Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewatahadharisha wananchi wanaopanga kusafiri kwenda nje ya nchi kuhakikisha kuwa wanafika katika vituo vya afya na kuchanjwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya Homa ya Manjano badala ya kuwalipa fedha baadhi ya watumishi wa afya wasio waaminifu ili watengenezewe kadi hizo kinyume cha sheria.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo jijini Dar es salaam amesema baadhi ya wasafiri wamekuwa wakishirikiana na watumishi wa afya wasiowaaminifu kwa kuwalipa fedha ili waweze kuwatengenezea kadi hizo na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Afya zao.

“Kumekuwa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao hupokea fedha na kisha kutengenezesha kadi za wasafiri zinazoonesha kuwa wamepatiwa chanjo, Jambo hili ni hatari kwa afya ya msafiri, sasa tunaona mlipuko wa ugonjwa huu ukitokea katika nchi za karibu ni muhimu mtu kuchanja ili kuepuka kuwa chanzo cha kuleta ugonjwa huu” Amesisitiza Dk.Neema.

Amesema ni jambo lisilokubalika kwa msafiri kuwa na kadi ya chanjo ya Kinga ya Homa ya Manjano akijua kabisa hajapatiwa chanjo hiyo na kuongeza kuwa jambo hilo linamuweka muhusika katika hatari ya kupata maambukizi akisafiri kwenye nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo.

“Napenda kusisitiza kuwa ni muhimu sana msafiri akachanjwa chanjo hii kwa ajili ya kinga ya afya yake mwenyewe, kupata kadi bila kuchanjwa na kwenda mahali ambapo kuna ugonjwa huu ni kujidanganya, epuka kuwa chanzo cha kusambaza ugonjwa huu” Amesisitiza Dk. Neema.

Kuhusu gharama za chanjo hiyo amesema kuwa msafiri anayetaka kupata chanjo hiyo anatakiwa kulipia gharama ya Elfu Ishirini (20,000/=) ikiwa ni malipo halali ya Serikali na mlipaji hupatiwa stakabadhi halali.

Aidha, amesema mbali na hatua zinazochukuliwa kudhibiti hali hiyo, Wizara inakamilisha utaratibu wa kuwa na kadi maalum ambazo zitakuwa tofauti, zenye nembo maalum ambazo mtu hataweza kughushi wala kufanya udanganyifu wa aina yoyote.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi kuhusu Chanjo ya Homa ya Manjano na vitendo vya baadhi ya watumishi wa afya wasiowaaminifu ambao hulipwa fedha ili waweze kuwatengenezea wasafiri kadi za Chanjo ya Homa ya Manjano na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo ambalo kinyume cha sheria na hatari kwa usalama wa Afya zao. Picha/Habari na Aron Msigwa – MAELEZO. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...