalimbali wakifuatilia hotuba iliyokuwa ikitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Egid Mubofu katika hafla fupi ya kukabidhiwa vyeti vya ubora kwa kampuni 86 jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...