Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo kwa wataalam wa TEHAMA wanaosimamia miradi chini ya Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP) Tanzania katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Arnold Mathoyo akieleza utaratibu wa mafunzo ya TEHAMA kwa washiriki wanaosimamia miradi ya TEHAMA chini ya Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP) Tanzania katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma.
Washiriki wa mafunzo kuhusu TEHAMA wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi (hayupo pichani).
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi i akifungua mafunzo kwa wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wanaosimamia miradi chini ya Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP) Tanzania katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma.
Usimamizi na utekelezaji wa Serikali Mtandao unahitaji Rasilimaliwatu
yenye weledi mkubwa wa kusimamia maeneo ya msingi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Bi. Susan Mlawi alisema hayo mkoani Dodoma wakati
akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa miradi mbalimbali ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotekelezwa chini ya Mradi wa
Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP) Tanzania.
“ Rasilimaliwatu katika eneo hili inahitaji kupewa mafunzo na kuendelezwa
katika nyanja muhimu za usimamizi wa TEHAMA na pia kuwa na uwezo na
uelewa wa mifumo na taratibu za utendaji kazi katika Taasisi za Umma” Bi.
Mlawi alisema.
Bi. Mlawi alifafanua kuwa, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa lengo
la Serikali la kuwajengea uwezo wataalam wake ili kuboresha utekelezaji
wa miradi ya Serikali Mtandao yenye lengo la kuziwezesha Taasisi za
Umma kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yamelenga kuongeza uwezo kwa wataalam
wa Serikali hususani katika Ununuzi na usimamizi wa utekelezaji wa
mifumo na mitandao mbalimbali ya TEHAMA inayowekwa katika Taasisi za
Serikali ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa Umma.
Bi. Mlawi aliainisha kuwa uteuzi wa washiriki wa mafunzo hayo
umezingatia ushiriki katika utekelezaji wa miradi ya RCIP na matokeo ya utafiti wa mahitaji ya mafunzo kwa maafisa TEHAMA wa Taasisi za Serikali,
uliofanywa na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) mwezi Septemba, 2015.
Alisisitiza kuwa, kila mshiriki atajengewa uwezo wa kiufundi kulingana na
mahitaji halisi katika eneo au maeneo ya kusimamia na kutengeneza
mifumo ya TEHAMA.
Naibu Katibu Mkuu huyo Bi. Mlawi, alielekeza washiriki wa mafunzo hayo
wahakikishe ujuzi watakaoupata unawafikia wale ambao hawakubahatika
kuchaguliwa kwa sababu idadi ya washiriki walioteuliwa kuhudhuria
mafunzo ni ndogo ikilinganishwa ya idadi kubwa ya Maafisa TEHAMA
waliopo katika Taasisi za Serikali ili kwa pamoja washirikiane kubuni
mifumo ya TEHAMA yenye kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa
umma.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina
jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya RCIP eneo la
Mifumo ya Serikali Mtandao “e-Government Applications” ambapo mifumo
mbalimbali ya TEHAMA (ya Kimkakati na ya Kisekta) inaendelea kuwekwa
na kutekelezwa katika Taasisi walizotoka washiriki wa mafunzo.
Mifumo hiyo ni Mfumo wa Wakala ya Usajili, Vizazi na Vifo (Birth and
Death Registration System) kupitia Wakala ya RITA; Mfumo wa Taarifa za
Biashara (National Business Portal) kupitia Wizara ya Viwanda na
Biashara, Mfumo wa Taarifa za Kitabibu (Telemedicine system) kupitia
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mfumo wa Taarifa za Ununuzi (e-
Procurement system) kupitia Mamlaka ya Uthibiti wa Ununuzi wa Umma
(PPRA) na Bohari ya Dawa (MSD), Mradi wa “electronic Records” kupitia
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na; Mradi wa “electronic Office”
kupitia Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, na Wakala ya
Serikali Mtandao (eGA).
Mafunzo hayo yatatolewa kwa Maafisa, Wasimamizi wa miradi 62; Wakuu
wa Vitengo vya TEHAMA 15 na Maafisa Ugavi 50 kutoka kwenye Taasisi
mbalimbali za Serikali na yatafanyika kwa awamu 5 katika ukumbi wa
Mikutano wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...