Baadhi ya mafundi wa kampuni ya kutengeneza ndege ya Bombardier ya nchini  Canada wakiendelea kuipaka rangi moja ya ndege mpya za Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) nchini humo hivi karibuni. Ndege hizo zinatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Septemba mwaka huu zikipishana kwa wiki moja.

Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) limesema ujio wa ndege zake mpya mbili aina ya Bombardier Q400 zinazotarajiwa kuingia hapa nchini siku chache zijazo, utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa shirika hilo, huku shukrani zaidi zikielekezwa kwa Rais John Joseph Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kufufua shirika hilo.

Akizungumza kupitia taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la hilo Muhandisi Patrick Itule alisema ujio wa ndege hizo utalirejesha shirika hilo kwenye biashara ya ushindani dhidi ya makampuni mengine ya ndege hapa nchini.

Ndege hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Bombardier ya nchini Canada zinatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Septemba mwaka huu zikipishana kwa wiki moja.

“Baada ya ujio wa ndege hizi hatuoni tena sababu ya sisi kukwama na tutakuwa tumeingia rasmi kwenye biashara ya ushindani kwa kuwa changamoto kubwa ya uhaba wa ndege ambayo imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa itakuwa imeanza kutatuliwa,’’ alibainisha Muhandisi Itule huku akisisitiza kuwa shirika hilo halitakuwa tayari kuwavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya sasa.

Alisema shirika hilo tayari limeunda kikosi kazi kinachosimamia masuala mbalimbali likiwemo suala la mafunzo ya watendaji wake mbalimbali ili kuendana na matakwa ya biashara hiyo kwasasa.

“Tumejipanga kuboresha mfumo mzima wa utendaji kazi na hiyo ni kuanzia mfumo wa ukataji tiketi na huduma zote muhimu kwa wateja ndio maana kwasasa tunawekeza zaidi kwenye ubora wa rasilimali watu ili kuwavutia zaidi wateja…uvutiaji ambao utaambatana na utoaji huduma kwa gharama nafuu,’’ aliongeza.

Akizungumzia uwezo wa ndege hizo, Afisa Biashara wa shirika hilo Bw Josephat Kagirwa alisema zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na kwamba ujio wake utaongeza njia za kusafiri kwa shirika hilo kutoka njia mbili za sasa hadi kufikia njia zaidi ya kumi.

“Tutakuwa na madaraja mawili yaani daraja la uchumi (Economy Class) litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara (Business Class) litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege. Kwa ujio wa ndege hizi tutaweza kuongeza safari za ndani na baadae mwakani itakapopatikana ndege ya tatu kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi ndipo tutaanza safari za nje ya nchi tukianza na nchi jirani,’’ alibainisha.

Alitaja baadhi ya mikoa ambayo shirika hilo litaboresha zaidi safari zake kuwa ni pamoja na Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Bukoba pamoja na Visiwa vya Comoro. Hata hivyo alisisitiza kwamba safari hizo katika maeneo tajwa na kwingineko zitaanzishwa baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu.

“Lengo ni kuhakikisha tunakuwa tayari kutoa huduma nje ya nchi ndani ya muda mfupi iwezekanavyo ili tuweze kutimiza wajibu wetu kama shirika la ndege la taifa kwa kutangaza nembo ya taifa letu nje ya nchi, kusafirisha watanzania sambamba na kukuza utalii kwa kuwaingiza na kuwasambaza watalii ndani na nje ya nchi kwa urahisi,’’ alisema.

Hata hivyo Bw Josephat alisema mabadiliko hayo yanaambatana na changamoto kadhaa huku akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uhaba wa wataalamu wa kutosha kuendana na kasi waliyojiwekea, gharama kubwa katika uwekezaji wa teknolojia ya kisasa na gharama za vipuri na mabadiliko ya mara kwa mara yanayochangiwa na ushindani katika biashara ya anga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ili kuliunga mkono shirika hili ukizingatia ushindani utakaokuwepo kutoka mashirika binafsi yanayotoa huduma ya usafiri wa ndege, wananchi tutatakiwa pia tuongeze matumizi ya ndege kama njia yetu ya usafiri.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...